TAMKO LA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA KUHUSU KATIBA INAYOPENDEKEZWA, MAHAKAMA YA KADHI NA HALI YA USALAMA NA AMANI YA NCHI.
Sunday, March 15, 2015
HILI NDIO TAMKO LA WAAMINI WA DINI YA KIKRISTO LILOSOMWA LEO KILA KANISA NCHINI
TAMKO LA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA KUHUSU KATIBA INAYOPENDEKEZWA
JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA TAMKO LA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA KUHUSU KATIBA INAYOPENDEKEZWA, MAHAKAMA YA KADHI NA HALI YA USALAMA NA AMANI YA NCHI.
SISI Maaskofu wa Jukwaa la Wakristo Tanzania linaloundwa na Taasisi
za Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Kikristo
Tanzania (CCT) na Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT),
tuliokutana leo tarehe 10 Machi 2015, tumepata nafasi ya kujadili kwa
kina kuhusu hali ya usalama wa nchi ilivyo sasa na mustakabali wake,
Katiba Inayopendekezwa na uanzishaji wa Mahakama ya Kadhi.
Baada ya kutafakari yote hayo, Jukwaa limefikia maazimio yafuatayo: 1.
Kuhusu uanzishaji wa Mahakama ya Kadhi: Suala la uanzishwaji wa
Mahakama ya Kadhi nchini kama tulivyotoa maoni yetu kwa Kamati ya Bunge
ya Katiba na Sheria (Januari 16, 2015); barua yetu kwa Waziri Mkuu na
matamko mbalimbali yaliyokwisha kutolewa kuhusu jambo hili; Mahakama ya
Kadhi inakiuka misingi ya Taifa hili kuwa na Serikali isiyokuwa na dini
wala mfumo wa sheria unaobagua raia wake kwa misingi ya dini.
Pia
mjadala unaoendelea unavunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ya 1977 Ibara ya 19. Kwa kuendelea kujadili suala hili katika Ilani za
Vyama vya Siasa, Majukwaa ya Kisiasa na Bungeni, limeligawa Taifa letu,
Serikali, Bunge, Mahakama na wananchi.
Mahakama ya Kadhi imekuwa
likiendelea kutumiwa na wanasiasa kama mtaji wao wa kujipatia madaraka
kwa gharama za kuleta chuki za kidini. Kwa dhamiri safi, Jukwaa
linatamka wazi kuwa mjadala unaoendelea kati ya Serikali na vikundi vya
kidini kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi kikatiba na kisheria
ufungwe na badala yake ziachiwe taasisi husika za kidini kuamua juu ya
masuala hayo bila kuihusisha serikali wala waumini wa dini nyingine.
2.
Kuhusu Katiba inayopendekezwa: Katiba Inayopendekezwa imeleta
mgawanyiko mkubwa katika Taifa kwani imepatikana kwa njia zisizo za
kiadilifu; na mchakato wake umeendeshwa kwa hila na ubabe. Aidha, Katiba
Inayopendekezwa haijajibu bado matakwa na malalamiko ya wananchi kwenye
masuala mbalimbali (Muundo wa serikali, miiko na maadili ya viongozi wa
umma, haki za binadamu, madaraka ya Rais, uwiano wa mihimili ya dola
n.k).
Ikumbukwe Katiba Inayopendekezwa ilipitishwa kwenye Bunge
Maalum la Katiba kwa ahadi ya Serikali kuipa dini ya Kiislam Mahakama ya
Kadhi. Inashangaza kuwa hata Serikali inatoa rushwa ili kufikia malengo
yake!!! Kwa hali kama hii, Kanisa haliwezi kuunga mkono kupitishwa kwa
Katiba Inayopendekezwa.
Hivyo basi, Jukwaa linawataka waumini
wake wote wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura, waisome Katiba Inayopendekezwa na kushiriki kikamilifu
vipindi vya elimu juu ya Katiba Inayopendekezwa na kisha wajitokeze kwa
wingi kupiga kura ya HAPANA kwa Katiba Inayopendekezwa kwa sababu
zilizotajwa hapo juu.
3. Hali ya usalama wa nchi ulivyo sasa:
Jukwaa linasikitishwa na viashiria pevu vya ugaidi vilivyoanza
kujitokeza nchini kwa takribani miaka mitano iliyopita. Kumekuwa na
vitendo vinavyoashiria kuchipuka kwa ugaidi kama vile uvamizi wa vituo
vya polisi, kuporwa silaha na mauaji ya polisi, mafunzo ya kareti katika
nyumba za Ibada, mafunzo ya itikadi kali za kidini kwa watoto
(Kilimanjaro), tukio la Amboni Tanga, mauaji ya viongozi wa dini
(Buselesele, Zanzibar, Arusha), uchomaji wa nyumba za Ibada na kumwagiwa
tindikali kwa viongozi wa dini. 4. Mauaji ya watu wenye ulemavu wa
ngozi (maalbino): Jukwaa linasikitishwa na mwendelezo wa mauaji ya watu
wenye ulemavu wa ngozi (maalbino) na ukatili unaosababisha ulemavu wa
kudumu wa maalbino katika nchi yetu. Hali hii inatishia utulivu, amani
na umoja wa kitaifa tuliokuwa nao kama taifa la mfano barani Afrika.
Jukwaa
linawaasa wananchi kuacha tabia hii ya kuua albino. Jukwaa linaamini
kuwa kukosekana kwa uwajibikaji wa viongozi wa serikali na kuongezeka
kwa wigo wa kipato kati ya walionacho na wasionacho kunachangia ongezeko
la vitendo hivyo viovu. Jukwaa linajiuliza: mbona tembo na ng’ombe
wakiuawa operesheni maalum zinafanyika na viongozi wanawajibika, kwa
nini maalbino wakiuawa viongozi hawawajibiki?
Kutokana na hayo
yote, Jukwaa linatilia shaka dhamira thabiti ya uongozi wa Chama Tawala
na Serikali yake katika kuvitokomeza vitendo vya kigaidi, mauaji ya
albino na uvunjifu wa amani unaoendelea hasa kutokana mikakati hafifu na
udhaifu mkubwa uliojitokeza wakati wa kuyashughulikia masuala hayo.
Kwa
kuwa Chama Tawala na Serikali wameshindwa kusimamia misingi iliyolea
taifa kama serikali isiyo ya kidini na taifa lenye amani; umoja na
utulivu; Jukwaa linawaelekeza waumini wote na wenye mapenzi mema wakati
wa uchaguzi mkuu ujao kufanya maamuzi yanayolitanguliza Taifa badala ya
kutanguliza mazoea, mapokeo, itikadi na ushabiki wa chama fulani cha
siasa.
YATOSHA KWA SIKU MAOVU YAKE: MATHAYO 6:34
Imetolewa na:
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin