MAHAKAMA
ya Wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma, imewapa adhabu ya kufua mashuka ya
hospitali na kusafisha mitaro ya barabara kwa muda wa siku 14, watu
wanne akiwemo Diwani wa Kata ya Kasanda Wilayni Kakonko kupitia Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), baada ya kukutwa na hatia ya
makosa matatu.
Mbele
ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kibondo, Erick Marley,
Mwendesha Mashitaka wa Polisi Peter Makala, amemtaja diwani huyo kuwa ni
Dicksoni Barutwa (40), na Daudi Obadia (32), Hatari Kasase (33) na
Brighton Jonas (29), wote wakazi wa Kata ya Kasanda wilayani Kakonko.
Makala
alisema kuwa Novemba 8 mwaka jana -2014 majira ya saa kumi jioni katika
Kijiji cha Kazilamihunda, watuhumiwa wote kwa pamoja walifika eneo la
Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji hicho isivyo halali kisha kuifunga Ofisi
hiyo kwa kuweka gundi aina ya Super Grew, na unga wa ngano kwenye kufuri
ili kuzuia mtendaji asifanye kazi yake.
Inadaiwa
kuwa watu hao walifikia uamuzi huo kwa madai kuwa hawamtaki Mtendaji
huyo wa kijiji Amosi Peter, na kumtishia kuwa watamuua.
Kufuatia
hali hiyo Diwani huyo na wenzake, mahakama ya Wilaya ya Kibondo,
imewahukumu kulipa faini ya shilingi elfu 50 au kufungwa jela miezi
mitano kwa kosa la kufunga Ofisi ya Mtendaji na pia kulipa faini ya
shilingi elfu 50 au kutumikia jela miezi miwili kwa kosa la kufanya
fujo.
Watuhumiwa
wote wamelipa faini hizo na kuachiwa huru isipokuwa Hatari Kasase (33),
ambaye anakabiliwa na kesi nyingine ya mauaji hivyo anaendelea kusalia
gerezani.
Aidha
katika kosa la kutishia kuua diwani Barutwa, na wenzake wamehukumiwa
adhabu ya kazi za kijamii ambayo ni kufua mashuka ya hospitali ya wilaya
ya kakonko kwa muda wa wiki moja na kuzibua mitaro ya barabara kwa muda
wa wiki moja ambapo tayari wamekabidhiwa katika Idara ya Maendeleo ya
Jamii, na wataanza kutumikia adhabu hiyo baada ya siku kuu ya Pasaka.
Watuhumiwa
wengine katika kesi hiyo ambao ni Boniface Obadia (35), Amos Buseni
(33), Majaliwa Charles (24), pamoja na Samora Barichako (35), wote
wakazi wa kijiji Cha Kazilamihunda wilayani Kakonko wameachiliwa huru
baada ya kukutwa hawana hatia katika mashauri yote.
Chanzo:Kigomalive
Social Plugin