Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MADHARA YA MGOMO WA MADEREVA WA MAGARI NA JINSI ULIVYOYEYUKA


Waziri wa Kazi na Ajira Mhe. Gaudencia Kabaka amefanikiwa kumaliza mgomo wa madereva baada ya kutangaza kufuta agizo lililokuwa likiwataka madereva wa mabasi na malori kwenda kusoma tena katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT)



Kuhusu suala la Madereva kusoma, Serikali na Madereva wamekubaliana kukutana mwezi huu tarehe 18 kuzungumza njia mbadala ya kutumika.


Miongoni mwa malalamiko ya madereva ilikuwa ni kukerwa na tochi za barabarani, hivyo jeshi la Polisi wamekubali kuziondoa.
Pia serikali imeagiza Madereva wote wapewe mikataba ya ajira za uhakika na waajiri wao na Trafiki wameagizwa kulifuatilia hilo.

KUTOKA MWANZA

Mamia ya abiria wanaotumia usafiri wa mabasi yanayokwenda katika mikoa mbalimbali nchini pamoja na nchi jirani ya Uganda kutokea kituo kikuu cha mabasi Nyegezi jijini Mwanza wameshindwa kusafiri kwa muda unaotakiwa, kufuatia mgomo wa madereva wa mabasi uliofanyika leo asubuhi katika maeneo mbalimbali nchini.


Mgomo huo umeanza majira ya saa 12.00 asubuhi na kusababisha malalamiko kutoka kwa abiria waliokuwa na shauku ya kuanza mapema safari yao.

Sakata la mgomo huo uliodumu kwa zaidi ya saa 6, likatua mikononi mwa mkuu wa wilaya ya Nyamagana Baraka Konisaga, ambaye bila ajizi akatoa agizo kwa madereva wa mabasi hayo ya abiria kuhakikisha wanasitisha mgomo huo mara moja ili kuwasafirisha abiria.

Baadhi ya madereva wa mabasi hayo ya abiria yapatayo 60 yanayotumia stendi ya Nyegezi, wamevunja ukimya na kueleza sababu zilizopelekea kugoma na kusababisha usumbufu mkubwa kwa abiria wakiwemo wagonjwa na watoto, huku makamu mwenyekiti wa umoja wa madereva mkoa wa Mwanza Shaban Wandiba akiwasihi madereva hao kutii agizo la mkuu wa wilaya ya Nyamagana.

HUKO MOROGORO VIPI?

Jeshi la Polisi mkoa wa Morogoro limewakamata watu saba na kuwafikisha mahakamani kwa tuhuma za kufanya vurugu na kuzuia  madereva wa mabasi na daladala wasipakize abiria kufuatia kuwepo kwa  mgomo.


Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro Leonard Paul amesema jeshi la  polisi limewakamata vinara waliokuwa wakiongoza mgomo kwa kuzuia madereva wa daladala wasipakie abiria hali iliyosababisha abiria kushindwa kusafiri kwa masaa kadha ambapo amesema katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Morogoro  watuhumiwa hao wamesomewa mashtaka.


Hali ya usafiri mkoani Morogoro imerejea ambapo wakazi wa mkoa wa Morogoro wakizungumzia hali ya mgomo huo wamepongeza hatua ya jeshi la polisi kuchukua hatua na kuwakamata vinara waliokuwa wakichochea mgomo mjini Morogoro na kuitaka serikali kuwa na utamaduni wa kutatua kero za malalamiko ya wananchi badala ya kusubiri kutibu matokeo huku akielezea adha waliyoipata kutokana na mgomo huo.


KUTOKA MUSOMA 

 

Abiria zaidi elfu moja waliokuwa wakisafiri kutoka Musoma kwenda Dar es Salaam kupitia mikoa ya Mwanza na Shinyanga wale wanaokwenda mpakani mwa Tanzania na Kenya Sirari pamoja na wa ndani ya mkoa wa Mara wameshindwa kusafiri baada ya madereva kuitisha mgomo.


Baadhi ya madereva ambao wamekutwa katika kituo kikuuu  cha  mabasi ya Bweri mjini Musoma,wamesema mgomo huo  umeitishwa kwa ajili ya kupinga agizo la serikali la kukataa kusajili upya leseni zao hadi baada ya kwenda kusoma katika vyuo  vinavyotambulika serikalini.

Kwa upande wao baadhi ya abiria wamesikitishwa na mgomo huo wa madereva ambao umesababisha hata wagonjwa kushindwa kusafiri hivyo wameita serikali kuchukua hatua za kumaliza migomo hiyo ambayo wamesema imekuwa kero kubwa kwa wananchi.

Mwandishi wa habari hizi ameshuhudua abiria hao wakiwa wamesimama kwa makundi katika kituo hicho kikuu cha mabasi huku magari makubwa ya abiria  yakishindwa kuingia kabisa kituoni hapo hatua ambayo imesabisha  baadhi ya abiria wakilazimika kukodisha  magari madogo aina ya taxi kwenda jijini mwanza kwa gharama ya shilingi laki nne kutoka laki mbili za kawaida.

CHANZO-Wadau mbalimbali wa Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com