Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Udasi mwambao mwa Ziwa Tanganyika, kata ya Kabwe wilayani Nkasi mkoani Rukwa, Ismail Ndomboya (42) amenusurika kuuawa na mamba kwa kupambana kijasiri na mnyama huyo kwa zaidi ya nusu saa.
Hata
hivyo, licha ya kuokoa maisha yake mnyama huyo katika mapambano
hayo alimng’ata na kumnyofoa mkono wake wa kushoto na kutokomea
nao ziwani.
Diwani
wa Kata ya Kabwe, Asante Lugwisha akizungumza na mwandishi wa habari
hizi kwa njia ya simu alithibitisha kutokea kwa mkasa huo uliotokea
juzi saa moja na nusu jioni wakati Ismail alipokuwa akioga katika
Ziwa Tanganyika kijijini Kabwe .
Akisimulia
mkasa huo, Diwani Lugwisha alibainisha kuwa jioni hiyo ya tukio
Ismail aliamua kwenda kuoga ziwani wakati huo akiwa pekee ndipo
ghafla mamba alimvamia ghfla na kumuuma mkono wake wa kulia.
“Kwa
ujasiri mkubwa Ismail alipambana kufa au kupona na mnyama huyo kwa
nusu saa huku akipiga yowe akiomba msaada lakini hakuna
aliyejitokeza kumsaidia kwa sababu sehemu aliyokuwa akioga ilikuwa
mbali na makazi ya watu,“ alieleza.
Aliendelea
kueleza kuwa hatimaye mamba aliunyofoa mkono wa kushoto wa Ismail
na kutokomea nao ziwani ndipo Ismail alipokimbia kuelekea
nyumbani kwake akiwa uchi.
“Baadaye
nilitaarifiwa kuwa Ismail ameshambuliwa na mamba wakati akioga
ndipo nilipofika nyumbani kwake, na tulijipanga tukamkimbiza katika
Hospitali Teule ya Wilaya (DDH) mjini Namanyere ambao tulifika saa
nne na nusu usiku ambako amelazwa kwa matibabu “ alieleza.
Mtaalamu
wa afya wa Hospitali ya Wilaya, ambaye alikiri kuwa si msemaji,
alikiri kupokelewa kwa mgonjwa huyo aliyejeruhiwa na mamba ambapo
aliielezea hali yake kuwa inaendelea vizuri.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Rukwa , Jacob Mwaruanda amethibitisha kutokea kwa
mkasa huo na kwamba uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.
Social Plugin