Wanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi Kanawa kijiji cha
Negezi wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga wakiwa wamekaa
chini darasani kutokana na upungufu wa madawati unaoikabili shule hiyo.
*******
Shule
ya msingi Kanawa ilyojengwa mwaka 1952 iliyopo kijiji cha Negezi
kata ya Ukenyenge wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga , inakabiliwa na tatizo la
uhaba wa madawati hali ambayo inawalazimu nusu ya wanafunzi wa shule hiyo,
kusoma wakiwa wamekaa sakafuni ambayo hata hivyo nayo imebomoka na kusababisha
usumbufu kwa walimu na wanafunzi.
Waandishi
wa habari waliotembelea shule hiyo walijionea hali halisi ambapo baadhi ya
madarasa yameota vichuguu ndani na kusababisha nyoka kutoka wakati
wanafunzi wakiwa darasani.
Mwalimu
mkuu msaidizi wa shule hiyo Zacharia Moshi alisema darasa la tano wanafunzi
wote wanakaa chini kwenye sakafu ,huku darasa la sita likiwa na madawati manne pekee
na wanafunzi wengine wanakaa chini kutokana na upungufu huo ambao umekuwa ni
kero kubwa licha ya kwamba shule hiyo ni kongwe ilianzishwa mwaka 1952.
Moshi
alisema madarasa mengine waliacha kuyatumia baada ya kuota vichuguu ndani ili
kuwaepusha wanafunzi kuumwa na nyoka, ambao walikuwa wakati mwingine wakitoka
kwenye mashimo ya vichuguu wakati watoto wakiwa darasani jambo ambalo
linahatarisha maisha yao pamoja na walimu na kupelekea darasa la kwanza na
chekechea kuchanganywa sehemu moja.
“Tunaiomba
serikali kupitia halmashauri yetu na wizara itusaidie kuboresha miundombinu ya
majengo ya shule kwani kwa sasa siyo rafiki kwa watoto hasa wa jinsi ya kike,
hebu fikiria shule ina wanafunzi 357 lakini madawati tunayo 56 tu hii ni kero
kubwa mno kwetu tunafanya kazi katika mazingira magumu sana” alisema mwalimu
Moshi.
Naye
diwani wa kata hiyo Makanasa Masanja alikiri kuwepo changamoto hizo
ambapo alidai wanaendelea kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na viongozi wengine,
huku akibainisha kuwa miaka ya nyuma shule hiyo ilikuwa na madawati ya kutosha
tatizo mengi yameharibika na gharama za kutengeneza ni kubwa hivyo wanajipanga
kuchonga mengine.
Kwa
upande wake mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Kishapu Jane Mutagurwa
alisema wilaya hiyo ina changamoto kubwa katika sekta ya elimu yakiwemo majengo
na madawati , ambapo alikubali kuzitambua changamoto za shule hiyo na
kubainisha kuwa tatizo kubwa ni ufinyu wa bajeti kwani fedha hazitolewi na
serikali katika muda uliopangwa.
Alisema
changamoto ya upungufu wa madawati ni kubwa lakini tatizo lililopo pindi
inapofanyika mikutano au sherehe katika vijiji ,wanayatumia kukalia na
uangalizi unakuwa siyo mzuri hivyo kuwa mwanzo wa kuharibika na kuwataka
viongozi wa maeneo husika kusimamia na kuongeza kuwa mwaka huu wa fedha
walitenga sh 300 milion kununu madawati lakini fedha hazijaja.
Mmoja
wa walimu anayefundisha shule hiyo Mariam Swalehe alisema changamoto
kubwa anayoipata ni wakati wa kukagua madaftari ya wanafunzi pamoja na mwandiko
kuwa mbaya , kwani wanafunzi wengine wanaandika wakiwa wamelalia matumbo
kutokana na darasa la tano kutokuwa na madawati hivyo kukaa chini.
Baadhi
ya wanafunzi Selina Mashishanga na Amina Juma walipohojiwa
waliiomba serikali kuwasaidia kwani wanasoma katika mazingira magumu, ambapo
wakati mwingine wanaamka mgongo unauma kutokana na kujikunja wakati wa kuandika
pamoja na kuumwa mafua na kikohozi mara kwa mara.
Na Kadama Malunde-Shinyanga
|
Social Plugin