1. UTANGULIZI
Ni kawaida unapopita mitaani au sehemu mbalimbali mijini au vijijini
hasa kwa wingi kabisa katika miaka ya hivi karibuni kuona maneno kama
…………COMPANY LTD. Sijui kama uliwahi kujiuliza maana ya neno hili
limited (LTD).
Pasi kuwaongelea raia wa kawaida wa wamitaani ambao
husoma neno hili katika mbao za matangazo na kwenye mabango mbalimbali
ya kibiashara ambayo hubandikwa mitaani au nje ya ofisi mbalimbali, wapo
watu ambao wana makampuni na wanalitumia pia neno hili lakini
ikawezekana wakawa hawajui hata maana yake.
Ni wakati sasa wa kufahamu maana na matumizi ya neno hili. Awali ya
yote ni vyema kufahamu kuwa neno hili lina maana kisheria na limewekwa
kwa mujibu wa sheria na matumizi yake ni ya kisheria. Unapolikuta pahala
ujue halijakaa bahati mbaya au halijawekwa kwa ajili ya urembo au
kupamba matamshi.
2. NINI MAANA YA NENO LIMITED ( LTD )
Kwa tafsiri ya moja kwa moja ya kiswahili twaweza kusema Limited ni
kikomo, ukomo, au mipaka. Zote ni maana za neno hilo na hutumika kwa
utofauti kutokana na kinachoelezwa. Katika makala haya tutatumia neno
ukomo ili kumaanisha Limited.
Katika sheria hasa sheria ya Makampuni ambayo hasa ndio inaangaziwa
leo neno limited linapotumika humaanisha ukomo wa hatia au ukomo wa
uwajibikaji wa wanachama katika kampuni( Limited Liability ).
Ni kwa
namna gani kuna ukomo wa uwajibikaji kwa wanachama katika kampuni na
katika lipi wanawajibika tutaona baadae.
3. AINA ZA LIMITED ( LTD ) .
Ni vyema kufahamu kuwa Limited nazo zina aina. Si kila limited unayoiona
inafanana na nyingine. Mara nyingi hutegemea kampuni imeundwa kwa
limited ipi.
Zipo aina mbili za limited.
Kwanza kuna limited ya Hisa, hii hujulikana kwa jina la kitaalamu
kama ( Company Limited by shares ).
Pili kuna limited ya makubaliano ambayo kwa kitaalamu huitwa (
Company limited by guarantee). Pamoja na aina hizo kutofautiana lakini
bado zote katika matumizi huwakilishwa na neno moja tu yaani ( LTD ).
Hii ni kumaanisha kuwa utofauti wake hauondoi msingi wa Limited . Katika
kuandika matangazo au mabango zote tutaandika, Mfano ……CO. LTD au ………
& CO. LTD na si vinginevyo. Tofauti hujionesha katika katiba
.
Uchambuzi kuhusu aina hizi za Limited nitaonesha kipengele
kinachofuata.
4. NENO LIMITED HUMAANISHA NINI LITUMIKAPO KATIKA KAMPUNI.
Utaratibu wa Limited upo kulinda maslahi ya baadae ya kampuni hasa
kipindi kampuni inapokuwa inakufa au inafilisika.
Kwa kawaida kampuni
inapokuwa inakufa au kufilisika hujikuta ikiwa `na madeni mengi kutoka
kwa wadai mbalimbali. Kufa kwa kampuni hakumaanishi kufa kwa deni la
wadai, hapana. Wadeni wanatakiwa kupata haki zao .Katika kuhakikisha
wadeni wanapata haki zao ndipo huu mpango wa limited ukaanzishwa.
Hapo
juu tumeona aina za limited kuwa kuna limited ya hisa (limited by
shares) na tukaona kuwa kuna limited ya makubaliano (limited by
guarantee). Sasa kwa undani kiasi tuangalie mojamoja.
( a ) Limited ya hisa ( Company limited by shares ).
Maana yake ni
ukomo uliofungamana na hisa. Katika kampuni kila mwanachama(member)
anakuwa na hisa zake.Hisa hizo huwa unaomba na unapewa.
Kila hisa
anayopewa mwanchama huwa inalipiwa na ina thamani yake. Kwahiyo
mwanachama anaweza kuwa na hisa ambazo anazimiliki akiwa tayari
amezilipia au hajazilipia au amezilipia nusu.
Katika hali hii kama
inatokea kuwa kampuni inakufa aidha kwa kufilisika au sababu nyingine
yoyote , zile hisa za wanachama ambazo walikuwa wanazimiliki lakini
hawajazilipia ndizo zitakazokamatwa na kuingizwa katika kampuni ili
zitumike kulipia madeni.
Aidha zile hisa ambazo mwanachama alikuwa
amezilipia haziwezi kutumika kulipa madeni ya kampuni na kanmwe haziwezi
kukamatwa.
Na kama kuna mwanachama ambaye alikuwa amelipia hisa zake zote kwa
ukamilifu basi hakuna hisa zake zitakazokamatwa atabaki salama na
hawezi hata kidogo kulazimishwa kutoa mali yake nyingine yoyote ili
kuchangia deni la kampuni.
Hapa ndipo tunapopata maana ya kwanza ya
neno limited ikiwa na maana ya ukomo wa uwajibijikaji.
Katika kuweka
sawa zaidi hapa tunaona kuwa ukomo au ulimited wa kuwajibishwa kwa
mwanachama umehusisha kukamatwa kwa hisa zake ambazo hajalipia.
Kwa maana
kama kampuni isingekuwa na ukomo kwa maana isingekuwa LIMITED
ingewezekana kukatwa hisa zote ambazo zimelipiwa na ambazo hazijalipiwa
na hata ikiwezekana mali zake nyingine binafsi, lakini kwa sababu kuna
ukomo ( ulimited) basi kikomo kinalazimisha kukamata zile hisa ambazo
hazijalipiwa tu na si vinginevyo.
Msisitizo ni kuwa uwajibijikaji wa mwanachama katika kulipa deni la
upo kwenye hisa na maalum kabisa hisa ambazo hazijalipiwa. Mwanachama
hawezi kuitwa kuchangia chochote isipokuwa zitatumika hisa zake ambazo
alikuwa hajalipia na kama amelipia zote hachangii kingine chochote.
Na
hii ni hata kama deni la kampuni ni kubwa kuliko hata mali zote
ilizobaki nazo aliyelipia hisa zake zote kwa ukamilifu hachangii
kingine chochote. Ndio maana huitwa uwajibikaji wenye ukomo ( Limited
Liability).
( b ) Limited ya makubaliano ( Limited by Guarantee ).
Kwa ufupi hii
humaanisha kuwa kampuni itaendesha shughuli zake kama kawaida ila
itakapotokea kuwa kampuni imekufa kwa sababu ya kufilisika au sababu
nyingine, wanachama (members ) watatoa michango yao kila mmoja ili
kuiwezesha kampuni kukidhi mahitaji yake ikiwemo madeni.
Uwajibikaji wa
wanachama katika kampuni za namna hii upo katika kuchangia. Pesa
wanayochangia huitwa “guarantee fund”.
Katika limited hii wanachama
hawachangii chochote mpaka kampuni isemwe kuwa imefilisika kabisa.
Ikiwa kampuni inaelekea kufilisika lakini haijafilisika wanachama
hawawezi kuchangia.
Limited hii huwa haipendwi sana na ni mara chache kukuta kampuni
imesajiliwa namna hii.
Kampuni za aina hii ni chache. Na hazipendwi.
Kampuni za namna hii mara nyingi hazina mtaji wa hisa ( share capital)
na hivyo wakati wa kufilisika inapotakiwa kulipa deni panakuwa hamna cha
kukamata na hivyo wanachama kutakiwa kuchangia.
5. JE YAWEZEKANA KUWAPO KAMPUNI BILA LIMITED ( LTD )
Tumeona hapo juu maana hasa limited na mazingira yake na tukasema kuwa
hiyo ni kwa mujibu wa sheria. Pia tunaona makampuni mengi ni limited na
kila anayeanzisha kampuni lazima aandike……LTD.
Swali ni je lazima
kampuni iwe limited.
Jibu ni hapana, si lazima kila kampuni iwe limited. Yawezekana ikaundwa
kampuni bila kuwa limited.
Kampuni za aina hii huitwa UNLIMITED
COMPANY. Hivyo basi kama limited company maana yake ni kampuni zenye
ukomo basi unlimited company ni kampuni isio na ukomo.
Tumeona kuwa
neno limited linatumika kueleza uwajibikaji wa wanachama pindi kampuni
inapokuwa katika msukosuko wa kufa.
Hivyo basi ukomo wa uwajibijkaji katika kampuni za namna hii hauna
mipaka(unlimited).
Hii ina maana kuwa hata mali binafsi za wanachama
zinaweza kutumika kulipa deni la kampuni. Wakati katika limited hilo
haliwezekana na hiyo ndiyo mipaka yake. Hii haina mipaka wanachama
wanalazimika kulipia kampuni deni.
Kampuni za aina hii nazo hazipendwi sana.
Nimalizie kwa kusema kuwa neno LIMITED unapoliona limeandikwa huwa
limaanisha nilichoeleza hapa juu .
Halitumiki kunogesha matamshi au
kuelezea ufahari.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA
SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE
, GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA
JUMATANO.
PIA NI KATI YA WANASHERIA WAANZILISHI WA BLOG HII
0784482959, 0714047241
bashiryakub@ymail.com
TANGAZO MUHIMU
VIWANJA NA NYUMBA ZINAUZWA.
-WANASHERIA WETU WATAKUANDALIA MIKATABA YOTE BURE NA
KUKUSIMAMIA MPAKA MANUNUZI YAKAMILIKE BURE.
-UHALALI WA NYARAKA NA UMILIKI UMETHIBITISHWA NA WANASHERIA
WETU.
-UTAPEWA MTU WA KUKUSAIDIA KUFANYA TRANSFER KWA HARAKA
BURE.
-IKIWA UTATOKEA MGOGORO NDANI YA MWAKA TANGU TAREHE YA
MANUNUZI UTAPEWA WAKILI WA KUSIMAMIA MGOGORO BURE
0783851726.
Na Bashir Yakub