Watu
wawili wamefariki mkoani Iringa akiwemo askari wa Jeshi la kujenga
Taita (JKT) na mtu mmoja anayetuhumiwa kuwa ni jambazi wakati wa
kurushiana risasi na jeshi la polisi baada ya kufanya uporaji eneo la
Mafinga wilaya ya Mufindi.
Kamanda
wa Jeshi la polisi mkoa wa Iringa ACP Ramadhani Mungi amesema Salma Semwiko
mfanyabiashara na mkazi wa Mafinga akiwa anaelekea kazini alivamiwa na
mtu aliyekuwa na silaha aina ya SMG kisha kumpora simu na fedha zaidi ya
laki saba.
Ameongeza
kuwa baada ya uporaji huo ilitokea pikipiki aina ya bodaboda na
kumchukua jambazi huyo kisha kukimbilia eneo la Kinyanambo na ndipo
yalipotokea majibizano ya silaha wakati polisi na wananchi wakifanya
jitihada za kuwakamata majambazi hao.
Kamanda
Mungi amesema Saidi Ng’umbi askari wa JKT amefariki papo hapo baada ya
kupigwa kifuani upande wa kulia na majambazi hao.
Amesema jeshi la polisi
wamefanikiwa kumkamata jambazi mmoja ambaye amefariki wakati akiendelea
kupatiwa matibabu baada ya kupigwa kwenye paja la mguu.
Aidha
ameongeza kuwa jeshi la polisi mkoani Iringa linaendelea na uchunguzi
zaidi wa tukio hilo ikiwa ni pamoja na kumtafuta jambazi aliyekimbia
katika tukio hilo.
Wakati
huo huo Kamanda Mungi amesema Winifrida Frank umri wa miaka 25 mkazi wa
eneo la Ipogolo Manispaa na Mkoa wa Iringa anashikiliwa na jeshi la
polisi kwa tuhuma ya mauaji ya kumtupa mtoto mwenye umri siku tatu
kwenye shimo la maji machafu.
Na Yonna Mgaya-Malunde1 blog Iringa
Social Plugin