POLISI WAMSHUSHIA KICHAPO KATIBU MWENEZI WA CCM MKOA ALIYEWAPIGA VICHWA NA NGUMI ASKARI POLISI!!

Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Simiyu ambaye amepata kipigo kitakatifu kutoka kwa askari polisi Wilayani Meatu Mkoani Simiyu, baada ya kukaidi amri ya askari hao kwa madai kuwa ni kiongozi wa chama kinachoongoza serikali.


KATIBU Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)mkoa wa Simiyu,Jeremiah Shigala amepigwa na askari wa jeshi la polisi wilayani Meatu mkoani Simiyu na kisha kuwekwa mahabusu kwa masaa kadhaa kwa madai ya kuwazuia kufanya kazi.

Tukio hilo lililotokea juzi mjini Mwanhuzi majira ya saa 2.30 usiku wakati askari hao wakitekeleza majukumu ya kufanya doria ya usiku mjini humo ili kuthibiti watu wenye nia ya kutenda uhalifu.

Baadhi ya mashuhuda  walioshuhudia tukio hilo waliwaeleza waandishi wa habari kuwa askari hao wakiwa sita walilikamata trekta lililokuwa  ikiendeshwa na kijana ( jina halikuweza kupatikana mara moja) mmoja bila kuwasha taa na hivyo kukiuka sheria za barabarani.

Mashuhuda hao walieleza kuwa wakati askari hao wakiendelea kumhoji kijana huyo ghafla alifika Kiongozi huyo wa CCM na kuanza kuwazuia askari kumhoji kijana huyo kwa madai kuwa anamfahamu.

“Baada ya kuwazuia wasimhoji askari walikataa akaanza kutumia lugha ya matusi  na kuwataka askari hao wasitishe mara moja mahojiano hayo hadi hapo atakapowasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo”, Walieleza mashuhuda hao

Walibainisha kuwa askari hao hawakukubaliana na matakwa ya kiongozi huyo, ndipo ghafla Katibu huyo wa CCM alipomvamia na kumpiga kichwani Askari polisi wa Usalama Barabarani Koplo Kulwa na kuanguka chini.

“Huyu Kiongozi wa CCM alimrukia mmoja wa askari hao na kumpiga kichwa hadi  kuanguka hali iliyosababisha kuanguka chini, hapo ndipo vurugu zikaanza kati ya kiongozi huyo na askari 6 ”,alisema Gwisu Masanja.

Askari hao mara baada ya kuona mwenzao amepigwa walimweka chini ya ulinzi katibu mwenezi huyo lakini alikaidi amri hiyo  na kuanza kujihami kwa kuwarushia ngumi askari.

Walieleza kuwa mara baada ya kuwepo kwa hali hiyo askari nao kwa kujihami  walianza kumshambulia kwa kumpa kipigo kwa kutumia vitako vya bunduki,virungu na mikanda hadi kumchania nguo zake na kubaki na nguo
za ndani tu na kisha kuwekwa mahabusu.

Kamanda wa polisi mkoani Simiyu,Naibu Kamishina Charles Mkumbo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akiwaonya viongozi wanaotumia nyadhifa zao kuingilia kazi zinazofanywa na jeshi hilo kuacha mara moja vitendo hivyo na hayuko tayari kuvumilia.
Alipotafutwa kwa njia ya simu Kiongozi huyo kuongelea juu ya sakata hilo, alisema kuwa hayuko tayari kuliongelea kutokana na kuwa katika sehemu isiyo sahihi na kuhaidi kuliongelea baadaye atakapopata muda.

Via>>Simiyunews blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post