Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RADI YAUA WATU WATANO SHINYANGA, WAMO WANAFUNZI WANNE


 
WATU watano wa familia moja wakiwemo wanafunzi wanne wamekufa papo hapo kwa kupigwa radi wakiwa shambani katika Kijiji cha Manungu kata ya Uyogo, Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.

 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kahama, Leonard Nyadaho, kwa niaba ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, watu hao walipigwa na radi Februari 28, mwaka huu na kufariki papo hapo kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha.
 
Nyadaho alisema mvua hiyo iliyoanza kunyesha juzi jioni katika kijiji cha Manungu kitongoji cha Izengwe. Alisema mvua hiyo iliwakuta wananchi hao wakiwa mbugani wakipanda mpunga ndipo walipopigwa na radi na kufariki.
 
Aliwataja marehemu hao kuwa ni Paulina Williamu (28), Magreth Mayunga (13), Herena Mayunga (14), Flora Mathias (13) na Veronica Mathias (14), wote wanafunzi wa Shule ya Msingi Manungu.
 
Mashuhuda walisema marehemu hao waliamka asubuhi na kwenda shambani kupanda mpunga, wakiwa huko ghafla lilitanda wingu zito ndipo mvua iliyoambatana na radi ilipoanza kunyesha.
 
Walisema mvua hiyo kubwa iliyokuwa imeambatana na upepo mkali ilikuwa na muungurumo wa radi wa mara kwa mara. Walisema ilinyesha muda mfupi na ilipokatika walisikia mayowe yakitokea walipokuwa watu hao.
 
"Baada ya kwenda shambani tulikuta wote hao wameshafariki," alisema mmoja wa mashuhuda hao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com