Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Cecilia Mosha (26) aliyejirusha kutoka ghorofa ya tatu hadi chini kutokana na hofu ya moto uliotokea katika Hosteli ya Mabibo, amevunjika mfupa wa bega.
Mwanafunzi
huyo alijirusha kupitia dirishani juzi katika harakati za kujiokoa na
moto baada ya jengo la wasichana, Block A kushika moto huku wanafunzi
wakiwa vyumbani wakiendelea na shughuli zao.
Cecilia
ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Shahada ya Uhandisi wa
Uchimbaji Madini, amesema alisikia kelele akiwa chumbani na alipotoka
nje akakuta moshi umetanda kila kona.
“Baada ya kuona hivyo niliona ni vema nijiokoe kwa kujirusha kutoka ghorofa ya tatu ya bweni hilo hadi chini kupitia dirishani,”alisema Mosha.
Amesema
baada ya kuruka hadi chini alikimbizwa katika kituo kidogo cha afya
karibu na hosteli hiyo ambako alipoteza fahamu na kushtukia yupo katika
Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI).
Naye Meneja Ustawi na Uhusiano wa Taasisi ya MOI, Almasi Jumaa alisema hali ya Cecilia si mbaya na anaendelea na matibabu.
“Tumempokea
huyo mgonjwa jana na baada ya timu ya madaktari kumfanyia vipimo vya
kutosha wamebaini amevunjika mfupa wa bega la kulia na kupata mshtuko wa
mwili … alipata maumivu ya kiuno na mwili kwa ujumla,” alisema Jumaa.
Ajali hiyo ya moto ilitokea juzi katika Hosteli ya Mabibo iliyopo Mtaa wa Ubungo Kibangu, Dar es Salaam.
Kwa
mujibu wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza
Mukandala moto huo uliteketeza ghorofa ya tatu ya jengo A linalotumiwa
na wanafunzi wa kike.
Alisema moto huo haukuwa na madhara kwa binadamu ingawa uliteketeza mali za wanafunzi.
Profesa Mukandali aliahidi uongozi wa chuo utahakikisha wanafunzi hao wanapata msaada wa hali na mali.