Kiongozi wa ACT-Tanzania Zitto Kabwe akiwahutubia wakazi wa Iringa katika viwanja vya Mwembetogwa Manispaa ya Iringa-Picha na Yonna Mgaya-Malunde1 blog Iringa |
Kuelekea
uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu Chama cha ACT-Tanzania kimefanya mkutano wa
uzinduzi wa chama ambao ni wa kwanza mkoani Iringa kwa kuwatambulisha viongozi
wake pamoja na kuwaeleza sera ya chama hicho.
Akizungumza
katika mkutano huo uliofanyika kwenye viwanja vya Mwembetogwa Manispaa ya
Iringa jana ,Kiongozi wa ACT-Tanzania Zitto Kabwe alisema msingi na
nguzo kuu ya chama hicho ni sera ya ujamaa ambayo ilitumiwa na enzi za uhai na
uongozi wa hayati mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Kabwe
aliongeza kuwa kuongezeka kwa wimbi la umasikini nchini imetokana na baadhi ya viongozi
wa nyanja mbalimbali kutotekeleza ahadi zao kwa wananchi pia kujinufaisha wao
zaidi kuliko kuwatumikia wananchi waliowapa kura kwa kuboresha maisha yao.
Aidha alisema taifa linapoteza kiasi kikubwa cha fedha kutokana na uwepo wa sera mbovu
za uthibiti wa rasilimali za madini,mbuga za wanyama,mafuta pamoja na ardhi
hali inayowafanya wawekezaji kutoka nchi za ulaya kuendelea kunufaika na
rasilimali hizo.
Katika hatua nyingine Zitto alimtaka waziri wa uchukuzi Samwel Sita kufanya uchunguzi wa uwepo wa tuhuma za ubadilifu kwa baadhi ya vigogo
waliofukuzwa kwa tuhuma za account ya Escrow kupewa mkataba wa zaidi ya kiasi
cha shilingi tilioni 54 kwa ajili ya kumilikishwa bandari ya Pangani mkoani
Tanga.
Naye
Mwenyekiti wa Chama hicho Bi.Anna Mghwira aliwataka wananchi kushiriki katika
uandikishaji wa daftari la kudumu la mpiga kura pindi muda ukifika.
Aidha
aliitaka serikali kutenga muda wa kutosha ili watu waweze kuipitia na kuielewa
katiba pendekezwa na kisha kuipigia kura.
Mghwira
alitoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Iringa kushirikiana kwa pamoja katika kulinda
amani na utulivu wa nchi.
Pia alitoa wito kwa wanawake kujitokeza kuwania kwenye
nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Hata
hivyo ziara ya mikutano ya Chama hicho kwa mkoa wa Iringa pia ilifanyika kwenye
mji mdogo wa Mafinga wilaya ya Mufindi ambapo kitaifa ilizinduliwa katika mji
wa Songea mkoani Ruvuma na inaendelea kwa mikoa zaidi ya kumi nchini ikiwa ni
pamoja na mikoa ya Morogoro na Dodoma.
Na Yonna Mgaya-Malunde1 blog Iringa
Social Plugin