WATU WATANO WA FAMILIA MOJA WAKO HOI BAADA YA KUNYWA DAWA WALIYOPEWA NA MGANGA WA KIENYEJI HUKO MTWARA

WATU watano wa familia moja katika Kitongoji cha Benaco, Kata ya Mtandi Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara, wamelazwa katika Hospitali ya Mkomaindo huku hali zao zikiwa mbaya baada ya kunywa dawa ya kienyeji waliyopewa na mganga wa tiba za asili.

 
Dawa hiyo ya kienyeji inaitwa nyungu, ambayo hutokana na mchanganyiko wa majani tofauti ambayo hupondwa kwenye kinu na kuchanganywa na maji na kuchemshwa.
 
Mgonjwa hufunikwa kwa nguo nyeupe na kufukizwa na mvuke wa maji hayo kisha huyanywa.
 
Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Masasi, Azaria Makubi, alitaja wanafamilia waliolazwa hospitalini ni baba wa familia hiyo Geofrey Evance (43), mke wake, Hadija Salumu (30), dada yake Fidea Evance (40) pamoja na watoto wake wawili, Husna Zuberi (8) na Godfrey Geofrey (10).
 
Imeelezwa baada ya wanafamilia hao kunywa dawa hiyo, wote hali zao zilibadilika ghafla huku baadhi wakitokwa mapovu vinywani na baadae walipoteza fahamu na kukimbizwa katika hospitali ya Mkomaindo ambako wamelazwa hadi sasa.
 
Makubi alithibitisha tukio hilo na kusema ni la juzi saa 12:30 jioni katika eneo la Makondeko, Halmashauri ya mji wa Masasi nyumbani kwa mganga huyo.
 
Alisema wana familia hao walikumbwa na kadhia hiyo baada ya kuitwa na mganga huyo msichana mwenye umri wa miaka 17 (jina tunalihifadhi) kwa lengo la kwenda kumalizia dawa hiyo ya kinga kwa wanafamilia hao kutokana na watoto wao wawili kupewa matibabu na mganga huyo wiki mbili zilizopita.
 
Mkuu wa kituo, alisema kwa mujibu wa maelezo aliyoyatoa mganga, alitoa dawa hiyo kwa wanafamilia hao waitumie kwa kuoga na kupaka kwenye miili yao na si vinginevyo.
 
Alijieleza kwamba, baada ya kuwapa, aliingia ndani ya nyumba yake lakini wanafamilia hao walidanganywa na jirani yao (aliyetajwa jina) kuwa ili kinga hiyo iwe ya kudumu na muda mrefu, ni lazima waoge na wanywe maji yake.
 
Kwa upande wao, wauguzi wa zamu; Prisca Mirumba wa wodi namba moja “B” ya wanaume na Sophia Erasto wa wodi namba sita ya wanawake, walisema waliwapokea wagonjwa hao juzi usiku saa 2:30 wakiwa wamepoteza fahamu huku baadhi yao wakitokwa na mapovu vinywani.
 
Ilielezwa, walibaini watu hao walipewa kimiminika kinachosadikika kuwa ni sumu. Walipewa matibabu ya awali ingawa hadi sasa kwa mujibu wa wauguzi hao, hali za wanafamilia hao si ya kuridhisha.
 
Chanzo cha dawa 
Akizungumza kwa tabu akiwa amelazwa kwenye wodi namba sita Hospitali ya Mkomaindo mjini Masasi, baba wa familia hiyo, Geofrey Evance alisema chanzo cha yeye na familia yake kwenda kwa mganga huyo kupata tiba ni baada ya watoto wake kukumbwa na ugonjwa wa degedege.
 
Alisema baada ya kufika kwa mganga, walipewa dawa hiyo ya nyungu na kisha kushawishiwa na jirani yao wainywe dawa hiyo na kwamba mara baada ya kunywa, walipoteza fahamu na walijikuta wakiwa hospitalini Mkomaindo, mjini Masasi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم