Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MVUA KUBWA YA RADI YAUA WATU 8 HUKO KIGOMA YUMO MWALIMU NA WANAFUNZI 6

 Mwalimu Merina Sekilo aliyenusurika kupigwa na radi wakati akifundisha darasa la kwanza,ambapo wanafunzi 6 walifariki dunia
 Mwalimu Veronika Mtes wa shule ya msingi Kibirizi aliyepata mshtuko baada ya tukio la radi akiwa katika hospitali ya Maweni mkoa wa Kigoma kwa matibabu.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya mkoa wa Kigoma,Maweni  akiongeza na Waandishi wa habari juu ya tukio la radi lililotokea hivi punde na kuuwa watu 8.

WATU wanane wakiwemo wanafunzi sita na mwalimu wa shule ya msingi Kibirizi  pamoja na mkazi wa eneo la Bangwe mjini Kigoma   wamefariki dunia baada ya kupigwa na radi huku wanafunzi wengi 15 wakijeruhiwa na radi hiyo leo mchana.

Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa kigoma(Maweni)Dkt Fadhili Kabaya amesema kuwa watu hao walifikwa na mauti hayo kufuatia mvua kubwa zilizonyesha zikiambana na radi zilizoanza majira ya saa sita mchana.

Dkt Fadhili amewataja waliopoteza maisha katika tukio hilo kuwa ni pamoja na mwalimu wa shule ya msingi Kibirizi Elinaza Mbwambo(25) na  Forcus Ntahaba(45)mkazi wa eneo la Bangwe mjini Kigoma.

Amewataja wanafunzi waliofariki dunia ambao wote ni wa darasa la kwanza kuwa ni Yusuph Ntahoma(8)Hassan Ally(9)Fatuma Sley(7)Zamda Seif(8)Shukrani Yohana(7) na Warupe Kapupa(10).

Amesema wamepokea majeruhi kumi na tano lakini kati yao kumi wametibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumba baada ya hali zao kuwa nzuri na watano wamelazwa wanaendelea na matibabu katika hospital ya Mkoa wa Kigoma.

Akisimulia tukio hilo mwalimu aliyekuwa anafundisha darasani Mwalimu Merina Sililo amesema  akiwa darasani akiendelea kufundisha ghafla aliona wingu zito jeusi limetanda hadi akashindwa kuendelea kuandika ubaoni.

''Manyunyu yalianza kidogo kidogo ikaja mvua kubwa na radi pamoja na miungurumo mikali sana ,iliyopelekea wanafunzi kuanguka ovyo darasa na kuzimia ,na mara niliona moto umetanda katika chumba kuzima cha darasa na mimi nilianguka chini na kupoteza fahamu''amesema mwalimu huyo.

Amesema apozinduka alijikuta katika hospitali ya Mkoa ya maweni akipatiwa matibabu baada ya kuletwa kwa msaada wa waalimu wenzake.

''Kwa kweli ni mungu tu mwenyewe ndiyo ameninusuru kwani nilirushwa mara tatu na radi na watoto wote wote darasani walikuwa wananiangukia mimi wengine walikuwa wanakimbia ovyo nje'',amesema Mwalimu huyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com