MUME NA MKE WALIOMWOZESHA BINTI YAO WA MIAKA 1O KWA MBUZI 12 WAFIKISHWA MAHAKAMANI


Mke na Mume wanaotuhumiwa kumuoza binti wa miaka 10 jana walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma Mjini huku Mahakama ikifunga dhamana yao hadi kesi hiyo itakapomalizika.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la kumuozesha mtoto mwenye umri wa miaka 10 ambaye ni binti yao kwa mahari ya Sh 100,000 na mbuzi 12.
 
Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Dodoma Mjini , Mwajuma Lukindo Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Lina Magoma, alidai washtakiwa Stephano Nyambuya (65) na mkewe Juliana Gidion (30) ambao ni wakazi wa kijiji cha Lionii wilayani Bahi mkoani Dodoma walitenda kosa la kumuozesha mtoto aliye chini ya miaka 15.
 
Mwendesha mashitaka huyo alisema watuhumiwa hao walitenda kosa hilo kinyume cha  kifungu cha sheria namba 138  (2) cha kanuni ya adhabu kilichofanyiwa marejeo mwaka 2002.
 
Magoma alisema wazazi na walezi hao waliamua kumuozesha mtoto aliye chini ya umri huo kwa Joshua Mnamba mwenye umri wa miaka (25), ambapo wote kwa pamoja walikana shitaka lao.
 
Hakimu  Mkazi Lukindo alisema washitakiwa hao wanatakiwa kuwa rumande kutokana na kosa walilotenda kutokuwa na dhamana.

Alisema sheria ya makosa ya jinai inazuia dhamana kwa watu wenye makosa kama hayo, hivyo washitawa watabaki rumande mpaka kesi yao itakapokwisha.
 
Mnamba ambaye alimuoa binti huyo alifikishwa mahakamani hapo Februari 24, mwaka huu na yuko rumande. Kesi hiyo imepangwa kutajwa tena Machi 16, mwaka huu.
 
Mshtakiwa huyo alishtakiwa kwa kosa la kubaka. Kwa sasa mtoto huyo aliyeozwa amepata hifadhi kwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Betty Mkwasa.

Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kulifuatiwa taarifa zilizotolewa na majirani kwa Serikali ya Kijiji na hatimaye Polisi na watuhumiwa kufanikiwa kukamatwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post