Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAASKOFU WA KANDA YA ZIWA WATOFAUTINA NA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA SUALA LA KATIBA TANZANIA,SIKILIZA SAUTI

Katibu wa kamati ya Mabalozi wa Amani wa Kikristo Kanda ya Ziwa ambaye pia ni askofu wa kanisa Tanzania Field Evangelism(TFE) la mjini Shinyanga Edson Mwombeki akizungumza leo mjini Shinyanga ndani ya kanisa hilo

Mwenyekiti wa Kamati ya Mabalozi wa Amani wa Kikristo Kanda ya Ziwa Askofu Amos Benjamin Madayi wa Kanisa la Elim Pentecoste Tanzania Jimbo la Magharibi
Kamati ya Mabalozi wa Amani wa Kikristo Kanda ya Ziwa inayoundwa na Maaskofu zaidi ya 10 na wachungaji zaidi ya 190 kutoka makanisa ya Kipentekoste imewataka viongozi wa dini na siasa kukaa pembeni,waiache katiba hiyo kama ilivyo na kuwaachia wananchi jukumu la kuipigia kura ya Ndiyo au Hapana badala ya kuwashawishi waipigie kura ya Ndiyo,Hapana au kutoipigia kura kabisa muda utakapofika. 

Tamko hilo la Mabalozi wa Amani wa Kikristo Kanda ya Ziwa limetolewa leo mbele ya waandishi wa habari mjini Shinyanga ikiwa ni siku chache tu baada ya Maaskofu wa Jukwaa la Wakristo Tanzania linaloundwa na Taasisi za Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT), kuwataka  waumini wake wote  wajitokeze kwa wingi kupiga kura ya hapana katiba inayondekezwa muda utakapofika.

Akitoa tamko hilo Mwenyekiti wa kamati hiyo Askofu Amos Benjamin Madayi wa Kanisa la Elim Pentecoste Tanzania Jimbo la Magharibi amesema wameshtushwa na tamko la viongozi hao wa dini kuikataa katiba inayopendekezwa na kwamba matamko kama hayo yanachochea uvunjifu wa amani katika nchi. 


Amesema kamati yao imesoma katiba inayopendekezwa,wameielewa na wanaikubali kwa sababu mchakato wake umepatikana kwa njia ya kupigiwa kura halali,na ili iweze kufanya kazi kama katiba inapaswa kupigiwa kura,hivyo wanahimiza wananchi wote wanaostahili kupiga kura ,wakajiandikishe na wapige kura kwa hiari na ridhaa yao wenyewe.


Naye katibu wa kamati hiyo ambaye pia ni askofu wa kanisa Tanzania Field Evangelism(TFE) la mjini Shinyanga Edson Mwombeki amesema siyo busara hata kidogo kwa viongozi wa dini kushawishi waumini wapige kura ya Hapana na kuwataka wakae pembeni kwani kila mwananchi ana hiari ya kupiga kama anavyofikiri yeye.

Amesema kama viongozi wa dini na wanasiasa wataendelea kutoa matamko ya kuchanganya wananchi amani ya nchi inaweza kuvurugika kwani hivi sasa kuna makundi matatu,likiwemo la wale wanaotaka wananchi wapige kura ya Ndiyo,wengine kura ya Hapana na jingine likishauri wananchi wasipige kura kabisa bali waende kulima siku ya kupigia kura katiba inayopendekezwa.


Katika hatua nyingine askofu Mwombeki ameitaka serikali kutojihusisha na masuala ya  mahakama ya kadhi kwani ni kuunga mkono suala hilo ni kufanya katiba inayopendekezwa Ibara ya 41.3 ikose maana na uzito uliobebwa na katiba inayopendekezwa.
Na Kadama Malunde-Shinyanga
NIMEKUWEKEA HAPA SAUTI WAKATI VIONGOZI HAO WAKITOA TAMKO LAO ,BONYEZA PLAY HAPA CHINI.
Ya Kwanza Askofu Mwombeki 
Ya Pili Askofu Madayi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com