ALIYERUSHA RISASI KWENYE MSAFARA WA MBUNGE CHENGE AHUKUMIWA KULIPA FAINI YA SHILINGI ELFU 2!!



Mahakama ya wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, imemhukumu Ahmed Ismael (34) mfanyabiashara mkazi wa Salunda Bariadi mjini kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini shilingi 2000 kwa kosa la kupatikana na hatia ya kutumia silaha kwenye mkusanyiko wa watu.

Mahakama hiyo ilitoa adhabu kwa mshitakiwa huyo, ambaye ni kada wa Chama Cha Mapinduzi wilayani Bariadi, chini ya sheria ya makosa ya jinai kifungu namba 4(1),(2) na (8) cha sheria za mikusanyiko ( Public Order Act) sura namba 385 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2012.

Akisomewa makosa yanayomkabili na mwendesha mashtaka mwanasheria wa serikali Mkoani Simiyu Yamiko Mlekano, alisema mtuhumiwa anatuhumiwa wa makosa mawili.

Yamiko alisema kosa la kwanza mnamo tarehe 22/04/2015 majira ya saa 10-12 jioni mshitakiwa akiwa katika mkusanyiko wa watu ndani ya kijiji cha Isanga wilaya ya Bariadi alipatikana na silaha aina ya Pistol (TISAS) yenye namba za usajili No.0620-11J00502.

Alibainisha kosa la pili kuwa siku na tarehe hizo hizo mshitakiwa akiwa katika maeneo ya Salunda kando kando ya Barabara kuu ya Bariadi-Maswa katika mkusanyiko wa watu alipatikana na kutumia silaha hiyo kinyume cha sheria.

Mbele ya hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama hizo Aidan Mwilapwa, mshtakiwa alikiri makosa yote, huku mwendesha mashtaka huyo akiitaka mahakama kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa hiyo ili iwe fundisho kwa watu wengine.

Akitoa hukumu juu ya makosa hayo hakimu Mwilapwa alisema kosa la kwanza mahakama imetoa adhabu ya kifungo cha kwenda jela miazi 6 au kulipa faini shilingi 1000, na kosa la pili kifungo jela miezi 6 au faini shilingi 1000.

Kwa makosa yote mahakama ilimuhukumu kwenda jela mshitakiwa kifungo cha kwenda jela mwaka 1 au faini shilingi 2000, ambapo aliweza kulipa faini hiyo na kuanikiwa kuwa huru.

Hivi karibu wakati Mbunge wa Bariadi Magharibi Andrew (CCM) Chenge alinusurika kipigo kutoka kwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Simiyu baada ya kupita katika ofisi zao akitoka kwenye mkutano wake.

Wakati akipita katika ofisi za chama hicho wafuasi waliokuwepo walianza kuushambulia kwa mawe msafara wa mbunge huyo kwa kile kilichoelezwa kuwa alikuwa akiwapigia kelele kutokana na moja ya gari lake la matangazo likiwa linapiga muziki wa chama chake (CCM).

Kutokana na tafrani hiyo Mfuasi huyo ambaye ni kada mkubwa wa CCM wilayani Bariadi, alirusha risasi 2 hewani kwa lengo la kuwatawanya wafuasi wa chadema walikuwa wakirusha mawe, huku akieleza kuwa sababu ya kurusha risasi ni kutaka kumuokoa mbunge huyo asipigwe na wafuasi hao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post