BAADA YA DC WA KAHAMA NA MWENYEKITI WA CCM KUVURUGANA_ WAHANGA WA MVUA YA MAWE WAFUNGA BARABARA KUZUIA MAGARI YOTE


Jinsi Magari yalivyozuiwa katika eneo hilo-picha kwa hisani ya Dunia Kiganjani blog

Abiria wanaokwenda mikoa ya Mwanza, Singida na Dar es salaam na Kwingineko na wale wanaokwenda mikoa ya Kigoma na magari yote yanayokwenda nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda na Congo, wamekwama baada ya wananchi wa kijiji cha Mwakata Kata ya Isaka wilayani Kahama kufunga barabara kuu ya kwenda maeneo hayo asubuhi hii.

Taarifa kutoka eneo la tukio zinasema kuwa wahanga hao wa janga la mvua ya mawe  na upepo iliyoua watu 46 na kujeruhi wengine zaidi ya 90, wameifunga barabara hiyo kuishinikiza serikali kuwapa misaada ya chakula na malazi.

Inaelezwa kuwa misaada ambayo imetolewa katika maeneo mbalimbali na kwamba serikali ya eneo hilo haijagawanya wahanga wanaohusika badala yake kupewa watu wengine.
Mpaka sasa mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Kahama ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo Benson Mpesya ameshaenda eneo la tukio ili kuwasikiliza wananchi hao na kujaribu kumaliza tatizo hilo.


Hata hivyo habari tulizozipata hivi punde zinasema kuwa tayari jeshi la polisi wilaya ya Kahama limefika katika eneo la tukio na kutumia mabomu ya machozi bila kuathiri wananchi na kufanikiwa kuwatawanya na kufungua barabara ambapo tayari magari yameanza kupita.

Ikumbukwe kuwa juzi Alhamisi Waziri mkuu Mizengo Pinda alikwenda kuzuru eneo hilo lililokumbwa na maafa hayo kwa ajili ya kutolewa kwa misaada ya kibinadamu, ambapo pia mazao shambani na vyakula vilivyokuwa majumbani pamoja na mifugo vimeathiriwa.

Tukio la kufungwa kwa barabara limekuja siku moja tu baada
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja kuibuka na kudai kusikitishwa na utendaji kazi wa mkuu wa wilaya ya Kahama Benson Mpesya kwa kushindwa kusimamia kikamilifu kamati ya ugawaji chakula na vifaa hali iliyosababisha waathirika wa mvua ya mawe na upepo katika kijiji cha Mwakata wilayani Kahama,kugombea chakula na kulalamikia kuuzwa kwa magodoro na branketi zilizotolewa misaada na wahisani.

Hayo yamejiri Jana Ijumaa wakati kamati ya maafa ya mkoa ikipokea misaada kutoka taasisi mbalimbali za fedha, mashirika na watu binafsi walioguswa na kutoa misaada ya chakula, magodoro na nguo.

 Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja alisema kuwa endapo utendaji wa wakuu wa wilaya kama alivyo mkuu wa wilaya ya Kahama usipobadilika Chama Cha Mapinduzi kitapata wakati mgumu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa kuwa baadhi yao hawaendani na sera ya chama.

Akijibu tuhuma hizo mkuu wa wilaya ya Kahama Benson Mpesya alisema kuwa yeye hausiki na upotevu wa vifaa vinavyodaiwa kuibiwa na kuuzwa kwa watu wasiohusika na kusema kwamba rawama hizo zielekezwe kwenye kamati ya maafa ya ugawaji.

Kufuatia hali hiyo mkuu wa mkoa wa Shinyanga Ally Nasoro Rufunga alilazimika kuingilia kati mgogoro huo na kuwaita wote kwa pamoja katika kikao cha zarula ambapo hakutaka kubainisha hatua zilizochukuliwa na kusema kwamba serikali imepokea maagizo ya kiongozi wa chama cha mapinduzi na kuyafanyia kazi kwa lengo la kuhakikisha waathirika wanapata huduma inayositahili.


ANGALIA PICHA ZAIDI LA TUKIO LA WANANCHI KUFUNGA BARABARA HAPA 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم