Askofu mteule wa jimbo katoliki la Shinyanga Liberatus Sangu Hayati Askofu Aloysius Balina |
Askofu mteule wa jimbo katoliki la Shinyanga Liberatus Sangu
leo amepokelewa rasmi katika jimbo la Shinyanga akitokea katika jimbo la
Sumbawanga alikokuwa anapumzika na kufanya mafungo maalum.
Mapokezi hayo yamefanyika leo asubuhi katika daraja la mto Manonga
lililopo mpakani mwa jimbo kuu la Tabora na Shinyanga ambapo waumini kutoka
sehemu mbalimbali kutoka jimbo la Shinyanga na maeneo ya jirani walikusanyika
kwa ajili ya kumlaki.
Akiwa katika eneo hilo askofu Sangu alibusu ardhi ya jimbo
la Shinyanga pamoja na kuwabariki waumini.
Baada ya kuwasili mjini Shinyanga alipita katika parokia ya
Buhangija kwa ajili ya Mazungumzo mafupi na padre wa kwanza mzalendo wa jimbo
la Shinyanga Mosinyo Zacharia Bruda kisha kupanda mti wa kumbukumbu katika
parokia hiyo.
Baada ya mapumziko mafupi askofu huyo alishiriki katika
ibada ya masifu ya jioni katika kanisa la mama mwenye huruma la Ngokolo mjini
Shinyanga ambapo alianza kwa kuonesha kwa kuonesha hati ya kitume kisha
kukabidhiwa funguo za kanisa kuu kabla ya kuingia kanisani.
Baadaye aliungama kanuni ya imani na kula kiapo cha uaminifu
kabla ya zana zake za kazi atakazozitumia katika utume wake kubarikiwa.
Ibada hiyo ya masifu ya jioni imeongozwa na askofu wa jimbo
la Bunda mhashamu Renatus Nkwande.
Kesho Askofu mteule Lebaratus Sangu atawekwa wakfu na
kusimikwa rasmi kuwa askofu wa jimbo katoliki la Shinyanga katika misa maalum
ambayo itafanyika katika kanisa kuu la mama mwenye huruma la Ngokolo mjini
Shinyanga,itakayoanza majira ya saa 3:45 asubuhi ambapo rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete anatarajiwa kuhudhuria misa hiyo.
Askofu Sangu anachukua nafasi ya aliyekuwa askofu wa jimbo
hilo Aloysius Balina aliyefariki dunia mwaka 2012.
Askofu mteule Sangu amefanya kazi katika Baraza la Kipapa la
Uinjilishaji wa Watu kwa muda wa miaka minane.
Askofu mteule Sangu amefundwa akafundika sasa anakabidhiwa
kazi ya kufundisha, kuongoza na kuwatakasa watu wa Mungu Jimbo Katoliki
Shinyanga.
Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata na Rais wa
Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa ni kati ya viongozi wa Kanisa wanaotarajiwa
kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumweka wakfu na hatimaye,
kumsimika Askofu mteule Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga,
Jumapili ya huruma ya Mungu kesho tarehe 12 Aprili 2015, Jimboni Shinyanga.
Imeandaliwa na Kadama Malunde kwa kushirikiana na Radio Faraja Fm na Vatican Radio.
Social Plugin