| ||
Mheshimiwa Freeman Mbowe akisalimiana na mkuu wa mkoa wa Shinyanga Ally Rufunga,wa kwanza kulia ni mkuu wa wilaya ya Kahama Benson Mpesya |
Mwenyekiti
wa CCM mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja akijiandaa kukabidhi msaada wa
fedha kwa niaba ya waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa.
|
VIONGOZI wawili wa
kisiasa nchini wameungana na watanzania wengine katika kuwapa pole na
kuwafariji wahanga wa mvua kubwa ya mawe iliyonyesha na kubomoa nyumba kadhaa
za wakazi wa kijiji cha Mwakata wilayani Kahama mkoani Shinyanga na kusababisha
vifo vya watu 47 huku familia 450 zikibaki bila makazi.
Viongozi hao ni pamoja na mwenyekiti wa Taifa wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na waziri mkuu mstaafu
Edward Lowassa ambao kwa ujumla wao walikabidhi msaada wa fedha jumla ya shilingi
milioni 15.
Akikabidhi msaada kwa niaba ya familia ya waziri mkuu
mstaafu, Edward Lowassa, mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani
Shinyanga, Khamis Mgeja alisema mara baada ya kutokea kwa maafa yaliyotokea,
waziri mkuu mstaafu na familia yake waliguswa na tukio hilo na hivyo kuona
umuhimu wa kuwasaidia wahanga wa maafa hayo.
“Mheshimiwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga na wakazi wote
wa kijiji cha Mwakata, kwa niaba ya familia ya waziri mkuu mstaafu Edward
Lowassa, naomba nikabidhi msaada wa shilingi milioni tano kwa ajili ya wahanga
waliokumbwa na tatizo hili ikiwa ni pole na rambirambi kwa familia ya watu
waliopoteza maisha,”
“Binafsi yeye mwenyewe alikuwa aje lakini kutokana na
majukumu aliyonayo ameniomba mimi mjumbe mwenzake wa Halmashauri Kuu ya Taifa
ya CCM (NEC) nifikishe salaam za pole na mchango wa kusaidia matatizo
yaliyojitokeza hapa, pia ameniomba niwaeleze kuwa anaungana na watanzania wote
kutoa pole zake za dhati kwa janga hili lililotokea,”
“Anasema yeye yuko pamoja nanyi na anaungana na
watanzania wengine wote na kwamba janga hili siyo lenu peke yenu bali ni la
watanzania wote na ameahidi kuendelea kushirikiana nanyi kwa hali na mali mpaka
pale hali zenu zitakaporejea kuwa za kawaida, na pia anatoa pole kwa uongozi wa
serikali mkoani Shinyanga,” alieleza Mgeja.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CHADEMA wa Taifa Freeman Mbowe
mbali ya kukabidhi msaada wa shilingi milioni 10 kwa niaba ya chama chake
aliwataka watanzania wote hasa viongozi wa CCM kutochanganya mambo ya siasa
pale panapotokea janga lolote la kitaifa na kwamba tukio la Mwakata ni janga la
Taifa.
Mbowe alisema kwa kawaida maafa yanapotokea hayana
itikadi ya chama chochote cha siasa na kwamba si vizuri kwa viongozi wa vyama
vya kisiasa kugeuza maafa ya kitaifa kuwa mashindano ya kisiasa na hakuna
sababu yoyote ya kushindana kuona nani katoa zaidi katika kuwafariji wahanga.
“Ndugu zangu sisi CHADEMA tumeguswa sana kwa tukio
hili, kwa hali hiyo tumeona tutoe kitu kidogo ili kuwasaidia wenzetu
walioathiriwa na mvua hii kubwa, kwa sasa tutatoa shilingi milioni 10 ambazo
hata hivyo tutaomba mtueleze ni vitu gani mnavyohitaji, kama ni vifaa au
vyakula mtueleze,”
“Tunasema hivi kwa sababu tunaweza kuja na unga hapa
kumbe kinachohitajika ni mafuta ya kula, au tukaja na maharagwe kumbe wengine
wameishaleta ya kutosha na kinachohitajika ni mabati au mifuko ya saruji, hivyo
baada ya msaada huu wa leo, tunatarajia kufanya mkutano mkubwa mjini Kahama kwa
ajili ya kuchangia wahanga,” alieleza.
Akipokea misaada hiyo mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Ally
Rufunga aliwapongeza waziri mkuu mstaafu Lowassa na Mbowe kwa jinsi
walivyoonesha kuguswa na tukio hilo na kwamba misaada waliyoitoa itasaidia
kupunguza makali ya matatizo yaliyojitokeza baada ya mvua kubwa iliyoleta
madhara kwa wakazi wa Mwakata.
“Kwa niaba ya mkoa wa Shinyanga tunawashukuru wote
walionesha moyo wa upendo wa kuwasaidia wahanga hao, na kwa upande wa
mheshimiwa Mbowe nikupongeze binafsi kwa jinsi ulivyoamua kuweka kando masuala
ya kisiasa na kutanguliza mbele uzalendo, tunakushukuru sana, mpaka sasa
tunaendelea kupokea misaada mbalimbali kwa ajili ya kaya 649 zilizoathiriwa na
mvua hiyo,” alieleza Rufunga.
Mpaka Machi 9, mwaka huu idadi ya watu waliokufa
kutokana na mvua kubwa ya mawe iliyopewa jina la Tornado iliyonyesha hivi
karibuni ilifikia watu 47 baada ya majeruhi mwingine aliyekuwa amelazwa katika
hospitali ya serikali mjini Kahama kufariki dunia juzi. Majeruhi wanne walikuwa wakiendelea na
matibabu katika hospitali rufaa ya Bugando jijini Mwanza.
BOFYA HAPA KUONA PICHA ZAIDI
BOFYA HAPA KUONA PICHA ZAIDI
Social Plugin