Chama
cha demokrasia na maendeleo (Chadema) kimesema muda wa mwezi mmoja
uliotolewa na tume ya taifa ya uchaguzi ( NEC ) hautoshi kuandikisha
wananchi zaidi ya milioni 24 katika daftari la kudumu la mpiga kura kwa
kutumia mfumo mpya wa Biometric Votres Registration ( BVR ), badala yake
wameitaka serikali kuongeza muda wa miezi minne zaidi.
Mwenyekiti wa chama hicho Mh. Freeman Mbowe, akihutubia maelfu ya
wakazi wa Mwanza na mikoa jirani ya kanda ya ziwa katika mkutano wa
hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Furahisha jijini Mwanza, amesema
muda wa siku 30 uliotolewa na tume hiyo kwa ajili ya kuandikisha
wapiga kura hautoshi kutokana na tume kutokuwa na vifaa vya kutosha na
pia ikizingatiwa kuwa mtu mmoja anatumia dakika 5 hadi 10 kuandikishwa
kwenye daftari hilo.
Kwa upande wake naibu katibu mkuu wa Chadema – Zanzibar, Salum
Mwalimu amesema uamuzi wa Chama cha mapinduzi kuwapa onyo baadhi ya
wanachama wake, wakiwemo wajumbe wa kamati kuu ambao wametangaza mapema
nia ya kugombea nafasi ya urais, itakayoachwa wazi na rais Jakaya
Kikwete baada ya uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu ni ishara na dalili za
wazi kwamba chama hicho hakijajiandaa kisaikolojia kuwa chama cha
upinzani kutokana na nguvu kubwa inayoonyeshwa na Chadema pamoja na
Ukawa.
Wakizungumza katika mkutano huo mkubwa, baadhi ya wabunge
wanaotokana na chama cha demokrasia na maendeleo akiwemo mbunge wa
Arusha mjini Mh. Godbless Lema pamoja na mwenyekiti wa taifa wa baraza
la vijana wa Chadema ( Bavicha ), Patrobas Katambi wamewataka watanzania
kupigania nchi yao kwa mambo ya msingi bila uwoga ili rasilimali zilizopo
ziweze kuwanufaisha wananchi wote.
Via>>Itv
Social Plugin