SERIKALI ya Kaunti ya Elgeyo Marakwet inakabiliwa na
changamoto kubwa ya kuwatuma wafanyakazi katika kituo cha afya cha
Simbeiwe, kaunti ndogo ya Marakwet Magharibi, baada ya wahudumu wa afya
wanaotumwa hapo kukataa kazi kwa kuhofia uchawi eneo hilo.
Kumekuwa na imani kwamba eneo hilo
ni kitovu cha uchawi katika kaunti huku wafanyakazi wakipata habari za
kuogofya kwamba mazimwi pia hutafuta matibabu katika kituo hicho.
Mmoja wa wauguzi aliyeacha kazi
katika kituo hicho aliripotiwa kutibu 'zimwi’ la kike ambalo lilifanya
muujiza kwa kuning’iniza mtoto mdogo hewani, bila kumshika, mbele ya
muuguzi huyo ambaye alikuwa akijitayarisha kumdunga sindano.
Waziri wa Afya katika kaunti hiyo,
Bw Thomas Ruto alisema idara yake inatafuta wahudumu wa afya ambao
wanaweza kustahimili kazi katika mazingira kama hayo.
Lakini Mwakilishi wa Wadi ya
Moiben-Kuserwo William Chesing’any, alipuuza madai hayo akisema kuwa
uchawi uliendeshwa na kizazi cha zamani ila kwa sasa haupo.
“Imani hiyo inaendelea kufifia. Sasa
tuna watumishi wa umma ambao ni pamoja na walimu wanaofanya kazi
Simbeiwet na Mindiliwo. Desturi hiyo inastahili kusahaulika,” alieleza.
Kwingineko, mhudumu mwanamume katika
kaunti hiyo amechukuliwa hatua kwa kuhamishwa kufuatia madai kuwa
alitaka kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wagonjwa wake.
Hii inafuatia hatua ya wakuu katika
lokesheni ndogo ya Kapcherop, Marakwet Magharibi, kupiga marufuku
wanawake wote na wasichana kutafuta huduma za kimatibabu katika
dispensari inayosimamiwa na mhudumu huyo anayetajwa kama mtundu.
Wakuu wa kaunti pia wanatazamia
kuchukua hatua zaidi dhidi ya mhudumu huyo ambaye amedaiwa kutaka kutoa
huduma za ziada kando na zile ambazo wagonjwa wa kike wanatafuta.
Marufuku yao ilifuatia malalamishi
kutoka kwa wagonjwa wa kike kwamba mhudumu huyo alikuwa na mazoea ya
kuwapapasa sehemu zao za siri akiwa anawahudumia hata kwa maradhi kama
mafua.
“Hata wakati mtu akitaka matibabu ya
mafua, yeye angempapasa kwa mkono wake kuanzia shingoni hadi kwa mapaja
kupima joto la mwili,” mmoja wa wakazi alilalamika.
Kudhihirisha madai
“Mwanamke aliyetumiwa na viongozi
kutafuta matibabu katika kituo hicho ili kudhihirisha madai hayo,
alithibitisha tabia ya muuguzi huyo, ambaye alijaribu kumwandama kingono
na nia nyinginezo ambazo hatuwezi kueleza,” alisema Bw Ruto.
Viongozi hao pia walibaini kuwa
kituo hicho kimetorokwa na wakazi wa kike ambao wameshauriwa na waume
wao na wazee wa kijiji wasisogee karibu na mhudumu huyo.
Dawa kadhaa zilizoharibika pia zilipatikana katika kituo hicho.
Afisa mkuu wa afya katika kaunti, Bi
Caroline Magut alitaja tabia ya mfanyakazi huyo kama isiyoamabatana na
maadili, kukosa utaalamu na pia ya kushangaza.
“Tumechukua hatua ya kinidhamu na
kwa sasa tunaendelea kumfuatilia kwa karibu. Tumemhamisha hadi katika
kituo chenye shughuli nyingi huku mipango ya kumuondoa kazini
ikitayarishwa,” alisema Bi Magut
Social Plugin