Hali ya taharuki imetanda katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha baada
ya kugundulika mahali walipofichwa watoto17 wakiwamo watatu wa familia
moja wanaodaiwa kupotea tangu mwezi Februari mwaka jana kwa madai ya
kufundishwa maadili ya imani ya dini ya kiislamu.
Umati mkubwa wa wakazi wa mji wa Moshi wamejitokeza katika kata ya Pasua mjini Moshi kushuhudia tukio la watoto hao wenye umri wa kuanzia
miaka miwili hadi 13 ambao walikuwa wanaishi kwa Bw.Abdelnasir
Abrahamani ambaye ni mfanyabiashara wa nguo nchini Kenya.
Akizungumza katika eneo la tukio mkuu wa wilaya ya Moshi Bw.Novatus
Makunga amesema tatizo hilo kwa mji wa Moshi ni kubwa na kwamba kwa
sasa nyumba hiyo imefungwa na kuondolewa watoto hao ili warejeshwe kwa
wazazi hao wakati hatua za kisheria zikiendelea.
Mmoja wa wazazi mwenye watoto watatu waliopotea tangu mwezi
February mwaka jana na kukutwa katika nyumba hiyo Bw.Ramadhani Mohamedi
amesema aligundua tukio hilo baada ya kukutana na mtoto wake wa kike
barabarani na kumweleza mateso wanayoyapata huko.
Naye mfanyabiashara huyo Bw.Abdulinasir Abrahamani amesema nyumba
hiyo ni familia na ndugu zao wa kiislamu lakini siyo kituo cha yatima,
ila ni sehemu ya kutolea mafundisho ya dini ya kiislamu.