Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Taarifa zaidi!! MVUA YA MAWE HUKO KAHAMA VIFO SASA NI 41 ,MAJERUHI 91

Idadi ya watu waliofariki kutokana na mvua huko Kahama imefikia watu  42 wengi wakiwa ni watoto huku majeruhi waliofikishwa hospitali wakiwa ni 91.



Watu 35 walifariki dunia papo hapo na wengine  wakiwa hospitali ya wilaya ya Kahama kutokana na mvua kubwa iliyoambatana na upepo na mawe yanayodaiwa kuwa na ukubwa mithili ya ndoo ndogo ya lita kumi katika kijiji na Kata ya Mwakata wilayani Kahama mkoani Shinyanga usiku wa kuamkia leo.

Malunde1 blog imeambiwa kuwa mvua hiyo imenyesha kwa muda wa takribani dakika 30,imeua pia mifugo wakiwemo ng’ombe na mbuzi na kuharibu vibaya mimea.

Afisa mtendaji wa kata ya Mwakata Mahega Mwelemi ameiambia Malunde1 blog kuwa maeneo yaliyoathirika kuwa ni cha Mwakata,Nhumbi na Magung’humwa.

Mwelemi amesema watu wengi wamefariki kwa kuangukiwa na nyumba zao,kuzidiwa na maji pamoja kupigwa mawe ya mvua ambayo hadi leo asubuhi yalikuwa yanaonekana kijijini hapo.

Mkuu  wa wilaya ya Kahama Benson Mpesya aliyefika eneo la tukio bado wanafanya ukaguzi katika kila kaya kubaini idadi ya watu waliofariki dunia,kujeruhiwa na idadi ya mifugo iliyokufa.

Awali Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha amesema  kuwa idadi ya vifo na majeruhi inaweza kuongezeka.

 Hata hivyo Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Ally Rufunga aliyefika eneo la tukio amesema waliofariki dunia ni hadi sasa ni 41 ,majeruhi 91 na jumla ya watu waliothirika na tukio hilo ni 4,291 kuongeza kuwa kinachohitajika sasa ni misaada mbalimbali ya kibinadamu.



Amesema Mvua hiyo ambayo ilinyesha kwa muda mfupi imewaacha watu 3,500  bila makazi katika kaya 350 huku nyumba zikifurika maji na baadhi ya mifugo ikisombwa.
Amesema mali mbalimbali zimeharibiwa vibaya ikiwemo mifugo kuzolewa na maji na vyakula kwenye eneo lote lililokumbwa na mafuriko hayo.
 
Hali ya majeruhi ambao wamepelekwa katika hospitali mbalimbali bado sio nzuri kwa baadhi ingawa wengine wanaendelea vizuri.

Kamanda wa jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Shinyanga Elisa Mugisha amesema baada ya kupata taarifa kuwepo kwa tukio hilo walifika katika eneo la tukio kwa ajili ya uokoaji

Na Kadama Malunde-Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com