KATIKA hali isiyo ya kawaida mtu asiyefahamika anayesadikika kuwa ni mchawi, amemkata kidole cha mkono wa kushoto mtoto wa miaka sita Chrispin Leonard Nkana (pichani) ambaye siyo Albino na kutokomea nacho kusikojulikana.
Tukio hilo lilitokea Machi 17, mwaka huu katika Mtaa wa Mtakuja eneo la Majengo Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa.
Akizungumza na mwandishi wetu aliyefika nyumbani kwa mtoto aliyekatwa kidole, mama wa mtoto huyo, Lucy Savery (26) ambaye ni mjane amesema Machi 17, mwaka huu saa sita mchana alikuwa kazini kwake katika hoteli moja mjini Sumbawanga alipigiwa simu na majirani kuwa mwanaye alikatwa kidole na mtu asiyefahamika na kuondoka nacho.
“Niliacha kazi na kukimbilia nyumbani, nilipofika nilimkuta Chrispin akilia sana akiwa amepakatwa na jirani zangu.
Tulipomuuliza nani amemkata kidole alisema kuwa ni baba mmoja aliyefika akamkamata na kuingia naye kwenye shamba la mahindi, akamtumbukiza nguo kinywani, akatoa mkasi mkubwa mfukoni na kumkata kidole kisha akakimbianacho kusikojulikana,” alisema.
Mama huyo aliongeza kwamba waliamua kumkimbiza Hospitali ya Kristo Mfalme, Sumbawanga wakaelekezwa wafike kituo cha polisi kwanza wapewe fomu namba tatu (PF3) ndipo mtoto apate matibabu maelekezo ambayo waliyatekeleza na mtoto akatibiwa.
Mtoto Chrispin alipohojiwa alisema kuwa mtu huyo alikuwa amevaa suruali nyeusi na shati jeupe na kuwa aliwahi kumuona mara moja kwenye mashine siku za nyuma.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, ACP Jacob Mwaruanda alipoulizwa juu ya tukio hilo alikiri kutokea.
“Tukio hilo lipo na linashughulikiwa na ofisi ya upelelezi ya mkoa kwangu bado halijafika na wakikamilisha upelelezi wataniletea nami nitawapa taarifa tutakachokuwa tumebaini,” alisema Kamanda Mwaruanda.
Na Willy Sumia-Sumbawanga
Social Plugin