Jeshi la Polisi Mkoani
Shinyanga limewakamata waganga wa tiba asilia 26 katika wilaya za
Kishapu,Shinyanga na Kahama katika msako mkali wa kuwasaka na kuwabaini waganga
wa jadi wanaojihusisha na shughuli za upigaji ramli chonganishi wanaotajwa
hujihusisha na mauaji ya albino nchini.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Shinyanga, Justus Kamugisha alisema operesheni ya kuwakamata waganga hao
iliendeshwa katika wilaya za Kahama, Kishapu na Shinyanga kuanzia Machi mosi
hadi Machi 9, mwaka huu ambapo baadhi ya waganga hao wanatuhumiwa kujihusisha
na mambo ya ukataji mapanga.
Kamanda Kamugisha alisema,
operesheni hiyo ilihusisha kuwapekua, kuwahoji na kisha kuwafikisha mahakamani
wale wote waliobainika kujihusisha na upigaji wa ramli chonganishi ambapo
baadhi yao walikutwa wakiwa na vifaa vya kupigia ramli hizo wakiwemo wanaojihusisha
na ukataji mapanga vikongwe.
Alisema, katika msako huo
waganga hao walikamatwa pia wakiwa na nyara mbalimbali za serikali, ikiwemo ngozi
za fisi, kicheche, nyani,nyati, simba, nyegere, korongo, digidigi, kitovu cha mbweha
na mikia ya nyumbu, pembe na viungo mbalimbali vya wanyama wa aina tofauti
tofauti ikiwemo vibuyu vilivyovishwa shanga.
Vifaa vingine ni mafuvu ya mbwa,vioo vya kupigia ramli,ngozi ya kalunguyeye,mwewe,mifupa na ndege pori,visu,vyuma,nyoka,mikuki,shanga na vitu vingine vya ajabu ajabu.
Kamanda Kamugisha aliwataja
waganga waliokamatwa, kuwa ni Ester Madirisha (65) mkazi wa Mwalukwa, Selekwa
Nicholaus (42) mkazi wa Mwang’osha, Siyantemi Jinasa (41) mkazi wa kijiji cha
Ibubu, Fatuma Shija (47) mkazi Ngogwa Kahama, Makandi Guma (51) mkazi wa Ibubu
na Gamaweshi Mayala (49) mkazi wa kijiji cha Lubaga.
Wengine waliokamatwa ni,
Saimon Lukelesha (34), Jidanda Samanya (20) na John Lubanga (28) wote wakazi wa
mkoa wa Tabora, Samwel Zengo (37) mkazi wa Lagana, Jimoka Jitobelo (93) mkazi
wa Ibingo, Shija Venji mkazi wa Ibingo Samuye, Milembe Ndahya (50) mkazi
wa Isela, Kashinje Nyakali (55) mkazi wa Samuye na Nzela Maige (55) mkazi wa
Isela Samuye.
Akifafanua Kamanda
Kamugisha alisema, katika msako huo watu wanne walikamatwa wakituhumiwa kwa
makosa ya kujihusisha na ukataji mapanga, ambao ni John Sabuni (45) mkazi wa
Shinyanga, James Machimanya (34) “Jaji”mfanyabiashara mkazi wa Kishapu, Jackson
Charles (55) mkazi wa Shinyanga, Juma Ndodi (50) mkazi wa kijiji cha Buyange.
Wengine waliotajwa kuwa ni
Kashinje Kayila (46) “Ntelezu”, Tabu Salamba (43) “Mandago” wote wakazi wa
kijiji cha Ngaganulwa kata ya Usanda, Itwelyamhela Shija (28), Jilala
Maige (44) wote wakazi wa kijiji cha Singita kata ya Usanda, Nyanzobe Shija
(36), Mbula Maduka (57), Masalu Nkuba (53) na Lugonda Kwangu (45) wote wakazi
wa Ibadakuli Shinyanga.
Hata hivyo kamanda
Kamugisha alisema, mpaka hivi sasa jeshi la
polisi linaendelea kumsaka mganga mmoja Milembe Shinji mkazi wa kijiji
cha Ibingo ambaye hajakamatwa kutokana na kutoweka nyumbani kwake wakati
opereshini hiyo ilipokuwa ikiendelea ambapo upekuzi ulifanyika katika nyumba
yake na kukamatwa kwa vifaa kadhaa ikiwemo nyara za serikali.
“Wote hawa baada ya
kuwafanyia mahojiano tayari wamefikishwa mahakamani ambako wamesomewa mashitaka
yao ya kujihusisha na vitendo vya upigaji ramli chonganishi na ukataji wa
mapanga ikiwemo kupatikana na nyara za serikali wanazozimiliki bila vibali vya
serikali, operesheni hii bado inaendelea katika maeneo mbalimbali ya
mkoa," alisema Kamugisha.
Na Kadama Malunde-Shinyanga
Social Plugin