Askofu mkuu wa kanisa la KKKT Dayosisi Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria Emmanuel Makala amesema
Chama Cha Mapinduzi kisipokuwa na umoja mwaka huu kitazikwa.
Askofu Makala aliyasema hayo juzi wakati akiweka wakfu kanda
ya Waona Nini kutoka kwaya ya Usharika ya KKKT Ebenezer kanisa kuu Shinyanga iliyozinduliwa
katika kanisa hilo ambapo viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa wakiongozwa na
mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM nchini Mgana Msindai walihudhuria.
Askofu Makala aliwataka wana CCM kudumisha amani ndani ya
CCM ili kuendeleza amani iliyopo nchini badala ya kuendeleza malumbano na
kwamba isipokuwa makini mwaka huu itazikwa.
“Nawaasa dumisheni
amani ndani ya CCM,dumisheni umoja,muwe kitu kimoja muongoze vizuri,msaidieni
rais naye ni mtu mnamtesa,msipokuwa makini CCM tutaizika mwaka huu,kila mtu
akitaka kuwa rais hatutafika mbali,hakuna nchi hii haiwezi kuongozwa na marais
wawili”,aliongeza Askofu Makala.
“Mimi siyo mwanasiasa lakini tumeapishwa kuwa na sauti za kinabii
na kuwaonya watawala kibiblia,kwa hiyo naomba sana kwa amani na ushirikiano
tulionao tuendelee kuulinda”,alisema Makala.
Katika hatua nyingine aliwataka viongozi wa siasa kutoona
aibu kuingia kwenye nyumba za ibada ili waombewe ili wawe waadilifu badala ya
kukimbilia kwa waganga wa kienyeji.
“Nendeni makanisani na misikitini muombewe,kiongozi mzuri ni
yule mwenye hofu na mungu,hatutaki kuwa na viongozi wezi na wenye madeni
,msione aibu kuja na hizo pesa mlizonazo msizifiche zileteni kwenye nyumba za
ibada hakuna atakayewafukuza”,aliongeza askofu Makala.
Makala alisema ili kuwe na amani nchini lazima watanzania
waheshimu mambo ya dini, akisisitiza waislamu na wakristo waachwe waabudu kwa uhuru na kuacha mambo ya ugomvi wa kidini.
Askofu Makala alisema watanzania wanatakiwa kudumisha umoja
na mshikamano walionao na kwamba amani haiwezi kuja kama hakuna uhusiano wa karibu
na mwenyeji mungu.
Katika hatua nyingine aliitaka jamii kuwapuuza baadhi ya watu wanaozusha
uvumi kuwa kanisa lake limejengwa kwa nguvu ya Freemasons.
“Kuna watu wanasema kanisa hili limejengwa na
Freemason,washindwe walegee kwa jina la yesu,kanisa hili limejengwa na sadaka
za wakristo wa kanisa hili na sio vinginevyo”,alisema askofu Makala.
Kwa upande wake mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM nchini Mgana
Msindai ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida aliyehudhuria uzinduzi
wa albam ya “Waona Nini” alisema Tanzania itaendelea kuwa na amani kutokana na
kwamba rais atakayepatikana ameteuliwa na mwenyezi mungu.
“Amani ya nchi hii itaendelea kuwepo kwani kiongozi
atakayepatikana ameteuliwa na mungu,sisi tunaamini rais atatokana na mapenzi ya
mungu hivyo watanzania wasiwe na wasiwasi wajiandae tu kupiga kura siku ya
uchaguzi kwani amani itakuwepo”,alisema Msindai.
Naye mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja aliwaomba
viongozi wa dini kuendelea kuiombea nchi ya Tanzania ili amani iendelee kubaki.
“Tanzania ni nchi yetu,sisi pia ni wadau wa amani,tunawaomba
viongozi wa dini kuendelea kutuombea na kuliombea taifa kwani amani itaendelea
kuwepo kutokana na ushirikiano miongoni mwetu”,alisema Mgeja.
Na Kadama Malunde-Shinyanga
Social Plugin