Marehemu
Kapteni Komba.
Picha
ya kwanza ya Marehemu komba mara baada ya kufariki dunia.
...Komba
enzi za uhai wake.
MBUNGE wa
Mbinga Magharibi, Kapten John Komba amefariki dunia Februari 28,2015 jijini Dar
es Salaam.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amethibitisha kutokea kwa kifo hicho, hata hivyo hakuwa tayari kuelezea kwa undani kwa madai kuwa taarifa hizo zimemfikia sasa hivi.
Mmoja wa
watoto wa Komba ambaye aliyejitambulisha kwa jina la Herman amethibitisha
kutokea kwa msiba huo na akasema, huku akilia, msiba wa baba yake upo nyumbani
kwake Mbezi Tangi Bovu, Dar.
Habari
zinasema asubuhi ya siku ya Jumamosi Komba alikwenda kwenye shughuli zake za
kikazi kama kawaida lakini baadaye akajisikia vibaya, hivyo akaamua kurudi
nyumbani ambako alizidiwa ndipo familia yake ilipoamua kumkimbiza Hospitali ya
TMJ lakini alipopimwa na madaktari ikathibitika kuwa alikuwa tayari ameaga
dunia.
habari
zaidi zinasema kuwa hivi sasa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali
ya Jeshi ya Lugalo.
Kapteni Komba
ambaye pia ni Mkurugugenzi wa Kikundi cha Maigizo cha Tanzania One Theatre
(TOT), ambacho kina kikundi cha taarabu na bendi inayokwenda na
mtindo wa Achimenengule, amekuwa akikisaidia sana chama chake, Chama Cha
Mapinduzi (CCM) katika kampeni zake wakati wa uchaguzi kwa kutunga nyimbo za
kuhamasisha wapiga kura na kushiriki kupiga live kwenye majukwaa ya kisiasa.
...alipokuwa
bungeni
Enzi za uhai
wake alitamani sana na kufanya juhudi kubwa ili mtindo wa Achimenengule
uwe wa kitaifa lakini ikashindikana, na badala yake Watanzania sasa tuna
muziki wa Mduara ambao umekuwa kama mtindo wa muziki wetu kwa sababu zifuatazo.
Kwanza, ni
mtindo halisi wa Kitanzania uliochipuka kutoka mahadhi ya kimwambao ya
Tanzania. Pili, ndiyo mtindo pekee uliowahi kutumiwa na bendi nyingi baada ya
kuasisiwa na ‘mabingwa’ wa muziki wetu, wana Njenje, The Kilimanjaro Band.
Baada ya
bendi hiyo kuuasisi, mtindo huo, tayari umepigwa na bendi kama TOT Plus, Chuchu
Sound, Pamo Sound, Inafrika Band, wana mipasho kadhaa na mwanamuziki mahiri
lakini asiyethamini kiwango chake kikubwa cha muziki, Bob Haisa.
Sababu ya
tatu ni kwamba mtindo huo umekuwa wa kupigwa na bendi nyingi, vikundi vingi na
wanamuziki wengi si kwa kulazimisha bali kwa mapenzi tu ya mashabiki wa muziki
wa Tanzania.
Kapteni Komba
awali alikuwa mwalimu wa shule ya msingi kabla ya kuingia jeshini na kuwa
kiongozi wa kikundi cha maonesho cha jeshi na baadaye Rais Mstaafu Ali Hassan
Mwinyi akamshawishi aachane na jeshi na kujiunga na CCM wakati wa mfumo wa
vyama mingi ulipoingizwa mwaka 1992.
“Mzee Mwinyi
ndiye aliyenifanya niache jeshi wakati huo nikiwa na cheo cha ukapteni.
Aliniomba nikisaidie chama kwa kuanzisha kikundi ambacho lengo lake lilikuwa
kukipigia debe CCM,” aliwahi kusema hivyo Kapteni Komba.
Ameshiriki
kampenzi za marais Ally Hassan Mwinyi, Benjamin William Mkapa na aliye
madarakani hivi sasa, Jakaya Mrisho Kikwete. Alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu
ya CCM Taifa na Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi hadi kifo kinamchukua.
Licha ya
siasa Kapteni Komba alikuwa anamiliki shule na pia alikuwa na biashara kadhaa.
Mwaka 2012 Komba aliwahi kupelekwa India kwa matibabu ambapo alifanyiwa upasuaji wa nyonga baada ya kupata ugonjwa uliosababisha mifupa kusagana sehemu hiyo ya nyonga.
Baada ya
kurejea nchini alisema upasuaji huo ulichukua saa tano na ulifanyika katika
Hospitali ya Apollo, India na alikanusha kuwa alikuwa na ugonjwa wa
figo.
Ugonjwa uliomuua ni shinikizo la damu ambalo lilikuwa likimsumbua kwa muda
mrefu.
..marehemu Komba akiongea na wanahabari nyumbani
kwake Mbezi tangi Bovu akielezea kuimarika kwa afya yake aliporejea kutoka
India kwenye matibabu, Julai 27, 2012.
MALI ZAKE
ZATISHIWA KUUZWA
Mapema mwezi
uliyopita mwaka huu, mali za Kapteni John Komba zilitangazwa kupigwa mnada
kutokana na kushindwa kulipa deni analodaiwa na Benki ya CRDB.
Mali hizo
zilihusisha eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 2,214 lililopo Mbezi Tangi Bovu,
Dar es Salaam, kiwanja namba 1030 kilichosajiliwa kwa jina la John Damiano
Komba na Salome Komba.
Kwa mujibu wa
tangazo lililotolewa kwenye vyombo vya habari, Kampuni ya Uwakili ya Mpoki
& Associates Advocates inayoiwakilisha CRDB ilitangaza kuuza eneo hilo la
kibiashara lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya mafuta, maduka
makubwa, benki, sehemu ya kufanyia mazoezi, hospitali na huduma nyingine za
kijamii.
Marehemu
Komba ameacha mjane, Bi Salome, ambaye ni mwalimu kitaalumu na watoto kadhaa.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi- ameen!
(Stori:
Gladness Mallya/ GPL)
Social Plugin