Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIKONGWE WATATU WAUAWA KIKATILI WAKIDAIWA KUZUIA MVUA HUKO DODOMA,MWINGINE ATOBOLEWA MACHO!!

 

Watu watatu wameuawa Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma katika matukio mawili tofauti yanayohusisha imani za kishirikina.

Akizungumzia matukio Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi DAVID MISIME – SACP amesema tukio la kwanza limetokea tarehe 01/03/2015 majira ya saa 01:00hrs katika kitongoji cha Golani, kijiji cha Masinyeti, kata ya Iduo, tarafa ya Mlali Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma ambapo mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la SAIDIA S/O CHAKUTWANGA mwenye miaka 80, kabila Mkaguru, Mkulima Mganga wa kienyeji aliuawa na watu waliojichukulia sheria mkononi kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na kutobolewa macho.

Kamanda MISIME amesema uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo cha mauaji hayo ni imani za kishirikina wakimtuhumu marehemu kuwa anazuia mvua kunyesha katika eneo hilo.

Pia Kamanda MISIME amesema katika tukio lingine limetokea tarehe 01/03/2015 majira ya saa 02:00hrs katika kitongoji cha Majengo, kijiji cha Ihanda, Kata na Tarafa ya Mlali Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma ambapo mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la PETER S/O KALULI mwenye miaka 85, kabila Mkaguru akiwa na mkewe aitwaye KAILA W/O KALULI mwenye miaka 80, Mkaguru wote wakulima na wakazi wa Kitongoji cha Majengo wakiwa wamelala ndani ya nyumba yao ya tembe, waliuawa na watu wasiofahamika kwa kuangushiwa ukuta wa nyumba yao kisha kuchoma moto na kubomoa nyumba mbili za tembe.

Watu hao walifanya uharibifu mwingine kwa kuwaua nguruwe mmoja na ng’ombe mmoja kumkata miguu.

Aidha Kamanda MISIME amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha mauaji na uharibifu huo ni imani za kishirikina wakiwatuhumu marehemu kuwa wanazuia mvua kunyesha. 

Watuhumiwa wanne akiwemo M/Kiti wa Kijiji cha Ihanda na wazee wawili wa kimila wa kijiji wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kuhusiana na tukio hili kwani taarifa zinaonyesha waliandaa vikao vya kutekeleza mauaji haya. 

Upelelezi wa matukio yote mawili unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwatafuta watuhumiwa wengine waliohusika na matukio haya.

Kamanda MISIME ametoa wito kwa wananchi kutochukua sheria mkononi  na kujiepusha na imani za  kishirikina zinazopelekea kuleta hofu na mashaka kwa jamii. Alisema ni jambo la aibu kwa jamii hadi karne hii watu kuamini kuwa kuna watu wanaoweza kuzuia mvua isinyeshe. 

Pia amewataka viongozi wa maeneo mbalimbali kutoa taarifa mapema polisi pale wanapoona mipango ya kihalifu kama hiyo ikipangwa.

 Na Sylvester Onesmo/Dorice Kigombe wa Jeshi la Polisi Dodoma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com