Mtaalam wa Macho fani ya Uoni Hafifu kutoka hospitali
ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga Dkt Ntoke Sospeter Wilson akiwaelekeza watoto hao
namna ya kutumia Darubini Kiona mbali-Picha zote na Kadama Malunde-Shinyanga
*************
Shirika la
Bima la Taifa leo limetoa msaada wa vifaa 34 vya kuwasaidia watoto wenye uoni
hafifu katika kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu wa ngozi(Albino) cha
Buhangija katika manispaa ya Shinyanga kutokana na idadi kubwa ya watoto hao kukabiliwa na changamoto ya uoni hafifu.
Vifaa
vilivyotolewa na Shirika la bima la taifa ni pamoja
na Darubini kiona mbali(Telescope
Monocular),kikuza maandishi cha Kusimamisha(Stand Magnifier) na Kikuza
Maandishi cha Kuweka juu ya Maandishi( Dome Magnifier).
Akizungumza
wakati wa kukabidhi vifaa hivyo mbele ya mstahiki meya wa manispaa ya Shinyanga
Gulam Hafeez Mukadam, meneja wa Shirika la Bima la Taifa tawi la Shinyanga
Halima Makange alisema shirika hilo limeguswa na changamoto ya vifaa vya
kujifunzia kwa wanafunzi wenye ulemavu wanaolelewa katika kituo hicho na kuamua
kutoa msaada huo.
Alisema
lengo la kutoa vifaa hivyo ni kuendeleza elimu kwa watoto hao kwani elimu ni
jambo la msingi kwao pamoja na kwamba wanapata hifadhi katika kituo hicho.
“Kilichowaleta
hapa watoto hawa ni elimu,tunahitaji kuwaendeleza kielimu ndiyo maana tumeleta
vifaa hivi 34,ambavyo vitawasaidia kujifunzia darasani”,alisema Makange.
“Kwa niaba
ya mkurugenzi wa shirika la bima la taifa Dar es salaam,nimeleta msaada huu
kuungana na jamii kuwasaidia watoto wetu,ingawa vifaa hivi ni vidogo kwa
kuviangalia lakini bei yake ni kubwa,tunamshukuru mkurugenzi wetu kwa kuona
umuhimu wa kutoa vifaa hivi,naomba vitumike kama vilivyokusudiwa”,aliongeza
Makange.
Kwa upande
wake mstahiki meya wa manispaa ya Shinyanga Gulam Hafeez Mukadam alisema vifaa
hivyo vitakuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi wenye uoni hafifu waliopo katika
kituo hicho cha walemavu.
“Kwanza
niushukuru uongozi mzima wa shirika la bima la taifa kwa kunikaribisha kuja kukabidhi vifaa
hivi,kwa niaba ya halmashauri ya manispaa ya Shinyanga tunashukukuru sana kwa msaada
huu,naomba shirika liendelee kutoa ushirikiano kwa jamii kwani wanatambua nini
jamii inahitaji,tutaendelea kushirikiana zaidi”,aliongeza Mukadam.
Naye
Mtaalamu wa Macho Fani ya Uoni Hafifu kutoka hospitali ya rufaa ya mkoa wa
Shinyanga Dkt. Ntoke Sospeter alisema vifaa hivyo vitatumika kuwaendeleza zaidi
kimasomo watoto hao ili wafanane na watoto wengine wasiokuwa na tatizo la uoni
hafifu.
“Mtoto
asiye ana tatizo la uoni hafifu anaona maandishi mapema zaidi,mwenye uoni
hafifu anakuwa na uwezo mdogo wa kufikia maandishi,hivyo tunapompa kifaa
tunamsaidia kufikia wenzake wanapofika”,alieleza Dkt Sospeter.
Kwa upande
wake msimamizi mkuu wa kituo cha Kulelea watoto wenye Ulemavu wa
ngozi(Albino),wasioona na wasiosikia Peter Ajali alilishukuru Shirika la bima
la taifa kwa msaada huo kwani wamelenga kudumisha akili za watoto kimasomo.
Alisema
asilimia kubwa ya watoto waliopo katika kituo hicho hawana uwezo wa kuona mbali
hivyo vifaa vilivyotolewa vitawasaidia kuweza kuona maandishi kwa ufasaha
zaidi.
|