KESI za kulawiti watoto mashuleni imeelezwa kuwa wanaofanya ukatili
huo wa kijinsia kwa watoto hao baadhi yao ni walimu wanaowafundisha na
kwamba kutokana na walimu hao kuhitajika shuleni hapo baadhi ya uongozi
wa shule umekuwa ukishindwa kuwachukulia hatua ikiwa ni pamoja na
kushindwa kuripoti katika dawati hilo.
Mkaguzi Msaidizi wa Polisi ambaye pia ni Mkuu wa Dawati la Jinsia
mkoani Kilimanjaro Prisca Maganga aliwaambia waandishi wa habari wa mikoa ya
Manyara, Tanga, Kilimanjaro na Arusha waliotembelea dawati hilo mwishoni
mwa wiki kuwa kwa mwezi Januari hadi Februari mwaka huu wamepokea kesi
10 za kutelekeza familia zikiwemo kesi 2 za kubaka.
Alisema kesi mbili hadi tatu za kulawiti wanafunzi wa shule za msingi
mkoani Kilimanjaro zimeripotiwa kwa mwezi Januari hadi Februari mwaka
huu katika dawati la jinsia mkoani humo ambapo katika kesi 10
zilizoripotiwa katika dawati hilo zilikuwa zikiongozwa na kesi za
kutelekeza familia.
“Kesi za ukatili wa majumbani kama kutelekeza familia zinaongoza kwa
mkoa wetu, tunapokea kesi 10 hadi 15 kwa mwezi chimbuko likiwa ni
kiuchumi na changamoto za maisha na akinamama wengi wanatelekezwa kwa
sababu ya utegemezi na sababu nyingine wanaume kuwa na tamaa na kuoa mke
mwingine,” Alisema mkaguzi huyo wa Polisi.
Akielezea ukatili mwingine wa majumbani, alisema wazazi wengi
wamekuwa wakitoa adhabu za viboko na vipigo vinavyokithiri kwa watoto
wao kwa lengo la kuwakanya kitabia bila kujua kwamba zipo sheria
zinazomlinda mtoto huyo dhidi ya ukatili huo na wakati mwingine wazazi
hao kulazimika kufikishwa katika vyombo vya sheria.
“Baba mmoja alikuwa akimpiga mtoto wake kwa mjeledi na kuacha alama
mbaya mwilini mara kwa mara na kuathiri masomo na makuzi yake na kumpiga
mama wa mtoto huyo kumbe wazazi hao ni waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi,
tunashukuru walimu wa shule aliyokuwa akisoma mtoto huyo kutupa taarifa
na ushirikiano hadi mtoto huyo kuendelea na masomo yake mpaka sasa,”
alisema.
Social Plugin