Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete
amewataka viongozi wa dini kutoruhusu siasa kufanyika kwenye kwenye nyumba za ibada kwani
kufanya hivyo kutalifanya taifa liingie kwenye machafuko.
Rais Kikwete alitoa rai hiyo jana wakati akitoa salamu zake
wakati wa ibada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa askofu mpya wa kanisa
katoliki jimbo la Shinyanga Liberatus Sangu iliyofanyika katika kanisa kuu la
mama kwenye mwenye Huruma la Ngokolo mjini Shinyanga ikiongozwa na askofu wa
jimbo kuu la Dar es salaam mwadhama Polycarp Kadinali Pengo.
Kikwete alisema katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye
uchaguzi mkuu baadhi ya wanasiasa na washirikika wao wamekuwa wakizunguka
kwenye nyumba za ibada na kuzungumza mambo ya siasa hali inayosababisha kuwagawa waumini
katika makundi ambayo yanaweza kupigana kutokana na tofauti za itikadi ya vyama
vyao vya siasa.
“Viongozi wa dini
kuweni makini,msiwape nafasi watu hawa,msiruhusu wanasiasa kuchukua nafasi
makanisani ili tujenge taifa letu,hakikisheni makanisa yanabaki kuwa sehemu ya
ibada na siyo majukwaa ya siasa”,alisema Kikwete.
“Msiruhusu siasa kuingia kwenye dini na dini kuingizwa
katika siasa,tukifanikiwa hayo tutakuwa tumefanya jambo kubwa,makanisa yabaki
nyumba za ibada siyo majukwaa,viongozi wa dini tusaidiane kwa hili,kwani
wanasiasa wanakimbilia makanisani”,aliongeza Kikwete.
Aliwataka viongozi wa dini kutoruhusu siasa kwenye nyumba za
ibada kwani kufanya hivyo ni hatari kwa amani,utulivu na taifa hivyo kuonya juu
ya siasa kuingia kwenye makanisa.
“Kama tutafika huko kitachotokea ni kwamba wakati wa
kushindwa kwa chama cha siasa ni sawa na kushindwa kwa dini ambayo ilikuwa
inaunga mkono chama hicho na hivyo kusababisha mgogoro kutokea hali ambayo
itasababisha machafuko katika taifa letu”,alisisitiza Kikwete.
“Kiongozi wa siasa akija kwenya kanisa mkaribisheni,akianza
masuala ya siasa ,mwambie hapa siyo mahali pake,hapakuhusu,siyo mahali pako
nenda kwenye majukwaa ya kisiasa mkashindane kwa hoja”,aliongeza Kikwete.
Katika hatua nyingine rais Kikwete aliwataka viongozi wa
dini kuwaelimisha wananchi kutoendekeza imani za kishirikina zinazosababisha
mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi(Albino) na Vikongwe kwani vitendo hivyo
vinachafua sifa ya nchi kimataifa.
Aidha alisema serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za
kidini ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa mahali pa
amani,upendo,mshikamano na utulivu.
Kwa upande wake rais wa baraza la maaskofu kanisa katoliki
Tanzania Tarcius Ngaralekumtwa alimpongeza Askofu Liberatus Sangu kuwa askofu
wa jimbo la Shinyanga baada ya miaka mitatu jimbo kukosa askofu kutokana na
kifo cha askofu wake mhashamu Aloysius
Balina aliyeaga dunia mwaka 2012.
Alisema anaamini askofu Sangu atawatumikia wanaShinyanga kwa
kutokana uzoefu alionao katika kazi za kitume.
Akizungumza baada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa rasmi askofu
Liberatus Sangu aliahidi kushirikiana na
serikali katika kuongoza waumini katika kutenda yaliyo mema mbele za bwana ili
kudumisha amani ya taifa.
Maelfu ya watu walishuhudia tukio hilo muhimu wakiwemo mapadre,watawa,waumini,wabunge,mawaziri,wakuu wa wilaya,wakuu wa mikoa,viongozi wa vyama vya siasa,viongozi wa dini dini mbalimbali na watu mbalimbali wenye mapenzi mema.
Askofu Liberatus Sangu anakuwa askofu wa nne katika jimbo la Shinyanga,wa kwanza alikuwa Askofu Mc Gurkin Eduard kuanzia 3.10.1956 hadi 1975,wa pili ni askofu Castor Sekwa,ambaye ni askofu wa kwanza mzalendo mwaka 1975-1996,wa tatu ni askofu Aloysius Balina kuanzia 16.11.1997 hadi 06.11.2012
Social Plugin