Chama
cha Alliance for Change and Transparency (ACT), kimesema kinatarajia
kunyakuwa majimbo manne ya ubunge katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika
Oktoba, mwaka huu.
Kimetaja
majimbo hayo kuwa ni Ubungo, ambalo linaongozwa na John Mnyika
(Chadema), Kawe linaloshikiliwa na Halima Mdee (Chadema), Segerea ambalo
Mbunge wake ni Makongoro Mahanga (CCM) na Kahama la James Lembeli
(CCM).
Kiongozi Mkuu wa Chama hicho, Zitto Kabwe, alisema hayo katika kipindi cha Hot Mix kinachorushwa na kituo cha EATV.
Zitto aliendeleza msimamo wake wa kutogombea ubunge kwenye jimbo lake la awali la Kigoma Kaskazini.
“Nina
maombi jimbo la Kahama, Kawe, Ubungo na Segerea lakini kwa kuwa ACT
kinaongozwa kizalendo, tutaweka utaratibu mzuri wa kuweka wagombea kila
eneo, binafsi kwa sasa siwezi kusema wapi nitagombea,” alisema.
Alipoulizwa ni eneo gani kati ya hayo aliyoyataja huduma yake inahitajika, alijibu kwa kifupi kuwa, nchi nzima ina muhitaji.
“Kabla
ya kampeni kuanza wagombea wakirudisha fomu ndipo mtajua Zitto
anagombea jimbo gani, lakini lazima niongozwe na chama nikagombee wapi ,
wanaweza kusema Zitto kagombee jimbo A,” alisema.
Aliongeza
kuwa, ACT kinahitaji kujipanga kuingia kwenye mapambano ya kufyeka
msitu wa siasa kwa kuwa ndani yake kuna vyama zaidi 22 na vingine vikiwa
na uzoefu mkubwa kutokana na kudumu zaidi ya miaka 23.
Alisema kazi kubwa walionayo ni kukijenga chama ili kiweze kulirudisha taifa kwenye misingi ya waasisi waliyoiacha.
Aliongeza kuwa, baadhi ya watu wanamuona kama anaanza upya kwa sababu wapo wachache waliwahi kujaribu na kuishia njiani.
Alipoulizwa kuhusu wachambuzi wa siasa wanavyomchukulia hivi sasa, Zitto alisema wapo wenye mtazamo hasi na wengine chanya.
Alisema
kwa wale wanaomchukulia kwa mtazamo hasi anaendelea kuwafundisha na
kuwaonyesha kwamba muono wao ni tofauti wakati wale wa chanya anaendelea
kuwasikiliza ili kupata muongozo zaidi kutoka kwao.
“Tukumbuke
hii nchi watu wamezoea kuchukia mabadiliko angalia kwenye sanaa
wakimuona Diamond amefanikiwa waanza kutoa maneno ambayo siyo, watu
wanachukia mabadiliko,” alisema.
Udaku Specially Blog
Social Plugin