Watu
watano katika Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza wamenusurika kifo baada
ya kuangukiwa na kifusi wakati wakiwa kwenye maandalizi ya kujenga jengo
lililotegemewa kuwa na ghorofa saba, eneo la Nyerere Road, leo majira
ya saa sita mchana.
Akizungumza
na waandishi wa habari eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,
Baraka Kunisaga amesema kuwa amesikitishwa na tukio hilo ambapo watu hao
wameangukiwa na ukuta wakati wakijenga msingi wa jengo hilo na hii ni
kutokana na kuwa na wakandarasi ambao hawajengi majengo kwa kiwango
kinachotakiwa.
Katika
hatua nyingine, Kunisaga amesema kuwa hali ya Watanzania kuwa
wanapoteza uhai wao kila kukicha kutokana na kuangukiwa na vifusi,
serikali haiwezi kukubaliana nayo hivyo amesitisha ujenzi wa jengo hilo.
Majeruhi
waliokumbwa na tukio hilo wameongea na waandishi wa habari japo kwa
taabu na kusema kuwa ukuta uliowaangukia ulikuwa umeunganishwa kama uzio
hivyo wakati wakiendelea kuchimba msingi, uzio huo ulikuwa ukiendelea
kutitia hivyo kusababisha kuporomoka na kuwaangukia.
Daktari
wa zamu wodi ya dharura, Ernest Elisenguo amethibitisha kupokea
majeruhi watano ambao wametokana na tukio la kuporomokewa na kifusi na
kuwataja kuwa ni Ramadhan Hussein Nyarandu, Rashid Mkumba Hamis, Elias
Bahati, Benson Agustino na Mtani ambapo watatu kati ya hao hali yao
imeendelea vizuri na wameruhusiwa kwenda nyumbani ila wawili kati yao
bado hali zao siyo nzuri na wataendelea kuwa chini ya uangalizi wa
madaktari.
Majeruhi
Rashid Mkumba Hamis, ameeleza kama ifuatavyo: "Mimi ni fundi na
nilikuwa natengeneza 'bezi' kwa ajili ya kushikilia nguzo za ghorofa
wakati ninaendelea na kazi yangu nikaanza kusikia udongo ukiniangukia
mgongoni, ghafla nikasikia matofali yananiangukia.
Katika
kujiokoa matofali yakawa yameniangukia kwenye miguu na bahati mbaya kwa
mujibu wa madaktari ni Kwamba nimevunjika mguu ila namshukuru mungu
kuona niko salama."