Watu watano wamekufa katika matukio matatu tofauti, wakiwemo watatu waliouawa na miili yao kuchomwa moto na wananchi wanaojiita wenye hasira, baada ya kutuhumiwa kuiba ng’ombe 40 katika Wilaya ya Bunda Mkoani Mara.
Kwa
mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Philipo Kalangi, tukio la
kwanza lilitokea Machi 24 mwaka huu, majira ya saa 3:00 asubuhi katika
kijiji cha Kunanga wilayani Bunda.
Alisema
watu hao watatu waliuawa kwa tuhuma ya kuiba ng’ombe 40, mali ya Julius
Malima (56), mkazi wa kijiji cha Kenkombyo- Neruma kata ya Neruma
wilayani Bunda, baada ya kuvunja zizi na kuanza kuswaga ng’ombe hao,
majira ya saa 10:00 usiku.
Alitaja
waliouawa kuwa ni Mayala Buluma (29) mkazi wa kijiji cha
Jiniva-Kyabakari Wilaya ya Butiama na Mukina Buluma (25), mkazi wa
kijiji cha Namhura wilayani hapa, ambao wote ni watoto wa mzazi mmoja.
Mwingine ni Chacha Masagati (22), mkazi wa kijiji cha Kyabakari Wilaya ya Butiama.