Imebainishwa kuwa asilimia 50 ya watoto yatima katika jamii
wanalelewa na wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 60 hali ambayo inasababisha
wazee kuendelea kuishi maisha magumu na kunyanyasika na kupoteza haki zao za
msingi.
Hayo yamebainishwa juzi na mratibu wa Chama Cha Wataalam
Viongozi Wanawake wa Kilimo na Mazingira (TAWLAE) Eliasenya Nnko(PICHANI) wakati wa
kikao cha Waandishi wa Habari klichofanyika mjini Shinyanga kuhusu kuongeza na
uhamasishaji juu ya sera ya mikakati ya kuboresha maisha ya wazee nchini.
Nnko alisema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 80 ya wazee
wanaishi vijijini huku 50% ya watoto yatima wanatunzwa na wazee hususani wazee wanawake kutokana na vijana kutekeleza watoto wazo na kukimbilia mjini kwa
sababu mbalimbali ikiwemo kisingizo cha kutafuta maisha.
Alisema sababu nyingine ya watoto yatima kulelewa na wazee
ni kutokana na vifo vya wazazi vinavyotokana na magonjwa ya kuambukiza ikiwemo
UKIMWI.
Katika hatua nyingine alisema wazee nchini wanakabiliwa na
changamoto ya ukiukwaji wa haki za wazee kama vile mauaji na unyanyasaji wa
wazee ikiwemo kupoteza mali zao,kupigwa,kupuuzwa na kutolewa maneno ya kashfa
sambamba na kufukuzwa kwenye maeneo yao.
Nnko aliongeza kuwa bado wazee wanabaguliwa katika taasisi
za fedha kwa kunyimwa mikopo ama mitaji ingawa asilimia 63 ya ardhi yote nchini
inamilikiwa na wazee kitendo ambacho kinasababisha waendelee kuishi maisha
duni.
Alisema kikwazo kikubwa kinatokana na mtizamo hasi wa jamii
kwa wazee,sera ya matamko kuhusu wazee kutotungiwa sheria,kukosa uwakilishi
katika vyombo vya maamuzi na baadhi ya wenye mamlaka kutopenda kuwapatia wazee
hata yale yaliyo kwenye sera na miongozo ya taifa.
Kwa upande wake afisa Maendeleo ya Jamii na Vijana katika
halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Daudi Kisangure alisema katika kukabiliana
na suala la wazee kulea watoto yatima serikali inaendelea kutoa elimu kwa jamii
kuhusu kujiunga na vikundi vya uzalishaji mali ili kuwafanya vijana
wasikimbilie mjini bali wabaki vijijini kwani watakuwa na kipato.
Kisangure alisema changamoto kubwa katika kukabiliana na
masuala ya wazee katika wilaya ya Shinyanga ni ufinyu wa bajeti ukilinganisha
na makundi mengine kama vile vijana na wanawake ambao hutengewa asilimia 5 kupitia
mapato ya ndani ya halmashauri husika.
Naye mganga mkuu wa wilaya ya Shinyanga Dkt Emmanuel Kadelya
Joha alisema ili kumaliza tatizo la changamoto ya huduma za afya kwa wazee
tayari jumla ya wazee 3000 kati ya 11,000 wamepigwa picha na watapatiwa vitambulisho
katika awamu ya kwanza.
Alisema zoezi la kuwapatia wazee vitambulisho kwa ajili ya
matibabu ni endelevu na wazee wanaendelea kujaza fomu katika ofisi za vijiji na
kata ili kuhakikisha kuwa hawapati usumbufu wanapofika katika vituo vya afya na
hospitali.
Na Kadama Malunde-Shinyanga