KUHUSU VIGOGO WA CCM ( Watangaza Nia) KUHAMA CHAMA WAKIPIGWA CHINI KWENYE KURA ZA MAONI

 

Kufuatia kuwepo kwa tetesi kuwa baadhi ya Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi  wa CCM watakihama chama mara baada ya kushindwa kura za maoni,mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga,Khamis Mgeja,amewaondoa hofu wanachama wa chama hicho  na wananchi kuwa hakuna atayehama na kwamba watabanana hapo hapo.

Mgeja alitoa kauli hiyo katika Kijiji cha Kangeme Kata ya Ulowa wilayani Kahama wakati wa sherehe za ushindi wa serikali za mitaa na vitongoji ambapo CCM ilishinda kwa asilimia mia moja katika Kata hiyo.

Mgeja aliwataka kuzipuuza taarifa zinazoenea kuwa miongoni mwao watahama CCM huku akiwaomba kutokuwa na mashaka ya kutokea mpasuko ndani ya chama katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Mwenyekiti huyo alisema ingawa kuna baadhi ya viongozi ndani ya Chama kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari wamediriki kudai kuna baadhi ya wanaonyesha nia katika nafasi mbalimbali za uchaguzi kupitia CCM, kuwa watajiengua pindi watakaposhindwa kura za maoni,alidai maelezo hayo siyo ya kweli bali yana nia ya kuwaogopesha wana chama na Watanzania kwa ujumla.

“Ndugu zangu ndani ya CCM kuna wanachama wakomavu,na waliowekeza jasho lao jingi kwa muda mrefu ndani ya chama,hawa wanajua kushinda na kushindwa na hasa kwa kuwa chaguzi za ndani ya chama huwa tunapangana,hatushindani,ndiyo maana mwaka 1995,Rais Kikwete alikubali matokeo na leo ndiyo Rais wetu,huyu ni kiongozi mkomavu na mvumilivu anayestahili kuigwa ndani ya chama,hivyo hakuna atakayehama tutabanana mpaka kieleweke dakika 90”,alisema Mgeja.

Aliwaomba wanachama wa CCM kuendelea kuwa na imani na chama chao hasa kwa kuwa haki itatendeka,kwa kila mwanachama atakayegombea nafasi ya udiwani,ubunge na urais katika uchaguzi mkuu ujao. 

Mgeja alisema  kuna baadhi ya viongozi na genge la watu wachache wamekuwa wakisambaza maneno ya kuwatia hofu wanachama na watanzania kuwa kuna baadhi ya wagombea watakatwa majina yao.

Alisisitiza kuwa Chama hakijawa na ajenda hiyo wala kuweka kwenye vikao,na kudai kuwa huo ni mkakati mchafu wa baadhi ya wagombea na wapambe wao kutaka kuchafuana na hasa wagombea wanakubalika kwa wananchi.

Aidha alionya viongozi wa Chama kulazimisha kuwachagulia wagombea wananchi,jambo ambalo limekuwa likiigharimu mara nyingi CCM kwa kushindwa katika baadhi ya maeneo kwenye chaguzi zilizopita,hivyo kuwataka kukubali chaguo la wanachama katika kumpata mgombea na sio viongozi.

“Tuache kubeba wagombea na kuwachagulia wagombea wananchi,nawaomba wanachama na viongozi tujifunze kama Kata ya Ulowa,kwa kuacha mapendekezo ya walio wengi ndani ya Chama, kumesababisha  kupata ushindi wa kishindo wa asilimia mia moja”,alisema Mgeja.

Katika sherehe hizo zilizoambatana na muendelezo wa hafla ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa chama hicho kutimiza miaka 38,Mgeja aliwasihi na kuwaomba wanachama na viongozi wakati wakitimiza miaka hiyo, watambue kuwa CCM imefanya mengi ya maendeleo kwa watanzania hivyo kutumia fursa kuyatangaza kuliko kupoteza muda mwingi kutengeneza mikakati mingi ya kumalizana na kuhujumiana.

Sherehe hizo pia zilikuwa ni za kupongezana kutokana na ushindi waliopata katika chaguzi za mitaa na vitongoji,ambapo Kata hiyo ilishinda vijiji sita vya Kangeme,Ulowa,Ngilimba,Ilomelo,Bugela na Ulowa namba nne na vitongoji 38 na wajumbe wote wa serikali za vijiji.
 Na Kadama Malunde-Kahama

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post