Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Kama wewe Siyo Muoga!! KUTANA NA MTANZANIA HUYU WA AJABU,ATOBOA SIRI NYINGI KUTOKEA KWA MAAFA MENGI NCHINI TANZANIA



Mtandao huu wa Malunde1 blog umezungumza na ndugu Lt Mberito Kimvelye Magova sasa akijulikana kwa jina la 8 Dahari amezungumza mambo mengi kuhusu maafa mbalimbali yanaoendelea nchini Tanzania kama vile mvua ya ajabu ya Mwakata Kahama,ajali za hapa na pale zinazoua watanzania wengi.Ni stori ndefu isome,inatisha na itakufumbua macho kwa mambo usiyojua.Soma alichokiandika hapa chini



@@@@@@@@@@@@@@@@
=DHANA YA KUFIKIRIKA CHANYA NA HASI=
HISTORIA FUPI YA MAISHA YANGU:
“LT MBERITO KIMVELYE MAGOVA” (MST)
NIMEIANDIKA NIKIWA DODOMA: TAREHE 16/06/2011
Mimi nimeamua kueleza historia fupi ya maisha yangu juu ya mambo mbalimbali ninayopambana nayo katika maisha yangu tangu mwaka 1956 mpaka sas. 

Wako watu Tanzania, Africa na Ulimwengu kwa ujumla hawataamini lakini ukweli uko kwenye matendo yanayotokea kwa sasa, hata mimi nilikuwa nayapuuza kwa “Ndoto na Maono” tangu mwaka 1956 kwa sasa nimeamua kuwapa historia ya maisha yangu na masuala ninayo  yafanya kwa sasa. 

 Baba mzazi wangu ni Kimvelye Mpandachombo Magova alifariki mwaka 1990 na Mama yangu ni Gislamali Zumba Selubava alifariki mwaka 2000, mimi nilizaliwa “Kitongoji cha Ngela, Kijiji cha Lyasa, Kata ya Image, Tarafa ya Mazombe, Wilaya ya Kilolo Mkoa wa Iringa”.Nilizaliwa tarehe 27/07/1952, baada ya kuzaliwa nilipewa jina la utoto “Mandili”. 

  Tarehe 24/06/1953 nilibatizwa kwenye dhehebu la RC katika Parokia ya Mwaya Ilula, Kilolo Iringa na kupewa jina la Albert (Alberto).  Mambo yaliyonipata tangu Mwaka 1956 hadi mwaka 2011 ambayo nayakumbuka kipindi nikiwa mdogo hadi sasa. 


 Ninavyoandika juu maisha yangu ya ndoto na maono, yalitokea na yanaendelea kutokea.


Mwaka 1956 tukiwa tunaishi Kitongoji cha Ngela saa 12:00 jioni mama alitenga chungu chenye maji kwa ajili ya kusonga ugali, mimi nilikaa nyuma ya wenzangu watatu, Chungu kilitenguka na maji moto yalimwagika na yaliniunguza mimi mguu wa kulia, mpaka leo nina alama ya kuchomwa. Lakini wenzangu wote watatu maji hayo hayakuwaunguza. 


 Mwaka 1956 nakumbuka ilikuwa saa 1:30 usiku nilisikia “Njiwa wa kufugwa” wanarukaruka na kupiga kelele kwa mama mdogo “Habiba Temapakwe Figowole”  nilipokwenda kuangalia nilikumta anajitundika kwa kamba, akiwa amesimama kwenye kinu cha kutwangia mahindi, mimi nilikwenda mbio kumwambia baba yangu, baba alikwenda mbio na kukata kamba kwa kisu akanusurika kufa.  Baba kesho yake alimrudisha kwao. 

  Mwezi wa tatu, Mwaka 1957 Marehemu kaka yangu Daniel K. Magova alikuwa anasoma Elimu ya awali, baada ya kurudi toka masomoni, mama alimwambia achukue jembe kwenda kupalilia Mahindi, wakati wa kupalilia alinikata na jembe kichwani upande wa kushoto mpaka sasa alama ipo. 

 Mwaka 1958 tulihama toka Kitongoji cha Ngela na kuhamia Kitongoji cha Sasagila, Kijiji cha Lyasa, Kata ya Image, Tarafa ya Mazombe Iringa Vijijini, kwa sasa Wilaya ya Kilolo.  Mwaka 1959 niliota ndoto walikuja watu watatu waliniambia kuwa “sisi ni Malaika wa Mungu” kati ya Malaika saba wala usiogope tutakuja tena, nilipoamka sikuona kitu ila niliogopa sana. 

 Mwaka 1960 niliota ndoto nilibebwa, na watu watatu nakunipeleka kwenye mawingu juu ya Anga, mimi niliogopa sana, waliniambia sisi ni Malaika watatu tumetumwa tukuonyeshe huku Angani, nilipoamka sikuona kitu, kwa kweli niliogopa sana. 


 Mwaka 1962 nilianza kusoma Darasa la kwanza Shule ya Msingi ya Lyasa, Kata ya Image, Tarafa ya Mazombe, Wilaya ya Kilolo Iringa Mwaka “1963 na 1964” sikusoma kwa sababu niliumwa na Nyoka na kulazwa Hospitali Iringa Mjini miezi minane, nakumbuka Daktari alikuwa Mjerumani aliyekuwa ananitibu. 

Daktari aliwambia Manesi kuwa kesho huyu mgonjwa hakuna kula kitu chochote atakwenda “Fyeta”. Usiku walikuja Malaika watatu wakaniambia hakuna kwenda “Fyeta”, watakukata Mguu.  Asubuhi Baba na Mama walikuja kuniona na kunionea huruma kwa sababu nilikonda sana.

 Manesi walikuja kunichukua kwenda”Fyeta” mimi nilikataa na kusema heri nife na miguu yangu yote kuliko kukatwa mguu wangu, nilishikilia kitanda kwa mikono yangu yote miwili.  Nesi alikwenda kumwambia Daktari, alipokuja aliniangalia na kutikisa kichwa aliwaambia Manesi mwacheni, Daktari aliondoka akiwa anatikisa kichwa. 

Mama alilia machozi nakusema mwanangu unateseka sana, tena umeknda sana.  Kesho yake Manesi walikuja na kusimama na kusema huyu kafa, mbona leo halalamiki. 

Walipofunua shuka waliona”usaa” mwingi mweusi kama mkaa. Walimwita Daktari, alimwambia mchukueni mkamukamue usaa. Uvimbe ulipasuka vidonda vitatu waliniminya “Usaa” na kuingiza gozi ya kitambaa chenye urefu wa mita moja kikiwa na dawa, kwa kuigiza kwenye kidonda na kutoa kila siku kwa muda wa wiki tano. 

Mwili wangu ngozi ilichubuka mwili wote kama vyoka.  Nilipewa ruhusa kwenda nyumbani nilitumia mkongojo alionipa na mtu aliyekatwa mguu, nilimwacha hospitali.  Baba alisema wewe kusoma shule basi usisome, mimi baba yangu sikujibu kitu. 

 Usiku walikuja malaika watatu walisema wewe shule soma, huu mguuu utapona, kwa kweli ndoto zangu zilinisumbua sana, kwa sababu niliwaona watu watatu wako mbele yangu, mimi nikiwa nimekaa nyuma yao wote walitazama mbele, niliwauliza ninyi ni malaika gani, walisema tekeleza tunachokwambia, sisi hutumwa kwako na Roho wa Mungu, nilipoamka nilitetemeka sana kwani sikuwaona watu. 

 Mwaka 1965 nilianza tena darasa la kwanza, baadae mguu ulinyoka na kutembea vizuri mpaka sasa ila kuna alama za makovu matatu kwenye mguu wa kulia. 

  Mwaka 1967 nakumbuka Baba aliniambia niende kuchunga Ng’ombe siku ya Jumamosi, nilikwenda mita 100, mimi nilikapotea nikawa kwenye msitu mnene sana  niliwaona Tembo, Fisi, Simba na Nyani.

 Mvua ilinyesha sana tangu saa 3:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni mimi nilipanda Mlima wa “Msasamu” ili niangalie nyumbani ni wapi, hadi nyumbani ni kilomita saba. 


 Nilikunywa maji yaliyotwama kwenye jiwe kama “Mtungi” ndipo nilipozinduka na kujua uelekeo wa nyumbani.  Nilifika nyumbani saa tano usiku, niliwakuta watu wamekusanyika wakidhani nimekufa kwa sababu Ng’ombe wote walirudi nyumbani. 


 Nilipolala usiku walikuja Malaika watatu na kuniambia kuwa “Mungu” anakuandaa kwa kazi maalumu usiogope kwa matukio yanayotokea mara kwa mara.  Asubuhi niliwambia wazazi wangu kuwa, kuna watu huwa wananijia usiku, lakini nikiamka huwa siwaoni ila wao hujiita “ Malaika” wazazi wangu waliniambia kuwa hiyo ni “Misoka au mitu”, mimi sikuwaelewa walikuwa na maana ganikwa maneno hayo. 


  Mwaka 1968 Malaika watatu waliniambia mwezi wa nane kwenye kichuguu chini ya mti aina ya (Mkalala), ndani ya kichuguu kuna “maji” nilipoamka, mama alikuwa anakoboa mahindi kwenye kinu, nilimwambia “mama”, nimeota ndoto kwenye kichuguu chini ya mti kuna maji, mama alichukua kajembe kadogo, alisema twende ukanionyeshe hayo maji.


  Mama nilimwonyesha kichuguu cha mchwa, alichimba na jembe moja tu, maji yalitililika meusi sana, mama aliniambia kuwa, haya maji uliyaweka mwenyewe, mwezi wa nane maji yatatoka wapi, wakati hakuna mvua, mimi nilimwambia niliota kwa kuambiwa na watu watatu ambao walijiita Malaika. Baba alisema kuwa, huyu mtoto hufanya maajabu mengi sio kama wenzake. 


 Mwaka 1969 Malaika watatu waliniambia kuwa, mwambie Baba yako asiende shambani kuna Tembo, asubuhi Baba nilimwambia juu ya ndoto zangu, Baba alicheka na kumwambia mama, mama alisema huyu humfahamu, akisema kitu hutokea, kwa hiyo usiende.  Baba alisema ni ndoto tu si kweli, Baba alikwenda shambani “Mkolomi” alikuta Tembo wanakula mazao (Mahindi na Ulezi), wako kwenye miti mikubwa kwa ajili ya kivuli. 


 Baba baada ya kurudi nyumbani alimwambia mama nimewakuta Tembo wengi shambani. Mama alisema huyu mtoto namwogopa sijui yukoje, akiota kitu ni kweli hutokea.  Mwaka 1970 niliota ndoto mama mkubwa kafiwa na kijana wake Gwerino Temapakwe Figawele. 


Baba na Mama walikwenda kulima, wakati wa kwenda shuleni nilikwenda shambani na kuwaambia kuwa, nimeota ndoto mtoto wa mama mkubwa kafa, mama aliniuliza nani kakwambia, nilimjibu nimeota ndoto, kabla sijaondoka kaka alikuja kutoa habari za msiba, mama alimwuliza huyu mdogo wako ulimwambia, kaka alimjibu  hapana.  Baba na mama waliacha kulima, mimi nilikwenda shuleni kuomba ruksa ili kwenda kwenye msiba. 

  Mim nilimaliza masomo ya msingi tarehe 27/09/1971 Shule ya Lyasa, Januari, 1971 alipopinduliwa Milton Obote Rais wa Uganda nilisikitika sana baada ya kusikia kuwa, Rais Milton Obote kapinduliwa na Iddi Amin Adada, wakati Rais Milton Obote alipokwenda Singapore kwenye mkutano wa kimataifa.


 Usiku niliota ndoto kuwa, nenda kajiandikishe kwenda JWTZ baada ya kumaliza Shule ya Msingi Lyasa, 05/10/1971 nilikwenda Iringa Mjini Tawi la Myomboni nilijiandikisha na kuchaguliwa kwenda “TMA (Tanzania Military Academey), Mgulani Dar es Salaam na kuanza mafunzo ya awali ya JWTZ. 

  Tarehe 10/11/1971 niliajiriwa na JWTZ Makao Makuu Upanga Dar es Salaam, Mkuu wa majeshi alikuwa General MSH Sarakikya na COS Col. John Bukuku nilimaliza mafunzo ya awali mwezi Mei, 1972, na kupelekwa kwenye Kikosi cha 13KJ cha kwanza cha Mizinga Tabora Tanzania.


 Mwaka 1973, nakumbuka nilikuwa natoka Mjini Tabora kwenda Milambo Baracks” tulikutana na mzee mmoja kwenye makutano ya Reli ya kutoka Kigoma na barabara ya “Mwanza Road” kwenda kambi ya Milambo karibu na mwembe kulia nilimwona mzee nilimsalimia na kuitikia, alikwenda kama mita 10, alisimama na kuniita we kijana simama, mimi nilisimama.


 Baada ya kusimama alikuja na aliniambia kuwa, “Wewe kijana unabahati sana, utafanya mambo mengi ya Tanzania na Mataifa”, nilimjibu kwa woga kuwa nimekusikia, alisema nenda. 

 Mimi nilijiuliza sana yule Mzee simjui na kwa nini alisema vile, niliendelea na safari yangu ya kwenda kambini Milambo. 

Mwaka 1972/1973 tulifundishwa na Wachina masomo ya mizinga Tabora, na kumalizia masomo kwa vitendo “Monduli Arusha na kurudi tena Tabora nilipanda cheo toka Private kuwa L/CPL. Nilifanya kozi ya Daraja la tatu la Mizinga. Mwaka 1973 tulishiriki kwenye ulinzi Manyovu Kigoma mpakani kati ya Burundi na Tanzania.

  Burundi walipigana vita vya “Ukabila” (Wahutu na Watusi) mwaka 1972 wakati wa utawala wa “Raisi Meja Michombero” wakimbizi 150,000 toka Burundi, walipoingia Kigoma walifanya uhalifu na kuuwa wenyeji wa Kigoma. 


 Mwaka 1974 nilikwenda na wenzangu kwenye ulinzi wa mpaka wa Mtukula kati ya Tanzania na Uganda kwa sababu ya vurugu za Idd Amin Dada wa Uganda. Pia nilipanda Cheo toka L/CPL kuwa CPL pamoja na kufanya Kozi ya Daraja la pili la Mizinga. Mwezi wa tisa 1974 hadi Juni 1975, mimi niliteuliwa kuwa mkufunzi wa Mizinga. 

Msumbiji ilipata uhuru 1975 mimi na wenzangu tulijishughulisha na masuala ya ukombozi kwa Msumbiji dhidi ya utawala haramu wa Makaburu (Wareno). 

Mwaka 1975 nilifanya kozi ya uongozi mdogo wa mizinga Tabora na kumalizia kozi Kititimo Mkoa wa Singida. Siku moja usiku niliota ndoto, Malaika watatu waliniambia kuwa, utasafiri kwa Ndege utakutana na watu wengi wakisema na kuimba nyimbo kwa lugha usioifahamu. 


 Mwezi June 1976 nilipanda cheo toka CPL na kuwa SGT pia niliteuliwa na Makao Makuu ya Jeshi kwenda kufundisha wapigania Uhuru wa (ZIPA) Zimbabwe walikuwa watu 5,000. Tulisafiri kwa Ndege ya JWTZ toka Tabora hadi Nachingwea Mkoa wa Lindi, ndege iliendeshwa na Rubani Captain Yakanda mimi nilikumbuka ndoto ya mwaka 1975 kuwa ni ya kweli. 


 Mimi na wenzangu tukiwa “Farm 17 Nachingwa” tuligawana wapigania Uhuru wa Zimbabwe waliongozwa na viongozi wakuu wao Ndugu Joshua Nkomo, Robert Mugale na Alex Nongo pamoja na makamanda wengine wapigania uhuru. 


Mimi na Makamanda wengine tulikwenda na baadhi ya wapigania Uhuru kufanyia mafunzo “Farm 2 Ntila” Nachingwa karibu na Bwawa la Maji. Nawakumbuka baadhi ya makamanda ambao tulikuwa nao “Farm 17 na farm 2 Nachingwea ni CoI Sama Mkuu wa Chuo , Lt. col Albai, Capt. Kiswaga, Capt, Palanjo, Capt Magori, Capt Mwakisunga, Capt Shimanyi Capt Lusilie, Lt Lumbila, Lt. Lihapa, Sgt Mtungi, Lt Njikanyika, Sgt Makungu na Makamanda wengine zaidi ya 100.


 Tulifanya kazi mchana na usiku kwa kujitolea. Mwaka 1977 niliota ndoto nikiwa na watu watatu ambao walijiita Malaika, waliniambia waambie wakuu wako hawa, wapigania Uhuru wamepanga kuwaua wote wakufunzi. 

Asubuhi sikusita ilibidi niwaambie Makamanda wangu kuwa, hawa wapigania Uhuru wana mpango wa kutuuwa wote. Makamanda walifanya uchunguzi na kubaini kuwa ni kweli, kuna baadhi ya viongozi wao ni “Mamluki” wa Simith wa Zimbabwe. 


  Ndipo walipotolewa wote kwa kuambiwa wanakwenda kozi “Cuba, Urusi na China” walifurahi sana walipofika Dar es Salaam wote walikuwa chini ya ulinzi Dar es Salaam.  “Farm 17 na Farm 2 Nachingwea” waliteuliwa makamanda wengine miongoni mwao.Hata hivyo walikiri kuwa. Makamanda wao walipanga kuwauwa wote na kuchukua silaha zote, na kurudi Zimbabwe.


 Baada ya Makamanda wapya kuteuliwa, mafunzo yaliendelea vizuri sana na wapigania Uhuru walikuwa na morali sana kuliko awali.  Mimi Mberito K. Magova nilitafuta mpigania Uhuru mmoja Ndugu “Pandeli Nehondo” kunifundisha Kishona ili kupata habari wakati wa kipindi cha “Moral time” usiku.  


 Kitendo cha kukesha nao usiku hadi saa saba usiku, waliniita “Comrade Harassman” kwa sababu ya kuwafundisha masomo ya ukakamavu na kwata. Mwezi Machi, 1978 niliteuliwa kwenda kozi ya uongozi mkubwa TAM (Tanzania Military Academy) Mgulani (Chuo cha Abdallah Twalipo) Dar es Salaam. Kozi kwa vitendo nilimalizia Mkumbo Morogoro mwezi wa 8/1978. Baada ya kozi niliomba likizo mwezi mmoja wa kumi (10) kwenda Iringa. Tarehe 01/10/1978 nilioa “Bi Emmanuela William Magohagasenga” wa Kihodombi Iringa.


 Ndoa nilifungia Kanisa la Consolata Mshindo Iringa. Katika ndoa yetu tuna watoto wane. (William M. Magova, Andason M. Magovaa, Happy M. Magova na Moses M. Magova) Tarehe 11/10/1978 Nduli Idd Amin alivamia Tanzania eneo la Kyaka na Kitengule kwa kupiga Mabomu kwa Ndege za Kivita. Tarehe 21/10/1978 alivamia eneo la Kagera na kuliteka kuwa, ni eneo la Uganda.


 Mimi niliondoka toka Lyasa, Image hadi Iringa na kwenda vitani tarehe 25/10/1978 hadi Tabora. Niliondoka Tabora tarehe 27/10/1978 kwenda vitani kwa kupitia Shinyanga kwa Ndege ya JWTZ. 


 Toka Shinyanga kwa Gari aina ya Landrover la JWTZ hadi Biharamulo Kagera, nilimkuta Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine alinikabidhi Landrover mpya 30 toka Cooper Motors Dar es Salaam, toka Biharamulo hadi Katoro Bukoba na kupokelewa na Makamanda wangu Capt. Joseph Mongi na Lt. Pindingu (alikufa vitani). Mimi nilikuwa Brigedi ya 208 KV.

 Iliyopita mtukula iliongozwa na Hayati Brig Mwita Marwa toka Mtukula hadi Kitgum Uganda mpakani na Sudan.  Vita tulipigana toka Katoro, Kyaka, Bunanzi, Igayanza (Igayanza sehemu ya maandalizi ya vita).  Brigedi ya 207KV iliongozwa na Brigedia John Walden upande wa Ziwa Victoria.  Brigedi ya 206KV iliongozwa na Brigedia Silasi Mayunga kupitia Kakunyu kuelekea Mbarara Uganda.  Mapambano yalianza rasmi sa 10:00 alfajiri tarehe 22/01/1979 kwa kukomboa ‘Mtukula”. Brigedi ya 208 KV iliyoongozwa na Brigedia Mwita Marwa. 


Mapambano ndani ya Uganda, vita vilianzia Kakuto, Sanje, Kiotela Kalisiso Masaka, Lukaya, Mityana maria Mpigi, Nakauka, Entebbe, Kampala, Jinja, Iganga, Tororo, Mbale, Kapchorwa, Busia, Moroto, Kaabong, Soroti, Lira, Gulu, Nimule hadi Kitgum Mpakani mwa Uganda na Sudan na kurudi tena Soroti. 


 Vita viliisha 06/06/1979 na kurudi Tanzania Tarehe 25/07/1979 tulipokelewa Bunanzi Kyaka Bukoba na “Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere” (Baba wa Taifa) Godfrey Binaisa alikuwa Rais wa Uganda baada ya Prof. Yusuph Lule, alitawala hadi Mwezi June 1979. Mimi nilipandishwa cheo toka Sgt. na kuwa 2Lt (2Lieutenant).  Mwezi Januri, 1981 tulihamishwa na wenzangu kwenda kuanzisha kikosi cha Mizinga (Artillery) Kiabakari Musomo Mara. 


Mwezi Julai 1982 nilipanda cheo toka 2Lt kuwa Luteni.  Mwaka 1983 nilikwenda kozi ya mizinga Chuo cha Mizinga (SOFA “School of Artillery”) Monduli Arusha kwa Masomo ya Uongozi wa mizinga Tanzania.  Mwaka 1984 nilijiunga na Sekondari ya Kiabari JWTZ. Mwaka 1985 nilipelekwa na Makao Makuu ya Jeshi kwenye mafunzo ya Ukada Chuo cha CCM Murutunguru Ukerewe Mwanza kusomea “Itikadi, Uchumi, Siasa, Uongozi, utawala na menejimenti (Urasimu)”.


MASOMO YA KUJIENDELEZA KWA KUJISOMESHA MWENYEWE.
1.   Mwaka 1972 nilisoma kwa njia ya Posta toka ICS (International  Correspondence School) toka Kenya Masoma ya Kiingereza, Hesabu, History, Siasa na Jiografia.
2.   Mwaka 1983 hadi tarehe 03/07/1985 nilisoma kwa njia ya Posta toka Taasisi ya watu Wazima (Institute of Adult Education) somo la Siasa hadi hatua ya tatu ni sawa na Kidato cha sita (“A”Level).


MASOMO YA TAALUMA YA KIJESHI (ARTILLERY) UHAMISHO.
1.   Mwaka 1986 nilisomea masomo ya RSO (Regimental Surveyor Officer) na FOO (Fighters Observation Officer) Chuo cha CTU Monduli Arusha kwa ajili ya mipango ya Kivita (Military Carrier Plan).


2.   Juni Mwaka 1986 nilihamishwa toka Kiabakari Musoma kwenda Kikosi cha 179KJ Kunduchi Dar es Salaam kuwa PEO (Political Education Officer) wa Kikosi .


3.   Julai, 1987 niliteuliwa na Makao Makuu ya Jeshi (MMJ) kwenda kusoma elimu ya juu ya “Ukamanda na Uuongozi” “Command and Staff” (Higher Military Matters Education) na elimu ya juu “Sayansi ya Jamii” (Social Science).  Chuo cha “V.I Lenin Academy Mascow Urusi” kwamuda wa miaka minne (4). Nilihitimu masomo 29, “masomo ya Sayansi ya jamii 15 na masomo ya kijeshi 14”


MASOMO YA ELIMU YA JUU YA KIJESHI.
Masomo ya “Sayansi ya Jamii” nilisomea mwenendo wa siasa ndani ya jamii” (Political Actual Movements in the Societies) na masomo ya Kijeshi nilisomea  “Elimu ya juu ya Kijeshi kwa ujumla” Command and staff (Higher Military Education and Carrier Plan).


Mwaka 1992 baada ya kurudi masomoni toka Moscow Urusi, Makao Makuu ya JWTZ walinipeleka Makao Makuu ya Ulinzi wa Anga Mbwezi Dar es Salaam, kwa sababu nilisomea masomo ya “Mizinga, Mabomu, Rada na Maroketi ya kutungua ndege” pamoja na masomo mengine ya kijeshi.  Nikiwa ADC HQ nilitembelea vikosi vya “Masaki, Mbagala, Gongolamboto, Mgulani na Lugalo” kwa Dar es Salaam


  Nilitoa ushauri juu ya utunzaji wa zana na vifaa vya kijeshi kuwa sio mzuri kwa kulingana nilivyosomea. Uongozi wa juu haukukubaliana na ushauri wangu Makamanda wengine, walisema unajifanya umesoma mimi nilichukia sana. 


Mimi niliamua kuacha  Jeshi mwaka 1992 kwa usalama wangu, nilipokubaliwa kuacha kazi ya JWTZ Julay 1992.  Niliandika malalamiko kwa kupunjwa malipo tuliyojilipia wakati wa masomo kwa vitendo toka Moscow kwenda Dar es Salaam na kurudi.  Pia malalamiko kwa kutotendewa haki kwa kulingana na sheria za Kijeshi ukisoma “Command and Staff” elimu ya juu ya Jeshi utapandishwa cheo. 


 Mchakato wa kesi ulipitia Makao Makuu ya Jeshi (MMJ), Wizara ya Ulinzi, Ikulu na Tume ya haki za Binadamu na Utawala bora.  Kesi ilianza mwaka 1992 hadi kwisha tarehe 05/01/2006 nilishinda. 


Makao Makuu walikubali kunilipa TShs. 388,000/= mimi niliwambia MMJ wanilipe kwa kiwango (Rates) cha sasa na gharama za usumbufu mpaka siku ya kulipwa haki yangu. Pia kwa nini hawakunipandisha  cheo kwa kusomea “Brigedia hadi Army” kwa kozi ya Suprerio Commoner” (Kamando Mkuu).

KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA KILOLO IRINGA MWAKA 1995.
Mwaka 1995 niligombea Ubunge Jimbo la Kilolo Iringa tulikuwa wagombea 15, Mbunge wa zamani Mhe: Stephen Mwaduma aliongoza na aliteuliwa kugombea.  Mimi Kamati ya siasa ya Wilaya Iringa vijijini iliniteua kuwa “Kampeni Meneja” wa Mhe: Stephen Mwaduma alishinda dhidi ya vyama vingine vya siasa na kuwa Mbunge wa Jimbo la Kilolo.


NDOTO TATANISHI KWA KUKUMBUSHWA NDOTO YA MWAKA 1968 YA MAJI KWENYE KICHUGU CHA MUCHWA.


Mwaka 1995 nilitoa ndoto walikuja Malaika watatu nikiwa nyumbani Lyasa Image Iringa kuwa, nikachimbe karibu na mti aina ya “Mtowo” pana jiwe la mviringo (Nununilo) kuna maji, hayo maji nijaze kwenye chupa ya Lita moja na nusu na kufunika, nisiyaache kama maji niliyoota mwaka 1968 maji hayo yakiisha kutakuwa hakuna “Amani na Utulivu Duniani”. Maji yale niliyatunza na yalikwisha kwenye chupa bila kumwagika mwezi wa tisa (9) mwaka 2010. 


 Lakini niliambiwa endelea kutoa ushauri juu ya Amani na Utilivu Ulimwenguni wakikataa acha. Ila iko siku tutakuja Malaika saba tutakwambia la kufanya Ulimwenguni. Nilitunza siri hakuna niliyemwambia sasa nasema kwa sababu wamenijia katika ndoto tarehe 22/05/2011 na kuniambia nifunge tangu tarehe 23/05/2011 hadi tarehe 24/06/2011 tutakuja tena kukwambia la kufanya Ulimwenguni.


 Wako viongozi wameanza kuhangaika juu yako.  “Nasubiri maagizo ya Malaika saba (7)” kwa kweli naogopa kwa sababu yote niliyoota yametokea, lakini nilitoa ushauri kwa maandishi.  


 Kwa sasa nimeamua kuwaambia Watanzania na Ulimwengu kwa ujumla juu ya “Amani, Utulivu, Ulinzi na Usalama”. Watawala, Viongozi na Watendaji wa Serikali, Vyama vya Siasa Matajiri na Madhehebu ya Dini wajali maisha ya wanyonge sio kuuwana na kuwabaka wanawake, Mwenyezi Mungu anachukia. Watu watapigana kwa itikadi za “Siasa, Dini, Ukabila, Ubabe, Udikteta na Ubaguzi wa rangi” watawala watauwawa na kupinduliwa, amani itakuwa hakuna kabisa.


MWAKA 1996 HADI MWAKA 1998 NILIFUNDISHA KIBAHA SEKONDARI.


Mwaka 1996 hadi Mwaka 1998 nilifundisha Shule ya Sekondari Kibaha, Shirika la Elimu Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani.  Masomo ya Uraia, Geografia na Historia (Civics or Socialogy, Geography and History).  Niliacha kufundisha baada ya kubaini mitaala kuwa na makosa hasa Uraia na Historia (Civics and History).
NDOTO JUU YA KIFO CHA MWALIMU JK. NYERERE.


Tarehe 13/10/1999 Niliota Mwalimu JK. Nyerere alikuja akisindikizwa na Malaika watatu niliambiwa ni sisi Malaika watatu, tumeletwa na Roho Mtakatifu, kwa kumleta Nyerere kwako.  Nyerere alikuwa na shuka nyeupe yenye ufito wa bluu na mto una madoa ya bluu na meupe. 

 Aliniambia kuwa, mimi nakufa endelea kushauri juu ya “Amani, Utulivu, Ulinzi na Usalama”. Mimi nilitaka kumpa mkono Mwalimu JK.Nyerere. Malaika walisema acha hiyo ni ”Dahari”.  Baada ya kuamka mimi nilitetemeka sana na sikuamini kama ni kweli.  Tarehe 14/10/1999 saa 7:00 mchana nilisikia kwenye Redio na TV kuwa Mwalimu J.K. Nyerere amefariki Uingereza, katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas.


UKAMUA KUMUENZI HAYATI  JK. NYERERE (BABA WA TAIFA)
Kwa kutokana na ndoto ya Tarehe 13/10/1999 ambayo Hayati Mwalimu J. K. Nyerere (Baba wa Taifa) aliletwa kwangu na Malaika watatu aliniagiza kuwa, niendelee kutoa ushauri juu ya “Amani Utulivu Ulinzi na Usalama” niliamua kuanza kumuenzi kwa kutembea kwa miguu toka Mailimoja Kibaha Pwani hadi Mtuwa Ilula Iringa.


Mchakato wa kutembea kwa miguu ulianza baada ya kupewa kibali na mkuu wa Wilaya Mhe; Hawa Ngulume Tarehe 06/05/2000 saa 04:00 Asubuhi mimi Mberito Kimvelye Magova (Mbekima) niliamua kumuenzi Mwalimu J. K. Nyerere “Baba wa Taifa” Ambaye kwa sasa ni Hayati, baada ya kuandikiwa barua ya tarehe 05/05/2000 Kumbu. Na.KBH/1.20/14/61, ambayo nilipewa na Mhe: Hawa Ngulule Mkuu wa Wilaya ya Kibaha baada ya kunihoji sana na “Kamati ya Ulinzi na Usalama”.  Niliwahakikishia kuwa mimi nina akili timamu juu ya kumuenzi Hayati Mwalimu J. K. Nyerere (Baba wa Taifa).


 Niliwaambia kuwa katika utawala wake kwa masuala mbalimbali aliyofanya katika utawala wake. Alikemea “Rushwa, Udini, Ukabila, Dhuluma, Uongo, wizi na Viongozi wazembe” wasiofuata “Maadili na Maudhui” ya kutofuata katiba na sheria za nchi.


Nilianza safari ya kumuenzi Hayati Mwalimu J. K. Nyerere nikiwa pekee yangu. Nilisindikizwa kidogo na Mkuu wa Wilaya Kibaha Mhe: Hawa Ngulume, Katibu wa Wilaya Kibaha Ndugu Hayati Sofia Uluvi, M/Kiti wa CCM Kata ya Mailimoja Ndugu Mzee Mrisho na Wana CCM Kumi (10) kwa kilometa moja tu.


Katika kumuenzi Hayati Mwalimu J. K. Nyerere (Baba wa Taifa) nilitoka Kibaha Pwani hadi Iringa kwa kutembea kilomita 378 kwa siku 14 na kupumzika siku tatu (3), jumla ni siku kumi na saba.
Vituo nilivyopita ni kama vifuatavyo:-


·        Tarehe 06/05/2000 nilitoka Mailimoja Kibaha saa 04:00 Asubuhi nilifika “Vigwaza” saa 12:00 jioni na kulala nyumba ya kulala Wageni ya “Mponda “ kwa kulipa Tshs. 1,500/=.
·        Tarehe 07/05/2000 niliondoka Vigwaza saa 12:00 Asubuhi nilifika Chalinze saa 1:00 usiku na kulala nyumba ya wageni ya “Furaha” kwa kulipa Tshs. 1,200/=.


·        Tarehe 08/05/2000 niliondoka Chalinze saa 03:30 asubuhi nilifika Bwawani Magereza saa 11:30 jioni na kulala nyumba ya wageni kwa kulipiwa na Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Bwawani.
·        Tarehe 09/05/2000 niliondoka Bwawani saa 02:30 asubuhi, nilifika Morogoro Mjini saa 11:00 jioni, nililala nyumba ya wageni ya ndugu “Ramadhani Hamis” nililipa Tshs. 2,000/=.


·        Tarehe 10/05/2000 nilikwenda saa 02:00 asubuhi kwenye Ofisi za RTD (TBC) na kuongea na watangazaji, Ndugu Sarah Dumba na Monica Lyampawe nilitoa Barua ya utambulisho toka kwa Mkuu wa Wilaya Kibaha Mhe: Hawa Ngulume.


·        Morogoro pia nilikwenda TV ya Abood na kuhojiwa na Ndugu John Ndumbaro, Hamis Mkumba, Bujaga Izengo Kadago, Devota Minja na Salumu Mkambala.


·        Morogoro nilipumzika siku tatu tangu Tarehe 10/05/2000 hadi Tarehe 13/05/2000 kwa ajili ya kujitibu, michubuko kwenye miguu kwa kutumia Dawa za asili nilizokuwa  nazo kwa kujitibu, Dawa za asili kwa magonjwa mbalimbali nilianza kuzitumia na kufanya atafiti tangu 1992 hadi sasa 2011 natumia dawa asili kwa magonjwa mbalimbali.


·        Tarehe 13/05/2000 niliondoka saa 02:00 asubuhi na kulala Melela kwa Katibu wa CCM Tawi Melela nilifika saa 11:00 jioni.


·        Tarehe 14/05/2000 niliondoka Malela saa 02:00 asubuhi na kufika Doma saa 10:00 jioni. Maafisa wa Mbuga za wanyama waliniambia Mbuga ya Mikumi kuna Wanyama hawaruhusu watu kutembea kwa miguu. Walinisafirisha kwa Gari hadi Mikumi na kulala nyumba ya wageni, jina Gesti halikuandikwa.


·        Tarehe 15/05/2000 nilitoka Mikumi saa 02:00 asubuhi na kufika saa 12:00 jioni Daraja mbili “Iyovu”.  Na kulala nyumba ya “Mabati” (full suit) ya Idara ya maji, Iyovu.


·        Tarehe 16/05/2000 nilitoka Iyovu saa 01:00 Asubuhi na kufika Mtandika (Ruaha Mbuyuni) saa 01:00 usiku na kulala kwa Chilwa Selubava, nyumba ya kulala Wageni.


·        Tarehe 17/05/2000 nilitoka Mtandika saa 02:00 asubuhi na kufika Mahenge saa 12:00 jioni na kulala kwa Ndugu Mbugi.


·        Tarehe 18/05/2000 toka Mahenge hadi Ilula Mtuwa nililala kwenye Nyumba ya kulala Wageni ya Ndugu Johannes Muhanga.


·        Tarehe 20/05/2000 nilikwenda kuripoti kwa Viongozi wa “Serikali, Kamati ya Ulinzi na Usalama”, Iringa Vijijini (kwa sasa Wilaya ya Kilolo). Nilionana na Mkuu wa Wilaya Ndugu Goloi, Mkuu wa Usalama wa Taifa na Mkuu wa Polisi Wilaya. Niliwaambia kuwa mimi ni mzima. Niliwaambia lakini lazima Nyerere tumuenzi hasa kwa masuala ya “Upendo, Umoja, Mshikumano, uelewano, Amani, Utulivu, Ulinzi na Usalama” kwa gharama zozote zile.
·        Tarehe 21/05/2000 niliondoka kwenda nyumbani Image Kijiji cha Lyasa kwa mapumziko mafupi.


·        Tarehe 27/05/2000 niliongea na baadhi ya viongozi Ilula Mtuwa juu ya umuhimu wa kudumisha masuala ya “Amani, Utulivu, Ulinzi na Usalama katika Taifa letu.


 Hata hivyo kuwe na dhana endelevu ya kumenzi Hayati Mwalimu J. K. Nyerere (Baba wa Taifa). Kwani alitafuta Uhuru bila kumwaga damu. Hata hivyo katika Utawala wake kuna baadhi ya viongozi na Watendaji wa Chama na Serikali walifanya mazoezi ya kutaka kumpindua. Mazoezi hayo yalishindwa mara tatu.  Mimi binafsi nitaendelea kumuenzi kwa yote aliyoyafanya Hayati JK. Nyerere (Baba wa Taifa) kwa Tanzania. Afrika na Ulimwengu kwa ujumla. 


Watu wote waliofanya Uhaini dhidi ya Utawala wake hakuwauwa aliwaweka kizuizini na wengine walikimbilia Uingereza na  walifia huko kwa uzee. Wakati Mwalimu J. K. Nyerere alipokuwa anang’atuka mwaka 1985 aliwatoa kizuizini.  Sitaki kuwataja majina kwa sababu kutakuwa na “dhana fikirika’ kati ya “Ukoo wa hayati Mwalimu J. K. Nyerere na Koo za waliwekwa kizuizini.


·        Tarehe 26/27/01/2001 katika maisha yangu sitasahau baadhi ya vyama vya Siasa vilivyochochea Wananchi Zanzibar. Wananchi kupambana na vyombo vya Dola na kusababisha zaidi ya watu 47 kufa na wengine kukimbia toka Zanzibar kwa sababu ya itikadi ya vyama vya  Siasa.


 Kitendo hicho mimi kiliniuma sana. Katika uzoefu wangu wa Siasa bado nasema hakuna “Ubia wa Siasa Kutawala Serikali moja”.  Kwani hata “Wahenga walisema tangu lini ”Paka na Panya” hukaa meza moja kujadili “amani na utulivu”.


  Hiyo ni “Dhana ya kufikirika chanya na hasi”.  Nchi zote zenye utawala wa Ubia wa itikadi za “Siasa na Dini” amani si sawia ndani ya janii ni “kufa, kukimbia, vurungu, migomo, migogoro, Malumbano, Wanawake kubakwa na Maandamano” ya kutaka haki, neema na utajiri bila kuwajali Wanyonge.


·        Tarehe 13/04/2001 na 19/04/2001 niliwahi kumuandikia Waziri wa Mambo ya nje wa Tanzania kueleza hali ya “Amani, Utulivu, Ulinzi na Usalama” , kwa nchi za DRC, Burundi, Tanzania hali ya kisiasa sio nzuri, OAU kutoelewana, E.A.C  kuvutana juu ya tawala za nchi zinazoongozwa na Marais Mseveni Chiruba, Mugabe, Bushi, Obasanjo, Buyoya na Kagame Nchi zao zina hali mbaya kiutawala kuanzia tarehe 03/05/2001 hadi 03/09/2001.  Wananchi hawawataki, ila wanatawaliwa kwa ubabe au udikteta.


·        Tarehe 11/09/2001 nilimwandikia Rais Benjamini William Mkapa juu “Kuvunjika Amani, Tanzania, Afrika na Duniani”. Hakupuuza alifuatilia yote niliyomweleza yote niliyomweleza kwa Tanzania.  Tarehe 17/09/2001 alinijibu kuwa endelea kuelimisha juu ya “Amani,utulivu, ulinzi na usalama” kwa Tanzania Afrika na Dunia kwa jumla.  Mpaka sasa namshukuru sana kwa nasaha za Rais Mstaafu “Benjamini William Mkapa” kwa kunipa “Ushupavu na Ujasiri” wa kuongelea masuala ya “Amani Utulivu, Ulinzi na Usalama” Tanzania Afrika na Dunia kwa ujumla.


·        Tarehe 26/09/2001 nilimwandikia barua kwa kumwambia Rais nifanye uzinduzi wa kumwenzi “Hayati Mwalimu J.K. Nyerere” tarehe 30/09/2001.  Barua hiyo sikujibiwa na zoezi nilisitisha sikufanya.


·        Tarehe 30/09/2001 niliandaa mada za uzinduzi wa Amani Duniani za kumuenzi Hayati Mwalimu J. K. Nyerere lengo ilikuwa kwenda kumpatia ujumbe Col. Gaddaf juu ya Amani Duniani, kwa ndoto yangu ya tarehe 13/10/1999 ya Mwalimu J. K. Nyerere aliyeletwa na Malaika watatu kwangu na kutoa maagizo kwamba Col. Gaddaf asimamie masuala ya “Amani na Utulivu” katika Afrika usipopeleka ujumbe huu “machafuko mengi Afrika na ulimwengu yatatokea makubwa” nilitaka kumpa mkono Malaika walisema acha hii ni “Dahari” aliniaga kuwa anakufa, ni kweli alikufa tarehe 14/10/1999.  Mambo yote niliyoota kwa kuagizwa na Mwalimu J. K. Nyerere yanatokea.


·        Tarehe 03/10/2001 Niliandika barua kwa Rais kuelezea hali ya amani katika Taifa baada ya kufanya Ziara katika Mikoa mitatu (3) (Iringa, Morogoro na Mbeya) kwa kufanya utafiti wa “Amani na Utamaduni” ndani ya jamii ya watanzania kutoweka.


·        Tarehe 08/10/2001 niliandika tena barua kwa Rais Benjamini William Mkapa kuomba ufadhili wa kumuenzi Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Baba wa Taifa) kwa ajili ya kwenda Libya kuonana na Col. Gaddaf, kupeleka ujumbe wa ndoto ya tarehe 13/10/1999.


·        Tarehe 14/10/2002 niliandika Makala juu ya Umuhimu wa “Amani” (Tanzania, Africa na Duniani) zoezi halikufanyika kwa sababu ya ukata wa maisha iliyonayo mpaka sasa.


·        Tarehe 18/11/2001 nilimwandika Rais BW. Mkapa juu ya Kero Malalamiko na dalili za kuvunjika amani. niliandika barua kwa Rais kueleza “Vigezo vinavyochochea vurugu, Migogoro na Kuvunja Amani” kwa Makamanda.

KUDAI MADAI YA HAKI ZANGU KWA KUONELEWA TANGU MWAKA 1992.
·        Ukweli wa madai yangu ni kwamba, kesi yangu ya kudai haki ilianza 1992 na kwisha 5/01/2006 nilishinda, lakini bado MMJ kunilipa pamoja na wenzangu watatu, ni kwa sababu ya urasimu wa baadhi ya Makamanda wa MMJ kwa kutozingatia NDA.

KUFANYA KAZI NDANI YA CCM TANGU 2003 HADI 2012.
·        Mwezi wa Machi 2003 nilichukuliwa na CCM na kuwa Katibu Msaidizi wa Wilaya ya Temeke na Mlezi wa Jimbo la Kigamboni Dar es salaam kwa kufanikisha chaguzi za TAMISEMI, na uchaguzi Mkuu wa Dola 2005, CCM ilishinda 100% (kwa Wabunge, Madiwani, Viti maalum wabunge na viti maalumu Madiwani). Vyama vya upinzani vilishangaa kushindwa.
·        Mwenzi Mei, 2006 hadi Oktoba, 2008 nilikuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Maswa Shinyanga. 


Tarehe 23/10/2007 Nilikata Tiketi Kituo cha Ubungo, Basi la Zakaria Coach Limited (A.M.Coach) la kutoka Dar es salaam kwenda Mwanza. Usiku niliota ndoto Malaika watatu walisema hakuna kusafiri, nilipoamka asubuhi nilifikiri zile ndoto kuwa nilishazoea kuota tangu udogo wangu, hao Malaika watatu hunijia kwa njia ya ndoto, niliota nimeumia Mkono wa Kulia, asubuhi nilichukua Karatasi na peni ili nijaribu, kuandika kwa Mkono wa kushoto, nilishindwa, nilisema hizi ni ndoto tu. 


Asubuhi tarehe 24/10/2007 nilisafiri kwa Basi la “Zakaria Coach Limited” (AM Coach) tulipofika Iguguno Singida Basi liligonga Lundo la Kifusi, mimi nilisema “ewe Mwenyezi Mungu heri kufa kuliko kuvunjika vunjika hakuna wa kuniuguza” Abiria wote waliniangalia mimi. Basi lilipinduka magurudumu juu, niliumia Mkono wa kulia na usoni, nilivunjika vidole vinne Karoso kidole gumba.


 Hospital Singida wakati wananipa matibabu, chumba kiligeuka na kuwa cha njano, watu wote sikuwaona ila niliwaona vivuli vya watatu wamepiga magoti na mikono yao waliweka kifuani mwao nilisikia, sauti kuwa huwezi kufa bado utapewa kazi ya kufanya Ulimwanguni nilipozinduka nilimwona Daktari na wenzake wananifunga vidonda.


 Kesho yake nilipelekwa Muhimbili kwa Ndege ndogo iliyokodiwa na CCM Taifa. Nililazwa Wodi ya MOI Muhimbili, Daktari aliyekuwa ananihudumia ni Dr, Paul G. Marealle. Lakini dawa za kunywa nilitumia Dawa asili bila Daktari kujua.


·        Mwezi Oktoba, 2008 hadi Septemba, 2010 nilikuwa Katibu wa CCM Wilaya Bukombe Shinyanga.


·        Tarehe 5/5/2010 niliota ndoto nikiwa Dar es salaam, Malaika watatu walisema hakuna kusafiri. Nilimuambia Mhe: Mbunge Ndugu Emanuel Luhahula, mimi nilimwambia kwa leo tusisafiri, tusafiri kesho. Yeye aliniambia hapana, lazima tusafiri leo. Tulisafiri Tarehe 6/5/2010, tulipofika sehemu ya Nasihukulu Kata ya Bukombe saa 3:20 usiku tulivamiwa na Majambazi, tuliporwa fedha, simu na vifaa mbalimbali pamoja na kupigwa mapanga. Mimi nilikatwa kwa panga kichwani upande wa kulia. Lakini aliyenikata nilimwambia kuwa heri uniuwe kuliko kunkatakata, kwani mpaka sasa nina mkono moja tu, aliondoka.


·        Mwezi Septemba, 2010 Hadi sasa 2011 nilikuwa Afisa wa CCM Makao Makuu Idara ya Organaizesheni. Nilibaini mapungufu ya utawala.


·        Tarehe 21/05/2011 walikuja Malaika saba na kuniambia nifunge kuanzia tarehe 23/05/2011 hadi 24/6/2011 ili nichukue jukumu la Kutibu watu na Amani Ulimwenguni, ni sisi Malaika saba tutakusimamia, tumeongezeka Malaika wanne sasa tuko saba.


·        Tarehe 24/06/2011 mimi“Nililaani, Nilikemea na kutoa Tamko” juu ya Vita Ulimwenguni. Pia nitaendelea kutibu watu kwa kutumia Dawa asili kama nilivyoambiwa na Malaika kwa njia ya ndoto. Mimi mwenyewe hutumia Dawa za Asili. Huwatibu watu wenye magonjwa tatanishi pia nafanya utafiti.


 Mimi Mberito K. Magova, kama nilivyofunga tangu tarehe 23/05/2011 hadi tarehe 24/06/2011 kwa maelekezo ya “Roho mtakatifu” kwa kuleta kwangu Malaika saba (7). Mimi sioni haya kusema mambo matatu juu ya “Amani , Utulivu, Ulinzi na Usalama” Katika Tanzania na Ulimwengu kwa ujumla kwa mambo yafuatayo:-
1.   Mimi “Nalaani” pia nashauri Serikali iwe makini sana kwa masuala mbalimbali yanayojitokeza ndani ya jamii katika Taifa letu. Ni hatari sana Tanzania kutokea vurugu na maafa ya kutisha katika Taifa.


a.   Baadhi ya vyama vya Siasa, kusema uongo, kuchochea jamii kuandamana, Migomo, Migogoro, Vurugu na Kudai fedha ni zoezi ambalo litavuruga “Uhuru, Uzalendo, Demokrasia, Amani, Utulivu, Ulinzi na Usalama katika Taifa letu”. Tutajutia kimaisha.


b.   Baadhi ya Vyama vya Siasa kuchochea wananchi ambao hufanya shughuli za machimbo, wafugaji, wafanya biashara wadogowadogo na wakulima kupambana na wawekezaji, pia kupambana na vyombo vya Dola vyenye Silaha ni dhana ya kuvuruga suala la “Ulinzi na Usalama katika Taifa”.


c.    Baadhi ya Vyama vya Siasa kuvuruga Muungano wa Tanzania, kusema Katiba ya Tanzania ina “Viraka” na wengine wanasema Katiba ina “Ukakasi” ni dhana ya kuutukana Umma (Serikali). Katiba ya Jamhuri ya Muungano ni ya Umma sio ya Vyama vya Siasa au Taasisi yeyote.


d.   Ni vitendo vya aibu kwa baadhi ya Vyama vya Siasa kuwatukana viongozi, kuwatuhumu kuwa mafisadi na wizi bila kuwapeleka kwa vyombo vya Shereia au kutoa ushahidi dhidi ya watuhumiwa, ni dhana ambayo itawagawa Watanzania.


e.    Wabunge kwenye Bunge kuingiza “Itikadi za Vyama” na kuacha kuongelea Uchumi maendeleo na huduma za jamii “Mijini na vijijini”, ni kitendo cha kutotenda haki kwa umma.
f.     Baadhi ya viongozi wa vyama vya Siasa kuwatumia wanafunzi wa vyuo vikuu kuvunja “Amani na Utulivu” kwa njia ya “Vurugu na Maandamano”, ni kuandaa kumwaga damu. Kwa sasa vyama vya Siasa na Dini ni hatari ulimwenguni.


g.    Baadhi ya Wabunge kila siku kuibua historia za “Ufisadi, DOWANS, EPA, Lichmond na kusema Serikali tangu ipate Uhuru haijafanya chochote, ni kuwahadaa wananchi, hata wao waeleze tangu tupate Uhuru wamewafanyia nini wananchi. Wananchi wana washangaa, Wabunge kwa kutokuwa wakweli. Pia Wabunge kwenye Bunge, wanahoji Serikali ina mpango gani na maendeleo kwa wananchi. Je! Wao Wabunge kwenye Majimbo yao wana mpango gani wa maendeleo ya wananchi? Maajabu hata ndani ya Bunge wabunge hutoa hoja binafsi siyo hoja za wananchi.


2.   Mimi “Nakemea” kwa mambo yafuatayo:-
a.   Wananchi kupambana na Polisi ni kitendo cha hatari sana katika Taifa letu lenye dhana ya “Upendo,Umoja na Mshikamano wa Kizalendo” vitatoweka ndani ya Taifa, maafa mengi yatatokea ndani ya jamii, hasa kwa wazee na walemavu ambao hawahudumiwi.


b.   Baadhi ya watu kufanya biashara ya “Dawa za kulevya, Bangi, Milungi na kutengeneza Noti bandia” (Fedha bandia) ni kuwa na utawala ovyo.


c.    Baadhi ya Wanaume kuwabaka wanawake na kuwalawiti watoto wadogo, ni vitendo vya kulaaniwa na Umma wa Tanzania.


d.   Nakemea baadhi ya “Viongozi na Watendaji” wanaoiba fedha za Umma na kununua magari na kujenga nyumba nyingi za kifahari wakati wananchi wanakabiliwa na “Ukata” wa maisha na makazi kuwa duni, Watanzania wasiwe na haya kuwasema na kuwakemea, viongozi na watendaji wasiowajibika.


e.    Nakemea baadhi ya magazeti kuandika mambo ya uongo na uchochezi kwa kuwasema viongozi na watendaji wa Serikali ya Chama Tawala, kuwa ni mafisadi bila kuwa na ushahidi, au kuwapeleka Mahakamani ni kuzidhisha vitendo vya ovyo katika Taifa. Watu wanaotuhumiwa wapelekwe kwenye vikao vya “Usalama na Maadili”, kwenye vyama vya siasa au wapelekwe “Baraza la Maadili na Mahakamani” ili haki itendeke, sio kuwasema kwenye vyombo vya habari na kwenye mabaa au vijiwe.


3.   Mimi “Natamka” mambo yafuatayo kwa Ulimwengu UN na AU wameshindwa juu ya “Amani,Utulivu, Ulinzi na Usalama” kwa Afrika na Ulimwengu kwa ujumla, kwa sababu wanaoneana haya, kuchukua hatua kwa Viongozi wanaotawala kwa kutumia vyombo vya dola (Majeshi ya ulinzi), kwa manufaa yao.
a.   NATO waache kuwaua watu wanyonge na kuharibu miundo mbinu Libya, masuala ya Demokrasia ni ya Walibya wenyewe siyo (AU, EU na UN).

b.   Migogoro ya Kisiasa kwa nchi zote zinazopigana Ulimwenguni imalizwe na “Wananchi wenyewe” kwa njia ya vikao sio kutumia silaha za kivita.


c.    Mataifa makubwa yaache kupeleka majeshi kwa nchi zenye “Vurugu na Migogoro” pia warudishe majeshi haraka toka nchi zenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.


d.   Nchi zote zenye vita vya wenyewe kwa wenyewe wajiuzulu kuanzia tarehe 16/7/2011hadi tarehe 12/8/2011. Kunzia tarehe 15/8/2011 hadi tarehe 30/8/2011 hali itakuwa mbaya sana kwa “Amani na Utulivu” Afrika na Ulimwenguni yatatokea maafa  makubwa kwa kutokana na “ajali, moto, vurugu”, vita, maandamano, kimbunga, tetemeko na maafa mbalimbali” kwani hakuna wa kumshinda Mwenyezi Mungu.


e.    Sisiti kusema Uhuru wa Sudan Kusini tarehe 9/7/2011 ndoto zangu zinakataa na kuniambia kuna umwagaji wa damu na watu wengi kikimbia kuanzia tarehe 6/8/2011 na kuendelea.
Samahani sana nimeamua kutoboa siri ya ndoto zangu za tangu mwaka 1956 kwa kuagizwa na Malaika watatu (3) kwa sasa Malaika saba (7) mara kwa mara hunijia.


Naomba samahani kwa Watanzania, Waafrika na Walimwengu kwa ujumla. Vielelezo vya barua mbalimbali ambazo niliwahi kutoa ushauri kwa kulingana na kuota ndoto. Nimeambatanisha vielelezo vichache ili mjue ukweli wa ndoto zangu kwa siku za nyuma hadi sasa.

 Hata hivyo bado naendelea kutoa ushauri kwa lolote ninaloota kwa Serikali, pia nashukuru Serikali inachukua hatua za kufuatilia matukio mbalimbali hapa Tanzania Afrika na Ulimwengu kwa ujumla. 


Viambatanisho hivyo ni Taarifa ya tarehe 09/05/2000, Oktoba 2000, Tarehe 11/09/201, 17/Septemba, 2001, 30/09/2001 na 14/Oktoba, 2002, Barua nyingine ninazo wala sihitaji kutoa huo ndio ukweli wa ndoto zangu. 

Nazidi kusema Ulimwenguni “Amani, Utulivu, Ulinzi na Usalama” hakuna ila ni vita na magonjwa.
Naomba samahani sana kwa maelezo ya maisha yangu kwa ufupi.

NDOTO ZA MWISHO NA KUPEWA JINA LA (8 DOHARI)
Kama kawaida yangu kujiwa na Malaika saba kwa kutumwa na Roho mtakatifu saa 08:30 tarehe 26/11/2014 walikuja Malaika saba na kuniambia kuwa sasa tunakuagiza mambo yafuatayo uyatekeleze.
1.   Kuanzia tarehe 07/12/2014 waambie viongozi wa Serikali ulimwenguni kuwa Mungu hapendi damu za watu kumwagika kama kuna kiongozi atakupuuza wewe kumpuuza Mungu.
2.   Mungu atachukua hatua za nguvu za asili kuanzia tarehe 08/12/2014 hadi tarehe 17/12/2015 kwa mambo mbalimbali.
3.   Mikutano haitafanikiwa pia kutakuwa na “Vurugu, Ajali, Moto, Maandamano, Maafa na Vita vibaya sana”.
4.   Tarehe 18/04/2015 jiandae kwenda kutibu ugonjwa wa “Ebola” dawa ulishaonyeshwa bila wewe hakuna wa kutibu pia utatibu magonjwa sugu.

5.   Kwa sasa Roho Mtakatifu amekupa jina unaitwa “Nane Dahari” maana ya jina hilo iko siku utaambiwa.  Andika ndoto zote na kuwapa mataifa bila woga.
6.   Mimi nilipoamka sikuamini wale Malaika saba waliokaa mbele yangu na kuelekea kaskazini sikuwaona. 

Ndipo nilipoandika maagizo. Mimi kuota “ndoto na maono” ni tangu mwaka 1956 mpaka sasa 2015 na yote yametokea na yataendelea Ulimwenguni.
7.   Namshukuru sana Mungu kunipa “Kipaji, Karama na Kipawa” kwa kuota masuala yatakayotokea.
8.   Mimi nakiri si “Mungu, Roho, Yesu na Muhamadi” ni mtu wa kawaida ila yote yatatokea.
9.   Nazidi kuomba samahani kwa Tanzania, Afrika na Ulimwengu kwa ujumla kwa sasa jina langu ni (8 Dahari).

Wenu katika Ujenzi wa Taifa,

………………………………………….
Lt. Mberito Kimvelye Magova (mst)
(MBEKIMA)
“HAKI ITATAWALA DUNIA, KAMWE DUNIA HAITATAWALA HAKI”









Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com