JOSEPH MAHUNDI KUKABIDHIWA MILIONI 1 NA KIKOMBE KESHO MKWAKWANI


Joseph Mahundi akifanya mazoezi kama moja ya ratiba zake za kila siku

Joseph Mahundi akishangilia bao na wachezaji wenzake

 Kiungo wa timu ya Coastal Union, Joseph Mahundi alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Disemba 2014 wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoendelea kutimua vumbi kwenye viwanja mbalimbali nchini. 

 Mahundi alitoa mchango mkubwa kwa timu yake ya Coastal Union mwezi Disemba mwaka jana na kuchaguliwa na jopo la makocha linalofanya kazi ya kuchagua mchezaji bora wa kila mwezi.

 Kwa kuibuka mchezaji bora, Mahundi atakabidhiwa zawadi ya shilingi Milioni 1 na kikombe katika mechi ya Coastal Union dhidi ya Azam. 

Vodacom Tanzania imefanya mahojiano mafupi na John Mahundi na unaweza kusoma hapa chini kumjua zaidi.

Vodacom-Tupe historia yako Mahundi
Mahundi-Nina umri wa miaka 24, nilianza kucheka soka timu ya mtaani inaitwa Matalawe nikiwa na umri wa miaka 17, baadaye nikachaguliwa kucheza Copa Coca Cola mwaka 2008 na Ruvuma tukapata ubingwa. 

Tulitoka mimi na wenzangu watatu kutoka Ruvuma. Nikaitwa kikosi cha Serengeti Boys na kuna wakati tulikwenda Brazil. 

Tuliporudi mimi nikajiunga na Azam U20, nilikaa Azam FC miaka 3 kukatokea mgogoro tukawa hatuko tena Azam. 

Nikachukuliwa Friends ligi daraja la pili, katika dirisha dogo la mwaka huo  nikasajiliwa Villa. Sikucheza Villa muda mrefu nikasajiliwa Coastal Union mwaka juzi lakini baada ya muda nikasajiliwa Ashanti. 

Mwaka jana nikapata tena nafasi ya kusajiliwa Coastal Union ambapo nipo hadi leo.

Vodacom-Nani  amekuhamisha kufikia hapa ulipo?
Mahundi-Mimi naamini katika kujifunza, kusikiliza watu, kufanya mazoezi kwa bidii na kumuomba Mungu. Nilipokuwa nikicheza nilikuwa natamani na kuwaangalia wachezaji kama John Bocco na Sure Boy wanavyocheza ili niwe kama wao.

Vodacom-Unaamini katika ndumba?
Mahundi-Katika mpira siamini kama kuna ndumba mimi naamini katika kumuomba Mungu na kufanya mazoezi kwa bidii.

Vodacom-Ikitokea umepigwa ‘’tobo’’ uwanjani unajisikiaje?
Mahundi-Ah! ni jambo la kawaida katika mpira, mchezaji wa timu pinzani akinipiga tobo ni kwamba kaniwahi tu.

Vodacom-Utajisikiaje siku ukiitwa Taifa Stars?
Mahundi-Nitajisikia vizuri sana kwasababu nimewahi pia kucheza Serengeti boys, inapendeza na inafurahisha unapovaa jezi kuwakilisha Taifa lako.

Vodacom-Unadhani kwa umri ulionao na hapo ulipo umechelewa au bado upo mahali sahihi kulingana na umri wako?
Mahundi-Ninaamini bado sijachelewa, nina miaka 24 na ninaona ninaelekea pazuri.

Vodacom-Unawashauri nini vijana ambao bado wanacheza mchangani?
Mahundi-Wasikate tamaa wafanye juhudi zaidi na zaidi.

Unaweza kufuatilia makabidhiano hayo fuata ukurasa wa Vodacom wa Facebook kwa kubofya hapa www.facebook.com/tzvodacom

Mchezaji mwingine atakaekabidhiwa zawadi  Jumapili  wiki hii ni Said Bahanuzi ambaye aliibuka mchezaji bora mwezi Januari 2015.
 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post