Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JINSI ASKOFU MTEULE WA JIMBO KATOLIKI LA SHINYANGA LIBERATUS SANGU ALIVYOPOKELEWA LEO SHINYANGA

Askofu mteule wa jimbo katoliki la Shinyanga Liberatus Sangu
 Hayati Askofu Aloysius Balina

Askofu mteule wa jimbo katoliki la Shinyanga Liberatus Sangu leo amepokelewa rasmi katika jimbo la Shinyanga akitokea katika jimbo la Sumbawanga alikokuwa anapumzika na kufanya mafungo maalum.

Mapokezi hayo yamefanyika leo asubuhi katika daraja la mto Manonga lililopo mpakani mwa jimbo kuu la Tabora na Shinyanga ambapo waumini kutoka sehemu mbalimbali kutoka jimbo la Shinyanga na maeneo ya jirani walikusanyika kwa ajili ya kumlaki.

Akiwa katika eneo hilo askofu Sangu alibusu ardhi ya jimbo la Shinyanga pamoja na kuwabariki waumini.

Baada ya kuwasili mjini Shinyanga alipita katika parokia ya Buhangija kwa ajili ya Mazungumzo mafupi na padre wa kwanza mzalendo wa jimbo la Shinyanga Mosinyo Zacharia Bruda kisha kupanda mti wa kumbukumbu katika parokia hiyo.

Baada ya mapumziko mafupi askofu huyo alishiriki katika ibada ya masifu ya jioni katika kanisa la mama mwenye huruma la Ngokolo mjini Shinyanga ambapo alianza kwa kuonesha kwa kuonesha hati ya kitume kisha kukabidhiwa funguo za kanisa kuu kabla ya kuingia kanisani.

Baadaye aliungama kanuni ya imani na kula kiapo cha uaminifu kabla ya zana zake za kazi atakazozitumia katika utume wake kubarikiwa.

Ibada hiyo ya masifu ya jioni imeongozwa na askofu wa jimbo la Bunda mhashamu Renatus Nkwande.

Kesho Askofu mteule Lebaratus Sangu atawekwa wakfu na kusimikwa rasmi kuwa askofu wa jimbo katoliki la Shinyanga katika misa maalum ambayo itafanyika katika kanisa kuu la mama mwenye huruma la Ngokolo mjini Shinyanga,itakayoanza majira ya saa 3:45 asubuhi ambapo rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete anatarajiwa kuhudhuria misa hiyo.

Askofu Sangu anachukua nafasi ya aliyekuwa askofu wa jimbo hilo Aloysius Balina aliyefariki dunia mwaka 2012.

Askofu mteule Sangu  amefanya kazi katika Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu kwa muda wa miaka minane.

Askofu mteule Sangu amefundwa akafundika sasa anakabidhiwa kazi ya kufundisha, kuongoza na kuwatakasa watu wa Mungu Jimbo Katoliki Shinyanga.

Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata na Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa ni kati ya viongozi wa Kanisa wanaotarajiwa kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumweka wakfu na hatimaye, kumsimika Askofu mteule Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Jumapili ya huruma ya Mungu kesho tarehe 12 Aprili 2015, Jimboni Shinyanga.

Imeandaliwa na Kadama Malunde kwa kushirikiana na Radio Faraja Fm na Vatican Radio.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com