Jana ilikuwa siku ya hisia tofauti kwa watu wawili wanaotajwa kwenye kinyang’anyiro cha urais, Edward Lowassa na Lazaro Nyalandu baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kumsifu mmojawao na kumponda mwingine.
Akiwa
Kondoa, Kinana alitumia muda mwingi kujibu kilio cha wananchi
wanaosumbuliwa na askari wa wanyamapori kwa kumponda Waziri Nyalandu
kuwa anazurura bila kushughulikia matatizo ya wananchi, lakini saa
chache baada ya kuwasili Monduli alimsifu Lowassa kuwa ni kiongozi
shupavu.
Tayari
Nyalandu ameshatangaza nia ya kugombea urais, wakati Lowassa, mmoja wa
wanachama wa CCM wanaotajwa sana kwenye kinyang’anyiro hicho,
hajatangaza uamuzi wake lakini anatumikia adhabu ya chama chake
kilichomfungia kujihusisha na harakati za uongozi pamoja na makada
wengine watano.
Baada
ya msafara wa Kinana kuwasili Monduli na kupokewa na viongozi wa chama
hicho wa eneo, katibu huyo wa CCM, Kinana alipata nafasi ya kuzungumza
machache kabla ya kuanza safari ya kukagua shughuli mbalimbali.
“Hatuna
shaka na Monduli kwa kuwa yupo kiongozi shupavu, ndugu yetu Waziri Mkuu
mstaafu na mjumbe wa (Halmashauri Kuu ya CCM) Nec,” alisema Kinana akiwaelezea wananchi waliokuwapo eneo hilo.
“Wa Monduli mna kiongozi shupavu na mchapakazi. Hongera Bwana Lowassa.”
Baadaye, Lowassa aliwakaribisha akisema: “Mmefanya kazi kubwa sana ya kukijenga chama chetu. Nawashukuru sana, karibuni.”
Naye katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema:“Nafurahi kuwa katika jimbo la mzee wangu, rafiki yangu Edward Lowassa. Mapokezi mazuri, bila shaka Arusha mmeamka.”
Kinana
amekuwa akitumia sehemu kubwa ya ziara yake kushuhutumu viongozi wa
Serikali na hasa mawaziri kwa kushindwa kuwatatulia wananchi matatizo
yao na ilifikia wakati aliwataja mawaziri wanne aliowaita kuwa ni
mizigo, tofauti na alivyofanya kwa waziri mkuu huyo wa zamani.
Lowassa
alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne na
anajulikana kama mtu aliye tayari kufanya uamuzi mgumu. Alilazimika
kujiuzulu wadhifa huo mwaka 2008 baada ya kuibuka kwa kashfa ya
Richmond.
Kinana
alikuwa mtu tofauti wakati akijibu kero za wananchi mkoani Singida,
ambako alimtaja moja kwa moja Waziri Nyalandu kuwa hashughulikii
matatizo ya wananchi na badala yake amekuwa akizunguka bila msaada
wowote.
Kinana
alisema hayo juzi katika Kijiji cha Ikengwa, Kata ya Kinyasi wilayani
Kondoa baada ya wananchi wa kijiji hicho kumchongea Nyalandu kwa Kinana
kwamba wizara yake inawaua na kuwaumiza bila ya hatia, hivyo wamechoka.
Wananchi
hao walisema mateso wanayoyapata kutoka kwa askari wa wanyamapori
katika Pori la Mkungunero ni makubwa ambayo yanalenga kuondoa uhai wa
watu.
Katibu
wa CCM wa Kata ya Inyasi, Jusberi Jumanne aliyesoma risala ya
malalamiko hayo, alisema wanaishi ndani ya kijiji chao na kufanya
shughuli zao za kilimo, lakini kila wakati wanachomewa nyumba, mazao yao
kufyekwa na hata kuwasababishia ulemavu na vifo.
“Mheshimiwa
katibu mkuu, hapa ni kijiji halali kilichosajiliwa 1974 na kupewa hati
398, lakini hifadhi hiyo ilikuja kuweka mipaka yao mwaka 2006, jambo
hili sisi tunaona ni uonevu ambao tunafanyiwa bila ya kushirikishwa na
kuambiwa tuhame kwa nguvu na hatujui mahali pa kwenda,” alisema.
Akijibu
hoja hiyo Kinana alionekana kukerwa na namna maisha ya watu wa maeneo
hayo yasivyoshughulikiwa ili nao waishi kama Watanzania wengine.
“Ni jambo la aibu kwa Waziri wa Maliasili na Utalii kusikia migogoro lakini yeye akawa kimya,”alisema Kinana.
“Nyalandu
awaeleze Watanzania kama kuna mahali amefanikiwa kumaliza kabisa
migogoro walau 10 kwani amekuwa ni bingwa wa maneno na matembezi.”
Kinana
alisema ni lazima Nyalandu abebe msalaba huo kwani roho za binadamu
zina thamani… ni heri roho ya binadamu kuliko mnyama ingawa alizuia
wanyama wasiuawe.
“Hawa
mawaziri lazima waje, na nina wasihi waje haraka, yaani Waziri wa
Maliasili na Utalii na mwenzake wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi,” alisema.
“Mfano
ni Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye anafanya kazi ya kuzunguka nchi
nzima na maeneo mengine wakati mizunguko yake haisaidii kuondoa
matatizo ya wananchi.”
Kinana
alitaka kamatakamata ya wananchi isimamishwe kwanza hadi ufumbuzi
kuhusu mipaka ya pori hilo itakapoangaliwa upya. Alipoulizwa kuhusu
tuhuma hizo, Waziri Nyalandu alisema anakubaliana na alichosema Kinana,
lakini akataka watu wajue kuwa mgogoro huo ni wa muda mrefu.
“Mgogoro
huo ni wa siku nyingi, hivyo busara inahitajika sana kulinda watu, mali
zao na maliasili. Niliunda kamati ambayo yumo Mkuu wa Wilaya ya Dodoma
na Manyara, Ma-RAS (maofisa utawala wa mikoa) wao na Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii ambayo imefanya uchunguzi pamoja na kuongea na
wananchi,” alisema.
“Kamati
inatarajiwa kumaliza kazi wiki hii na itanikabidhi kwa kuwa mimi ndiye
niliyeiunda. Nimepanga kwamba ndani ya hizi wiki mbili za Bunge, mimi na
Waziri wa Ardhi tutatangaza suluhisho la tatizo hili. Tutaenda pamoja
Mkungunero kuongea na wananchi.”
Katika
mkutano huo, Mbunge wa Kondoa Kaskazini, Zabein Mhita alisema kuwa
katika kata hiyo na maeneo mengine kumekuwa na kelele zinazotishia amani
na tayari kwa baadhi ya watu wameshapoteza maisha.
Walimkabidhi Kinana maganda ya risasi pamoja na rundo la mabaki ya nguo zilizochomwa moto na askari wa wanyamapori.