KAMATI
Kuu ya CCM (CC) imewasimamisha uongozi wa vikao vya chama, vigogo
watatu wa chama hicho, akiwemo Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka kutokana na kuhusishwa na
sakata la Escrow.
Wengine
waliosimamishwa kuhudhuria vikao vinavyohusu uamuzi wa chama ni pamoja
na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na Mbunge wa Sengerema,
William Ngeleja.
Hatua
hiyo inatokana na uamuzi wa Kamati Kuu iliyoketi Januari, mwaka huu
Zanzibar, kuagiza Kamati ndogo ya Maadili kuwaita na kushughulikia suala
la viongozi wa chama hicho, waliokuwemo katika vikao vya uamuzi ya
chama hicho waliohusishwa na sakata la Escrow.
Akitoa
taarifa ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichofanyika Ikulu Dar es
Salaam jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa
(NEC) ya CCM, Nape Nnauye alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya Kamati
ya Maadili inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho (Bara),
Philip Mangula kuwahoji vigogo hao.
Alisema
Kamati hiyo ya Maadili iliwasilisha ripoti yake kwa Kamati Kuu jana,
ndipo ukafikiwa uamuzi wa vigogo hao kusimamishwa kuhudhuria vikao vya
chama vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu kwa Profesa Tibaijuka na
Halmashauri Kuu kwa Chenge na Ngeleja.
“Uamuzi
wa Kamati Kuu ni kuwasimamisha uongozi wao kwenye vikao vya chama,
kwamba wasihudhurie vikao vya chama vya Kamati Kuu kwa yule mjumbe wa
Kamati Kuu na Halmashauri Kuu kwa wajumbe wake, kwa kipindi ambacho
Kamati hii ndogo ya Maadili wakiendelea kupitia nyaraka mbalimbali
zinazohusu suala hili,” alisema Nape.
Akizungumzia
vigogo sita wa chama hicho waliokuwa kwenye adhabu baada ya kuthibitika
kukiuka maadili ya Chama na kuanza kampeni mapema, Nape alisema
tathimini ya mwenendo wao bado inaendelea.
Vigogo
hao ambao tathimini ya mwenendo wao bado inaendelea, ni pamoja na
waliokuwa mawaziri wakuu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye na Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wengine
ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba,
ambaye ameshatangaza nia ya kugombea urais, Waziri wa Kilimo na
Ushirika, Stephen Wasira na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Alisema
kanuni za usalama na maadili ya chama iliyotumika kuwahukumu, ni
inayosema onyo kali alilopewa mwanachama, maana yake atakaa chini ya
uangalizi kwa kipindi kisichopungua miezi 12.
“Sasa
baada ya ile miezi 12 kuisha, kamati ndogo ya maadili inaendelea na
kazi yake ya kuchunguza mienendo ya hao waliokuwa wamepewa adhabu,
katika kipindi chao cha adhabu ya miezi 12 wametekeleza masharti ya
adhabu zao,” alisema.
Alisema
baada ya hapo, kamati hiyo itawasilisha ripoti ya uchunguzi wake kwa
Kamati Kuu ambapo kama kutakuwa na taarifa yoyote, itatolewa kwa umma.
Aidha,
Nape alitumia fursa hiyo kuwaonya baadhi ya wanasiasa wengine
waliojitokeza na kutangaza nia zao za kugombea urais kwa kuvunja sheria
na taratibu za chama hicho, wasije kukilaumu chama hicho.
“Kila
mmoja ambaye atavunja kanuni katika mchakato mzima wa kutafuta
kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi, atachukuliwa hatua, hakuna atakayepona
katika mkono wa sheria na taratibu za chama kama atazivunja, ni suala
la muda kama kuna mtu anaendelea kuvunja.
“Msisitizo
wa Kamati Kuu ni kwamba watu wote wanaotaka uteuzi wa chama, wafuate
taratibu ili tusije tukalaumiana baadae, kwa sababu wakati mwingine
wanadhani ni suala la Nape au Katibu Mkuu kuwa mkali, hii ni kanuni,
hakuna atayepona.
“Hili suala la watu sita lilianza muda mrefu, lakini
yapo maneno wako na wengine wanavunja sheria na taratibu lakini, msimamo
wa chama hiki hakuna atakayevunja sheria akaachwa salama,” alisema.
Social Plugin