Wakati msako wa kukamata wapiga ramli chonganishi
ukiendelea nchi nzima hasa katika mikoa ya kanda ziwa, jeshi la polisi nchini
limepewa onyo kali kutoka kwa waganga wa jadi juu ya vifaa vinavyokamatwa
wakati wa msako huo.
Jeshi hilo limepewa tahadhari ya kukumbana na
hatari yoyote wakati wa baadaye, ikiwa litaendelea kukamata vifaa hivyo
vikiwemo vibuyu, vitambaa vyeupe na vyeusi, ngao, mikuki, pamoja na shanga huku
likitakiwa kurejesha mara moja baadhi ya vifaa hivyo ambavyo vimekamtwa.
Tahadhari hiyo ilitolewa jana na Katibu Mwenezi wa
chama cha waganga wa Tiba Asili Tanzania (CHAWATIATA) Bw. Steven Sebastian
kutoka Mkoani Mwanza, wakati akiongea katika Mkutano wa waganga wa jadi Wilaya
ya Bariadi Mkoani Simiyu uliofanyika katika ukumbi wa CCM Bariadi.
Katibu huyo akiongea mbele ya Mkuu wa polisi
Mkoani Simiyu Charles Mkumbo alisema kuwa kitendo kinachofanyana jeshi hilo cha
kukamata vifaa hivyo, ni kitendo cha hatari kwani kinaweza kusababisha hali ya
migogoro mikubwa kati ya jeshi la polisi na jamii.
Sebastian alieleza kuwa vibuyu, vitambaa vyeupe,
na vyekundu, shanga, ngao, pamoja na mikuki, ni vifaa ambavyo waganga hao
walirishwa na wazee wa zamani ambao alieleza kuwa vifaa hivyo walivitumia
katika kutafuta uhuru.
Aidha alisema kuwa endapo zoezi hilo litaendelea
bila ya kusitishwa upo uwezekano mkubwa na wazee hao wa zamani kukasirika kwa
kiasi kikubwa kutokana na kugusa vifaa vyao ambavyo walivirisisha kwa watoto
wao ambao ni waganga wa jadi wanatuhumiwa kupiga ramli chonganishi.
“ Nitoe tahadhari mbele yako Mkuu wa polisi msako
huu unaoendelea umelenga kusambaratisha jadi wakati ndizo zilizotumika kuleta
uhuru…vifaa hivi vinavyokamatwa virejeshwe mara moja…wazee hawa wakikasirika hakuna
hatakaye baki ndani ya jeshi la polisi..msitake kugombana na mila..gomba na
wanapiga ramli chonganishi..lakini chonde chonde rejesheni vibuyu vyetu haraka”
Alisema Kiongozi huyo
Alieleza kuwa viongozi wa zamani wa makabila
mbalimbali ( machifu) walikuwa wanatumia vifaa hivyo kufanyia kazi mbalimbali
ambazo alisema kuwa zilikuwa zinatumika vizuri na siyo kuwa zinatumika katika
kuua watu kama inavyodhaniwa.
Alisema kuwa wazee hao wanaweza kukasirika wakati
wowote kuanzia hivi sasa ikiwa vibuyu vyao vitaendelea kukamatwa, sambamba na
vingine vitashindwa kurejeshwa kwa wamiliki wao waliowaachia.
Alilitaka jeshi hilo kuacha mara moja kupeleka
chuki za moja kwa moja kwa waganga wa jadi ambao wanatumia vifaa hivyo kwa nia
njema, na badala yake chuki hizo zielekezwe kwa wanaopiga ramli chonganishi.
Aidha Katibu huyo alisema kuwa kwa watuhumiwa
wanatakaobainika ndiyo chanzo cha kuuawa au kukatwa kwa viungo vya watu wenye
ulemavu wa Ngozi (Albino), alitaka adhabu yao iwe kunyongwa hadharani.
Akiongelea hoja hiyo Mkuu huyo wa polisi Mkoani Simiyu alieleza kuwa siyo kweli kuwa waganga wa jadi wanaonewa au kusingiziwa
kuwa hawapigi ramli chonganishi bali katika uchunguzi wao wamebainika kuwa
ndiyo chanzo kikuu.
Aliwataka waganga ho kuacha mara moja vitendo
hivyo, huku akiwataka kila mmoja kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja anapatiwa
leseni au kujiandikisha kwa viongozi wao wa vijiji au mtaa ili kuweza kukwepa
msako mkali utakaoanza baada ya mwezi mmoja.
Hata
hivyo waganga hao walifanya uchaguzi katika Mkutano huo ambapo walimchagua
Mayunga Kidoyai kuwa Mwenyekiti, Shinyanga Isamila Makamu Mwenyekiti, Njile
Kasula Katibu, pamoja na John Kunini ambaye alichaguliwa kuwa Katibu Msaidizi.
Via>>simiyunews blog
Social Plugin