CHAMA
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimewatoa hofu wanachama wake
mkoani Shinyanga kikidai propaganda zinazoenezwa na Kiongozi Mkuu wa
Chama cha ACT-Wazalendo, Bw. Zitto Kabwe, anayedai chama hicho
kimepoteza mwelekeo si za kweli bali ni uongo.
Mbunge
wa Arusha Mjini ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA Taifa,
Bw. Godbless Lema, aliyasema hayo hivi karibuni mkoani Shinyanga kwenye
mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Mahakama ya Mwanzo.
Alisema
chama chao bado kipo imara na hakitagawanyika kama inavyodaiwa na Bw.
Kabwe ambaye CHADEMA kilimfukuza katika chama baada ya kukisaliti hivyo
kukiuka Katiba ya chama hicho.
"Ndugu
zangu wana Shinyanga, CHADEMA tupo imara na tutaendelea kuwa imara hadi
tukamate dola na kuwakomboa Watanzania ambao wanateseka tangu tupate
uhuru.
"Zitto
hana ubavu wa kukigawa chama chetu kama anavyofikiri na
kuamini...anahangaika bure, alitaka kukiua tukamshtukia na mimi ndiye
mtu wa kwanza kubaini njama zake na wenzake akiwemo Samson Mwigamba na
Profesa Kitila Mkumbo; hivyo hawatubabaishi kwa lolote," alisema.
Bw.
Lema aliongeza kuwa, Bw. Kabwe alikuwa chanzo cha kufifisha ushindi wa
CHADEMA katika baadhi ya majimbo katika Uchaguzi Mkuu wa 2010 baada ya
kutoa taarifa za uongo kwa wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo ya
Katavi, Musoma Vijijini na Singida Mjini na kusababisha wagombea wa CCM
wapite bila kupingwa.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho Taifa
(BAVICHA), Patrobass Katambi, aliwataka wanachama wa CHADEMA kusimama
imara ili kukiimarisha chama chao na waachane na Bw. Kabwe aliyeonesha
dhahiri usaliti wake baada ya kujiunga na Chama cha ACT-Wazalendo.
"Huyu
Bw. Kabwe alikana katakata kujihusisha na Chama cha ACT-Tanzania kama
kilivyofahamika awali; lakini siku chache baada ya kutimuliwa CHADEMA
akajiunga nacho.
"Anawadanganya
Watanzania kuwa yeye ni mjamaa na moja ya sababu iliyomtoa CHADEMA ni
kutokuwepo demokrasia ya kweli...kama kweli anathamini demokrasia mbona
baada ya kujiunga na ACT ghafla amejitangazia madaraka ya Kiongozi Mkuu
wa chama," alihoji Katambi.
Katika
hatua nyingine, CHADEMA kimetoa wito kwa wakazi wa Mkoa huo kujitokeza
kwa wingi ili kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura
waweze kupata haki yao ya kuchagua viongozi waadilifu katika Uchaguzi
Mkuu.