Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha |
Mwanamke mmoja mkazi wa Kitongoji cha Ulowa katika kijiji cha Ulowa namba 4 wilayani Kahama mkoani Shinyanga,Chausiku Hamis (54)ameuawa kwa kupigwa mawe kisha kuchomwa moto na kundi la mwananchi wenye hasira katika msiba wa mtoto Deus Peter (1) baada ya mama moja kupandisha majini na kusema
bibi Chausiku anahusika na kifo cha mtoto huyo.
Diwani wa kata hiyo Paschal Manyego ameiambia Malunde1 blog kuwa chanzo cha tukio hilo kinatokana na mtoto Deus Peter mwenye umri wa mwaka moja ambaye inasemekana alifariki katika mazingira ya
kutatanisha.
Kufuatia utata wa kifo cha mtoto huyo siku ya msiba mama moja aliyehudhuria msiba huo alipandisha majini na
kumtaja bi Chausiku Hamisi ndiyo anahusika na kifo cha mtoto huyo.
"Ilikuwa 26.3.2015 majira ya saa 2.30 usiku wakati wananchi wa kitongoji hicho walikuwa nyumba kwa mzee Peter,kwa ajili ya
kumfariji,ghafla mama moja aliyekuwepo hapo alipandisha mashetani
na kumtaja bibi Chausiku Hamis kuwa anahusika na kifo cha mtoto huyo",alieleza Diwani
“Mimi sikuwepo katika msiba huo wa mtoto
huyo ila nilipigiwa simu na mtendaji wa kitongoji kuwa kuna fujo kwenye
msiba kwa mzee Peter kuna mama amepandisha mashetani,anasema kuwa bibi Chausiku ndiyo ameficha mtoto huyo na ndipo wananchi walipoanza kumzonga, mama
huyo na kuanza kumponda mawe".
"Alipoona hali inakuwa mbaya bibi huyo alikimbilia
ndani ya nyumba ili kuokoa maisha yake lakini wananchi hao walimfuata na kumtoa
nje ya nyumba yake na kuendelea kumponda kwa mawe mpaka kufa na kisha kumchoma moto" alisimulia Mayengo diwani wa kata ya ulowa.
Diwani Paschal alisema mwenyekiti wa serikali ya
mtaa na mtendaji wa kitongoji hicho wote wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa
uchunguzi wa tukio hilo la kusikitisha kwa jamii.
Akizungumzia tukio hilo mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja alilaani vikali vitendo kama hivyo vya kuwaua vikongwe na kudai kuwa ni
laana kubwa sana kuua watu wasio na hatia kwa kuamini mambo ya uongo huku akiitaka jamii kubadilika kwa kuacha kujichukulia sheria mkononi.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus
Kamugisha alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Na Kadama Malunde-Kahama