Wimbo wa John Komba aliouimba katika msiba wa Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1999, jana uliibua majonzi na kusababisha
viongozi mbalimbali, akiwamo Rais Jakaya Kikwete, kutoa machozi
ulipoimbwa kumuaga mbunge huyo.
Wimbo huo uliobadilishwa maneno yanayohusu Mwalimu
Nyerere na kuingizwa yanayomtaja mbunge huyo wa Mbinga Magharibi, mbali
na Rais Kikwete ulimliza pia Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, Spika wa
Bunge, Anne Makinda, Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka,
Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba na waombolezaji wengine.
Sehemu ya mashairi ya wimbo huo uliokwenda kwa
jina la “Nani Yule” ulioimbwa na wanamuziki mbalimbali wa bendi nchini,
na kuwatoa watu machozi iliimbwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,
Nape Nnauye.
“Kapteni Komba familia yako umeiacha na nani,
chama chako umekiacha na nani, nenda baba msalimie Mwalimu, mweleze hali
ya Watanzania ilivyo hivi sasa, mweleze hali ya nchi yetu ilivyo hivi
sasa hasa wakati huu, msalimie Mzee Kawawa Simba wa Vita”
Baadhi ya wanamuziki walioshiriki kuimba wimbo huo
ni King Kiki, Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata, Jose Mara ambaye ni
mwanamuziki wa bendi ya Mapacha Watatu na Luiza Mbutu wa African Stars.
Wakati wanamuziki hao wakiendelea kuimba wimbo
huo, idadi ya watu wanaolia ilizidi kuongezeka, hasa wanafamilia ndugu
na jamaa wa marehemu.
Waombolezaji walisikika wakilia huku wakisema,
“Jamani alikuwa akitunga nyimbo kuwaimbia wenzake waliofariki dunia,
sasa leo anaimbiwa yeye.”
Alipofariki Mwalimu Nyerere Oktoba 14, mwaka 1999,
aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Magharibi, Komba akiwa na bendi ya TOT
alitunga nyimbo za maombolezo ukiwamo wa “Nani Yule’, ‘Kwaheri Mwalimu’,
ambazo jana zilitumiwa na wanamuziki kumuimbia yeye, wakibadilisha
baadhi ya maneno.
Mwili wa mbunge huyo (61) aliyefariki dunia
Jumamosi iliyopita kwa ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu, uliagwa
katika viwanja vya Karimjee ambapo salamu mbalimbali za rambirambi
zilitolewa kabla ya mwili huo kusafirishwa kwenda Songea mkoani Ruvuma.
Hata wakati wa kuagwa mwili huo, idadi kubwa ya
wabunge wenzake waliohudhuria walishindwa kujizuia kulia huku
wakikumbushana ucheshi aliokuwa nao Komba enzi za uhai wake.
Pengine msiba huo utakuwa umewagusa wengi
wanaomfahamu kwa mambo mengi, na kwa kuwa kipindi hiki nchi inajiandaa
kupata rais mpya, kwa kuwa kazi yake kubwa ilikuwa ni kuipigia debe CCM
kupitia uimbaji wake.
Kulingana na maelezo ya waombolezaji, Mwanajeshi
huyo aliyestaafu akiwa na cheo cha kapteni alikuwa ni mtu ambaye
hakusita kueleza kile alichokiamini, jasiri asiyekubali kushindwa,
mcheshi wakati fulani na mtu wa kutoa misaada.
Kijana mmoja ambaye alishindwa hata kutaja jina lake kutokana na
kulia kwa uchungu, alilazimika kuondolewa katika viwanja hivyo baada ya
kutaka kwenda kuaga tena mwili wa mbunge huyo, huku akisisitiza kuwa
ndiyo aliyekuwa akimsomesha.
“Kapteni jamani umeondoka, hivi nani atanisomesha
mimi. Niacheni nikamuage kwa mara nyingine huyu ni kama baba yangu
mzazi, nitakuwa mgeni wa nani,” alisema kijana huyo na kuzidisha vilio,
hasa kwa watoto wa marehemu.
Watu kutoka maeneo mbalimbali walifika katika
viwanja vya Karimjee kumuaga mbunge huyo kuanzia saa tatu asubuhi,
akiwamo mama mmoja aliyedai kuwa ametoka mkoani Mwanza kuja kuuaga mwili
wa mbunge huyo.
Huku akilia mama huyo alisema, “Komba baba
nimetoka Mwanza kwa ajili yako jamani, nenda ndugu yangu, nenda tu ipo
siku tutaonana.”
Shughuli hiyo ilianza saa 3 asubuhi kwa wanamuziki
mbalimbali wa bendi, muziki wa kizazi kipya na waigizaji wa filamu
kuimba nyimbo za kumkumbuka mbunge huyo.
Wakazi wa Dar es Salaam walimiminika katika
viwanja hivyo na tofauti na shughuli nyingine kama hizo, hakukuwa na
ulinzi mkali wala watu kukaguliwa na vifaa maalumu.
Mara baada ya viongozi wa Serikali kumaliza kuaga
mwili wa mbunge huyo, wananchi wengine nao walipewa fursa ya kuaga na
kusababisha askari wa Bunge kutumia nguvu ya ziada kuwazuia kutokana na
kutofuata utaratibu uliowekwa.
Watu hao walionekana kuwa na shauku ya kuaga mwili
wa mbunge huyo, baadhi wakilalamikia kitendo cha kuzuiwa na askari hao
wakisema kuwa Komba alikuwa mtu wa watu na wao wana haki ya kumuaga.
Hata hivyo, baadaye askari hao waliwahimiza watu
hao kufuata utaratibu uliokuwa umepangwa na wote wakapata fursa ya kuaga
mwili huo hadi shughuli zilipomalizika saa 7:30 mchana.
Salamu za CCM
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema,
“Sauti ya Komba imezimika lakini imefuatiwa na sauti ya vilio vya watu
waliompenda wakiomboleza. Alikuwa mwalimu, mwanajeshi, kiongozi, mbunge,
mwanasiasa na mwanamuziki mwenye kipaji cha kutunga nyimbo zinazoendana
na wakati.”
Kinana alisema nyimbo zilizotungwa na Komba
zilitumika kuwapa hamasa wanajeshi wa Tanzania waliopigana vita vya
Tanzania na Uganda mwaka 1978 hadi 1979 vilivyouondoa utawala wa Iddi
Amin nchini humo.
“Katika msiba wa Mwalimu Nyerere nyimbo alizozitunga ziliwaliza
Watanzania, atabaki kuwa mfano wa kuigwa. Kifo chake ni pigo wa CCM,
bendi yake, wasanii na wana familia yake,” alisema Kinana na kufafanua
kuwa chama hicho kimetoa rambirambi ya Sh5 milioni.
Kambi ya Upinzani
Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Kambi ya
Upinzani Bungeni, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari alisema
kifo cha Komba kimewagusa wabunge wote bila kujali itikadi zao za vyama.
“Kifo hiki kinatukumbusha kuwa hapa duniani
binadamu tunapita tu. Tunatakiwa kutenda mema kwa ndugu, rafiki na Taifa
letu,” alisema.
Kamati ya Bunge
Mbunge wa Mchinga na Mwenyekiti wa Kamati ya
Maendeleo ya Jamii ambayo Komba alikuwa makamu wake, Said Matanda
alisema kuwa alizungumza na marehemu saa tano kabla ya kufikwa na mauti.
“Tulikuwa tukizungumzia safari ya kamati yetu
kwenda Ethiopia ambayo ilikuwa tuifanye kesho yake (Jumapili iliyopita),
lakini saa tano baadaye nikapata ujumbe kuwa amefariki dunia,
sikuamini,” alisema.
Alisema marehemu alikuwa zaidi ya kiongozi kwa
kutunga nyimbo zenye ujumbe mzuri kwa jamii na alikuwa na uzoefu wa
miaka tisa katika kamati hiyo na ndiyo maana wajumbe wa kamati hiyo
hawakusita kumchagua kuwa makamu mwenyekiti wao.
Salamu za Serikali
Akitoa salamu za Serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu wa Bunge), Jenista Mhagama alimwelezea
Komba kama kiongozi aliyejitolea katika kila jambo.
“Juhudi na mipango aliyoifanya Komba katika jimbo
lake Serikali kupitia ilani ya CCM itatekeleza. Serikali itatoa
rambirambi zake kwa familia ya Komba wakati mwafaka,” alisema.
Ujumbe wa Makinda
Spika Makinda aliwataka Watanzania kuwa na tabia ya kusamehe hata kama wametendewa mambo yanayowakwaza.
“Hapa duniani tunapita tu, hatutakiwi kuwatendea
watu mambo ambayo sisi hatupendi kutendewa. Tusidhani kuwa kila
tunachokitaka na kukiamini kitadumu, si hivyo. Komba ameondoka kama moto
wa kibatali unavyozimika,” alisema.
Makinda alisema kama Komba angepewa dakika 15 za
mwisho kabla ya kufariki ili aseme jambo lolote, ni wazi kuwa angesema
kama kuna aliowakosea wamsamehe.
Alisema binadamu wote ni ndugu na hata wakifa
inaelezwa na viongozi wa dini kuwa wanakwenda kukutana na raha au shida
ambazo zinategemea na matendo yao waliyokuwa wakiyafanya duniani.
“Wanachama wa CCM tunamwombea marehemu na tunaamini kuwa Mungu atatupa Komba mwingine,” alisema.
Salamu za familia
Msemaji wa familia ya Komba, Dominick Mwakangale
alisema mwili wa mbunge huyo ambao baadaye jana jioni uliagwa na wakazi
wa Songea, utazikwa leo kijijini kwake Lituhi wilaya ya Nyasa mkoani
Ruvuma.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria ni Rais mstaafu,
Benjamin Mkapa, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, Katibu Mkuu
Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip
Mangula na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa.
Wengine ni Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(Nec) Jaji Damian Lubuva, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis
Mutungi, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Hussein Katanga, Katibu wa Shughuli
za Bunge John Joel, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju,
Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Meya wa Jiji la Dar
es Salaam, Didas Masaburi na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Adam
Kimbisa.
Imeandaliwa na Fidelis Butahe, Raymond Kaminyoge na Susan Mwillo-Mwananchi