Jeshi
la polisi mkoa wa Geita limewakamata waganga wa kienyeji 32 wanaopiga
ramli chonganishi katika msako uliofanywa hivi karibuni ili kuhakikisha
mauaji ya vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi yanakomeshwa kabisa.
Akizunguza na waandishi wa habari baada ya kufanya msako na
kuwakamata waganga hao kamanda wa polisi mkoa wa Geita Sacp Joseph Konyo amesema waganga hao wamekamatwa wakiwa na vifaa mbalimbali
ambavyo ni matunguri na ngozi za wanyama kama vile simba chui na
nyati vikiwa vimekaushwa.
Kamanda Konyo mesema sasa wakati umefika wa kuhakikisha mauaji yanayotokana na imani
potofu za kishirikina yanakomeshwa na ili kuyakomesha watu wa kwanza
kudhibitiwa ni waganga wa kienyeji wanaofanya shughuli zao pasipo
kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa na nchi.
Kamanda Konyo amesema upo ushahidi wa wazi unaonyesha mahusiano ya
karibu ya mauaji haya ya vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi na
waganga wa kienyeji kwani ndio wahusika wanaoagiza viungo vya Albino na
ndio hao wanaopiga ramli za uongo kuonyesha kuwa vikongwe hasa wanawake
ndio wachawi.
Ameongeza
kuwa jeshi la Polisi haliwezi kuhangaika
na watu wengine wakati huku waganga ndiyo wanaosababisha mauaji hayo ya
walemavu wa ngozi na vikongwe huku wakisababisha wananchi kuacha kufanya
shughuli zao za kila siku
Kamanda Konyo amesema serikali haiwezi kuvumilia waganga wa namna
hii wanaoipotosha jamii hivyo msako huu utaendeshwa katika mikoa yote
Tanzania bara ili kubaki na jamii salama isiyokuwa na vitisho vya mauaji
ya kikatili kama haya.
Baadhi ya wananchi mkoa wa Geita wameipongeza hatua ya serikali
kuanza sasa kuwachukulia hatua watuhumiwa wote wanaopatikana na tuhuma
za mauaji yanayotokana na mila potofu na ushirikina.
Na Valence Robert -Malunde1 blog Geita