WAENDESHA BODABODA NAO WAANDAMANA KWA LOWASSA,KAULI YA NAPE YAMCHEFUA LOWASSA

Waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda zaidi ya 60 na wananchi wa kawaida wamefunga safari kutoka wilayani Mbarali mkoa wa Mbeya mpaka mjini Dodoma kumshawishi Edward Lowassa agombee urais

 
Siku moja baada katibu wa itikadi na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Nape Nnauye kutoa kauli ya chama hicho kuhusu makundi yanayojitokeza kumshawishi waziri mkuu mstaafu Mhe Edward Lowassa kugombea urais, kuwa yanaweza kumkosesha sifa kiongozi huyo ya kuwania nafasi hiyo,  Lowassa amejibu kauli hiyo na kudai anashangazwa nayo huku akihoji imetokana na maamuzi ya kikao gani ndani ya CCM.

Lowassa anatoa kauli hiyo katika muendelezo wa kupokea makundi mbalimbali ya jamii kumshawishi kuwania nafasi urais ambapo safari hii (leo) waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda zaidi ya 60 na wananchi wa kawaida wamefunga safari kutoka wilayani Mbarali mkoa wa Mbeya mpaka mjini Dodoma, kumshawishi agombee.

Lowassa amesema kauli ya Nape Nnauye inamshangaza kwani Chama Cha Mapinduzi kina utaratibu wake wa kujadili mambo kama hayo kupitia vikao mbalimbali.
Lowassa pia amewataka wanaoendelea kumnyooshea vidole kuhusu hatua ya wananchi wenye imani naye kujitokeza kumshawishi awanie nafasi hiyo wasubiri ufike wakati muafaka, ili wana-CCM na wananchi waweze kutoa maamuzi yao.

Lowassa amesisitiza watu hasa vijana kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ili wapate haki yao ya kikatiba ya kuchagua kiongozi wanayemuhitaji.
Awali kundi hilo la vijana na bodaboda waliosafiri umbali wa kilometa zaidi ya 600 wakiongozwa na kamanda wa UV-CCM wilaya Mbarali Ibrahim Ismail wamesema lengo la safari yao hiyo ni kuungana na watanzania wengine kumtia moyo Lowassa ashawishike kuwania urais kwani wana imani kubwa naye.

Wamedai kuwa pamoja na mambo mengine kama alivyoweza kujenga shule za kata nchi nzima pia ataweza kutegua bomu la tatizo la ajira hasa kwa vijana.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post