MKUU WA WILAYA YA SHINYANGA AWATAKA WATUMISHI WA SERIKALI KUTOCHANGANYA SIASA SUALA LA UJENZI WA MAABARA

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro
Mkuu mpya wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro amewataka watumishi wa serikali kutojiingiza katika mambo ya siasa badala yake wasimamie shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa maabara.

Matiro ameyasema hayo juzi wakati akijitambulisha katika kikao cha baraza maalum la madiwani wa manispaa ya Shinyanga kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga wakati akihamasisha madiwani na watendaji wa serikali kusimamia ipasavyo suala la ujenzi wa maabara katika shule za sekondari.

Matiro amesema watendaji wanapaswa kujiweka pembeni na mambo ya siasa na badala  yake wawaachie wanasiasa ili kufanikisha shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa maabara kwani kuna baadhi ya wanasiasa wanawashawishi wananchi wasichangie ujenzi huo.

Amewataka watendaji wa serikali kutojiingiza  katika siasa,na kwamba watachukua hatua kali kwa watu wote watakaokwamisha ujenzi wa maabara.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya amewataka viongozi wa serikali na vyamavya siasa kuhamasisha wananchi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili muda utakapofika waipigie kura ya ndiyo katika inayopendekezwa na kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao.

Naye mstahiki meya wa manispaa ya Shinyanga Gulam Hafidh Mukadam aliyekuwa mwenyekiti wa kikao hicho ametumia fursa hiyo kumkaribisha mkuu huyo mpya wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro aliyetokea wilaya ya Makete kuchukua nafasi ya Annarose Nyamubi aliyehamishiwa katika wilaya ya Butiama mkoani Mara.

Mukadam amesema ujenzi wa maabara katika manispaa hiyo umefikia pazuri na kwamba hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu ujenzi utakuwa umekamilika huku akiahidi yeye na madiwani wa manispaa hiyo kushiriki kikamilifu katika kufaninisha ujenzi wa maabara na shughuli mbalimbali za maendeleo.
Na Kadama Malunde-Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post