Imebainika kuwa wakati Bunge la Kumi likiwa limebakiza mkutano mmoja tu
wa bajeti kuhitimisha ngwe yake ya miaka mitano, wapo baadhi ya wabunge
ambao hawajauliza swali la msingi, la nyongeza wala kuchangia chochote.
Kwa
mujibu wa tovuti ya Bunge inayoonyesha idadi ya maswali yaliyoulizwa na
michango ya kila mbunge, wapo wabunge wawili ambao hawajawahi kuuliza
wala kuchangia chochote tangu Bunge hilo, lenye wabunge 358, lilipoanza
Uchaguzi Mkuu uliopita hadi sasa.
Vilevile,
tovuti hiyo inabainisha majina ya wabunge waliofanya vizuri zaidi
katika kila eneo, yaani maswali ya msingi, ya nyongeza na michango
waliyotoa katika mijadala mbalimbali.
Katika
orodha hiyo, Spika Anne Makinda, ambaye pia ni mbunge wa Njombe Kusini,
ndiye anayeonekana kinara kwa kuchangia mara 2,055 pale anapoongoza
Bunge na kuuliza swali moja huku naibu wake, Job Ndugai (Kongwa) akiwa
amechangia mara 1,350 bila kuuliza swali hata moja.
Kiwango
cha michango ya wabunge kimeelezwa na baadhi ya wasomi kuwa inategemea
mambo mengi, ikiwamo mbunge kuwa sehemu ya Serikali na hivyo kushindwa
kuihoji, uwezo wake kielimu na msimamo wake
kiitikadi. “Wabunge wengine tunaona ni
wafanyabiashara ambao hawana elimu. Walishinda kwenye uchaguzi kutokana
na fedha zao lakini hawana uelewa wa mambo. Sasa hawa hawawezi kuchangia
chochote kwa sababu hawajui,” alisema Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo
Kikuu cha Ruaha (Rucu) alipoulizwa kuhusu suala
hilo.
Katibu
msaidizi wa Bunge, Emmanuel Mpanda alisema pamoja na kuwa taarifa za
tovuti hiyo zinahuishwa mara kwa mara, zilizomo kwa sasa hazihusishi
michango ya wabunge ya Mkutano wa 19 uliomalizika Aprili Mosi.
Alisema
orodha ya wabunge 10 waliochangia sana na wengine 10 waliochangia mara
chache, haihusishi kiti cha spika, wenyeviti wa Bunge na mawaziri.
Wabunge 10 wenye michango michache
Nambari
moja inashikwa na wabunge wawili ambao pia ni viongozi wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ambao ni mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi,
Mohamed Said Mohamed (CCM) ambaye ni mwakilishi wa Mpendae na Naibu
Waziri wa Kilimo na Maliasili, pamoja na mbunge wa Kitope (CCM), Balozi
Seif Ali Iddi ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar. Hao
ndiyo pekee ambao hawakuchangia kitu chochote bungeni.
Anayefuatia ni mbunge wa Babati Mjini, Kisyeri Chambiri (CCM) ambaye amechangia mara nne lakini hakuwahi kuuliza swali lolote.
Katika
orodha hiyo wabunge waliochangia mara tano bila kuuliza maswali yoyote
ni Dk Mohamed Seif Khatibu (Uzini - CCM), Edward Lowassa (Monduli),
Shawana Hassan (Dole - CCM). Mbunge wa Kalenga, Godfrey Mgimwa aliuliza
maswali matatu ya nyongeza na kuchangia mara mbili.
Mwingine ni Ali Haji Juma wa (Chaani – CCM) aliyechangia mara nne, akauliza swali moja la msingi na moja la nyongeza.
Wanafuatia
Khamis Ali Kheir wa Jimbo la Kwamtipura (CCM) aliyechangia mara nane
bila kuuliza swali lolote, wabunge wa viti maalumu (CCM), Mwanakhamis
Kassim Said aliyeuliza swali moja la msingi na kuchangia mara saba na
Kiumbwa Mbaraka aliyeuliza maswali manne na kuchangia mara tatu.
Wabunge 10 waliochangia zaidi
Wabunge
waliochangia mara nyingi wanaongozwa na John Mnyika wa Ubungo (Chadema)
ambaye amechangia mara 540 na kuuliza maswali 16 ya msingi na 52 ya
nyongeza.
Anayefuatia
katika orodha hiyo ni Tundu Lissu (Singida Mashariki - Chadema) mwenye
michango 276, maswali manane ya msingi na 24 ya nyongeza.
Mbunge
wa tatu ni wa Kasulu Mjini (NCCR - Mageuzi), Moses Machali ambaye
aliuliza maswali 23 ya msingi, 68 maswali ya nyongeza na kuchangia mara
214.
Nambari
nne imekwenda kwa Mbunge wa Kilwa (CCM), Murtaza Mangungu aliyeuliza
maswali 26 ya msingi 74 ya nyongeza na kuchangia hoja mara 131.
Mbunge
wa tano ni Diana Chilolo (Viti Maalumu-CCM) aliyeuliza maswali ya
msingi 19, ya nyongeza 88 na michango 116, wa sita ni Leticia Nyerere
(Viti Maalumu - Chadema) aliyeuliza maswali 23 ya msingi, 60 ya nyongeza
na kuchangia mara 139.
Anayeshika
namba saba ni Halima Mdee wa Kawe (Chadema) aliyeuliza maswali 11 ya
msingi, 32 ya nyongeza na michango 175. Nambari nane imeshikwa na Felix
Mkosamali (Muhambwe-NCCR) aliyeuliza maswali 19 ya msingi, 44 ya
nyongeza na michango 151.
Aliyeshika
namba tisa ni Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini - Chadema) aliyeuliza
maswali 13 ya msingi, 49 ya nyongeza na michango 149 kabla ya kujiuzulu
ubunge baada ya kufukuzwa uanachama na chama chake.
Mbunge wa 10 ni Seleman Jafo (Kisarawe-CCM) aliyeuliza maswali ya msingi 17, ya nyongeza 35 na michango 141.
Mtazamo wa wasomi
Profesa
wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala alisema hatua ya
baadhi ya wabunge kukaa kimya bungeni ina sura mbili. Kwanza; baadhi yao
wanajiona ni sehemu ya Serikali kwa hiyo wanaogopa kuikosoa.
Alisema
kundi hili linajumuisha baadhi ya wabunge ambao ni mawaziri, waliowahi
kuwa mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na baadhi ya wabunge
kutoka CCM.
Kundi
la pili, Profesa Mpangala alisema ni la wabunge wenye upeo mdogo wa
mambo, kwa kuwa ili mbunge aweze kuuliza maswali na kuchangia hoja,
lazima awe na upeo mkubwa wa mambo ya kijamii, kiuchumi na kimataifa.
Mwanazuoni
huyo alikumbuka pendekezo lililotolewa kwenye Rasimu ya Katiba kuweka
sifa ya elimu kwa mbunge, lakini likatupiliwa mbali kwa sababu kiligusa
masilahi ya wabunge wengi.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Bakari Mohamed alisema kuna
mambo ambayo Serikali inakuwa imeweka msimamo, hivyo wabunge walio
kwenye mrengo wa Serikali hawawezi kuuliza au kuchangia kinyume na
msimamo waliouweka.
Alisema wabunge wanatofautiana kiutendaji, baadhi wakijizatiti kwenye majimbo yao bila kuona umuhimu wa kuzungumza bungeni.
Hata
hivyo, alisema wabunge wa namna hiyo hawana sifa za kuwa wabunge kwa
sababu ni udhaifu mkubwa kukaa bungeni miaka mitano ukashindwa kuuliza
au kuchangia chochote chenye masilahi kwa wananchi.
Msomi
huyo aliongeza kuwa pamoja na kuwapo viongozi wa Serikali bungeni ambao
hawawezi kuikosoa, jambo hilo haliwanyimi fursa ya kuuliza au kuchangia
juu ya mambo yanayohusu majimbo yao.
CHANZO: Gazeti la Mwananchi
Social Plugin