Siri ya mafanikio ya Padri feki, Josephat Asenga, aliyekamatwa mkoani Morogoro, katika kuongoza Misa ya Kanisa Katoliki kwa kufuata taratibu zote maalumu bila kutiliwa shaka, imebainika.
Asenga
aliyetumia vitambulisho feki, alipojitambulisha kwa uongozi wa Kanisa
Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Maria Madeko mkoani Morogoro, alipopewa
fursa ya kuongoza Misa, alitekeleza wajibu huo wa kipadri bila kuacha
shaka.
Akizungumza
na mwandishi, kiongozi mmoja wa Kanisa Katoliki (jina limehifadhiwa),
alithibitisha kuwa Asenga alipofika Parokiani hapo kati ya Mei na Juni
mwaka jana, hakutiliwa shaka hata kidogo kuwa si Padri.
Kwa
mujibu wa kiongozi huyo, Asenga alifika kanisani hapo akiwa amevaa
mavazi ya kipadri na kujitambulisha kuwa yupo nchini kwa mapumziko,
akitokea nchini Marekani, alikodai ndipo anakofanyia shughuli zake za
upadri katika Jimbo Kuu la New York.
Mbali
na kuvalia mavazi ya kipadri, Asenga pia alionesha kitambulisho na
kusababisha uongozi uamini kuwa ni Padri na kumpa makaribisho ya Padri
mwenzao.
“Alipoonesha
kitambulisho tulimwamini na jinsi alivyokuja na mavazi ya upadri na
muonekano wake alionao, haikuwa rahisi kumtilia shaka,”alisema kiongozi huyo.
Baada
ya kupata makaribisho ya kipadri, Asenga kwa mujibu wa kiongozi huyo,
aliomba apangiwe zamu ya kuongoza misa ya Jumapili iliyofuata na
kukubaliwa.
Kiongozi
huyo alithibitisha kuwa Asenga aliongoza vyema misa hiyo, kwa kufuata
taratibu zote za kanisa hilo kama zinavyofuatwa na mapadri wengine.
Kwa
kawaida Misa katika Kanisa la Katoliki, huanzia Sakestia, sehemu
ambayo mapadri na waministranti, ambao ni wasaidizi wao, huvaa majoho na
kusali kabla ya kuingia kanisani wakisindikizwa na nyimbo.
Baada ya kuingia madhabahuni, Padri hubusu madhabahu kabla ya kualika waumini katika Misa.
Mualiko
huo hufuatiwa na maelezo kidogo na kuanza Ibada ya Kitubio, ambayo
waumini hutubu dhambi zao na kujiweka tayari kusikiliza neno la Mungu.
Ibada
ya kusomwa neno, kwa kawaida masomo matatu kutoka vitabu vya Agano la
Kale na Jipya katika kitabu cha Bibilia Takatifu, Padri huanza kutoa
mahubiri.
Mahubiri
yakiisha, Misa huendelea kwa sadaka na baadaye, Padri huongoza waumini
kuanza kukumbuka maelezo ya siku ambayo Yesu Kristo alitoa Sakramenti
katika Chakula cha Mwisho kwa wanafunzi wake akitaka wamkumbuke.
Kwa
kawaida, eneo hilo ndipo Padri kwa mamlaka aliyopewa, hufanya mageuzi
ya sakramenti kuwa Hostia Takatifu, kwa maneno mengine hubariki mkate
kuwa Mwili wa Kristo na divai kuwa Damu ya Kristo.
Kwa
Wakatoliki, eneo la mageuzi ni eneo muhimu na ndio waumini hutuma
maombi kimya kimya, wakiamini ndio Kristo anashuka mwenyewe.
Baada
ya kutumikia Kanisa na kukubalika, Asenga aliaga kuwa anarudi nchini
Marekani kwa kuwa muda wake wa mapumziko, umekwisha na kuagwa na Kanisa.
Wakati
uongozi wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Maria Madeko, ukiwa
na imani kuwa Asenga ni Padri na amerejea New York, kuendelea na Utume,
walipata taarifa za kushangaza kutoka kwa baadhi ya waumini, wakidai
wamekutana na Asenga mitaani.
Mbali
na taarifa hiyo ya kukutwa mitaani na waumini wake, taarifa zaidi
zilieleza kuwa amekuwa akiishi na mwanamke katika eneo la Ujenzi,
kinyume na desturi za mapadri wa Kanisa Katoliki duniani, ambao
hawaruhusiwi kuoa.
Baada
ya taarifa hizo, kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro,
Leonard Paulo, Asenga aliwekewa mtego na Paroko wa Parokia hiyo ya
Mtakatifu Maria Madeko, Malt Dyfrig Joseph.
Paroko
huyo inadaiwa aliwaomba waumini wamshawishi Asenga afike parokiani hapo
na baada ya kufika, alihojiwa na Paroko huyo na kudai kuwa alipata
upadirisho katika Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam.
Kwa
mujibu wa Kamanda huyo, baada ya Paroko huyo kupata maelezo hayo,
alifanya mawasiliano na Katibu wa Jimbo hilo la Dar es Salaam na
kujibiwa kuwa hakuna jina la Padri huyo.
Mtego
wa pili kwa mujibu wa Kamanda Paulo, ulifuata kwa Paroko huyo kutoa
taarifa Polisi kuhusu uwepo wa Padri feki, ambaye aliaminiwa kwa kiwango
cha kuruhusiwa kuongoza Misa.
Taarifa
hizo zinasema Alhamisi ya wiki hii, saa 10:30 jioni, Asenga alimpigia
simu Paroko huyo na kuomba ampangie kazi ya kuendesha Misa Jumapili ya
leo parokiani hapo, na kukubaliwa ambapo Paroko huyo alimtaka afike
kanisani.
Baada ya kufika, taratibu za kujulisha Polisi zilifanywa na askari walipofika kanisani hapo, walimkamata mtuhumiwa huyo.
Kwa
mujibu wa Kamanda Paulo, baada ya kufanya mahojiano na Asenga, alikiri
kuwa yeye si Padri na walipokwenda nyumbani kwake kufanya upekuzi,
walimkuta akiwa na majoho saba ya upadri.
Taarifa
zaidi tulizozipata jana, zilibainisha kuwa Asenga huenda kwa kutumia
mbinu hizo hizo, alishaaminiwa kuongoza Misa katika mkoa wa Kilimanjaro
katika maeneo ya Uru na Moshi na mkoani Singida.
Mbali
na kukubalika katika mikoa hiyo, lakini taarifa zaidi zilibainisha kuwa
Asenga alifanikiwa kote huko kuongoza Misa na kuaminiwa, kutokana na
mafunzo ambayo aliwahi kupata huko nyuma.
Inadaiwa Asenga alianza kupata mafunzo katika Seminari ya Kanisa Katoliki ya Uru, ambako alipata mafunzo ya elimu ya sekondari.
Baada
ya kumaliza kwa mafanikio masomo yake katika seminari hiyo,
alichaguliwa kujiunga na Seminari ya Kibosho, ambayo inatajwa kuwa
maalumu kwa ajili ya kutoa elimu ya falsafa kwa wanafunzi na wengi ni
wanaotarajiwa kuwa mapadri.
Mafanikio
aliyoyapata katika masomo ya falsafa katika Seminari ya Kibosho,
yalimwezesha kujiunga na Seminari ya Kipalapala, ambako inaelezwa ndiko
kunakotolewa mafunzo ya Liturgia, ambayo nayo ni sehemu ya mafunzo
wapewayo wanafunzi wanaotarajiwa kuwa mapadri.
Ingawa
taarifa za mafunzo aliyopata zinatiliwa shaka, lakini namna
alivyoongoza Misa bila kutiliwa shaka, imesababisha baadhi ya waumini
kuanza kumjadili, ili kufahamu hasa nia yake ilikuwa ipi.
Kutokana
na taaluma nyingine aliyonayo ya uhasibu, amesababisha baadhi ya
waumini kuunganisha matukio na uwezo wake na kuamini kuwa huenda hakuwa
akitafuta sadaka.
Mmoja
wa waumini aliyezungumza nasi kwa sharti la kutotajwa jina, alidai kuwa
huenda Asenga alikuwa na njama za kujipatia fedha kwa njia ya
udanganyifu kutoka kwa wafadhili mbalimbali.
Kwa
mujibu wa madai ya muumini huyo, watu wa aina ya Asenga, ambaye ana
taaluma na uwezo wa kipadri, wana njia nyingi za kujipatia kipato, hivyo
inawezekana alidanganya wafadhili wake kuwa yeye ni Padri ili apate
ufadhili huo.
Muumini huyo alikwenda mbali na kudai huenda masharti ya ufadhili huo, ni kupata picha au sauti yake akiongoza Misa kanisani.
“Inawezekana
kuna mahali aliomba ufadhili kwa ajili ya kitu fulani na aliwadanganya
kuwa yeye ni Padri, ndio maana akaamua kuomba zamu ya kuongoza Misa.
“Utapeli umeingia mpaka kwenye nyumba za ibada kweli? Wanadamu tumekosa hofu ya Mungu!” Alihoji muumini huyo na kuasa jamii kuwa macho, kwa kuwa hivi sasa matapeli ni wengi na kila siku wanatoka na mbinu mpya.
Social Plugin